Friday, 21 January 2011

WATU WENYE ULEMAVU WAWEZESHWE KUKABILI SOKO LA AJIRA

Watu wenye ulemavu wawezeshwe kukabili soko la ajira

Achukizwa na ubaguzi wanaofanyiwa
Na Abdi Shamnah

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, amesema watu wenye ulemavu wawezeshwe kielimu ili waweze kutumia fursa za ajira zilizopo badala kukumbukwa kwenye upendeleo.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo huko Migombani alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar, ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzitembelea Idara zilizoko chini ya Ofisi yake.

Makamu huyo alisema tatizo la ajira ni kilio cha vijana nchini kote, hata hivyo serikali ina wajibu mkubwa kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata elimu ya kutosha ili waweze kutumia vyema fursa za ajira zilizopo.

Maalim Seif alisema lazima walemavu wawezeshwe katika kupewa haki na fursa za kielimu ili waweze kushindana kwenye soko la ajira kwa sifa walizonazo na si nafasi za kupendelewa.

Alisema lengo la serikali kuiona jamii ya Wazanzibari inapata haki na fursa sawa na wengine bila ubaguzi wa aina yeyote, iwe kwa misingi ya kimaumbile, jinsia au ukamilifu wa viungo.

Maalim Seif alisema elimu kwa jamii ya watu wenye ulemavu inawezekana, mbali na vifaa wanavyotumia kugharimu fedha nyingi.

Katika hatua nyingine Malim Seif, aliwapongeza walimu wa skuli ya msingi mjumuisho Kisiwandui, kwa kazi ngumu ya kuwaendeleza kielimu wanafunzi wenye mahitaji maalum, wakiwemo wasioona,viziwi pamoja na walemavu wa akili.

Wakati huo huo Maalim Seif alifanya mazungumzo na watendaji wa Jumuiya za Watu wenye Ulemavu, ambapo moja ya changamoto kubwa waliyonayo ni tatizo sugu la unyanyaswaji wa kijinsia dhidi yao.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya watu wenye Ulemavu wa Akili, Faudhia Haji Mwita, alisema sheria iliopo haitoi mwanga mzuri, kukiwa na kesi nyingi za vijana wenye ulemavu wa akili kubakwa.

Alifafanua nyingi ya kesi hizo zinapofikishwa Mahakamani , mapungufu ya kisheria hujitokeza na washitakiwa kuachiwa kwa kile kinachodaiwa ‘mdhuriwa kushindwa kujieleza’.

Aidha alisema vijana wenye ulemavu wa akili wanakabiliwa na changamoto kubwa paler wamalizapo skuli, kwa vile huwa hawana shughuli maalum za kufanya.

Makamu huyo pia alipata fursa ya kuzitembelea Jumuiya mbali mbali za watu wenye ulemavu, ikiwemo UWZ, Jumuiya ya wasioona, Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu na Kituo cha watu wenye Ulemavu na Maendeleo.

No comments:

Post a Comment