Thursday 6 January 2011

DK. SHEIN MAPINDUZI YAMEMKOMBOA MZANZIBAR KIAFYA.

Dk.Shein: Mapinduzi yamemkomboa Mzanzibari kiafya

• Ataka wataalamu, wananchi kuongeza uzalendo
• Asema SMZ inaandaa maslahi bora kwa watumishi
Na Mwantanga Ame
Alhamisi 6, Januari 2011

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wataalamu na wananchi wote wa Zanzibar kuongeza uzalendo wa kuitumikia nchi yao ili maendeleo zaidi yapatikane.

Dk. Shein alisema hayo huko Chuo cha Afya Mbweni kwenye hotuba ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa Majengo ya dakhalia kwa wanafunzi katika Chuo hicho, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa vijana na wataalamu wanaoenziwa na nchi yao kwa kupewa huduma mbali mbali ikiwemo elimu, kuitumikia wanapokuwa wataalamu kwa maslahi ya wote.

Alisema ni jambo lisilopendeza vijana kuondoka nchini na kwenda kutafuta kazi nchi nyengine, na kuacha kuitumikia Serikali yao ambayo imetoa fedha nyingi na gharama kubwa kuwasomesha hadi kufikia viwango walivyofika.

Alisema hali hiyo imesababisha upungufu wa wataalamu katika sekta mbali mbali nchini, zikiwemo zenye kuhusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi kama vile afya.

Alifahamisha kuwa dhamira ya serikali ni kutoa huduma bora kwenye sekta ya afya, hivyo itahakikisha suala la elimu linapewa kipaumbele sambamba na kuwaandalia mazingira mazuri kimaslahi watendaji wake ili waweze kubakia nchini.

Hata hivyo Dk.Shein ameeleza kwamba utaratibu unafanywa kuwashughulikia wale walioondoka nchini baada ya kusomeshwa, kushindwa kufuata mikataba ya kuitumikia nchi kama walivyoahidi.

Dk. Shein, aliwataka wanafunzi wa Chuo hicho kuzithamini nguvu zinazotolewa na serikali katika kuwaimarishia huduma muhimu za masomo yao na wafikirie kuwa wataalamu wazuri watakaohudumia wananchi wa Zanzibar.

Aidha alifahamisha kuwa serikali imeanza utaratibu wa kutoa ushawishi wa kuwarudisha nchini baadhi ya madaktari ambao waliondoka nchini kufuata maslahi mazuri kwengineko.

Alisema mpango huo utaiwezesha kuifanya kada ya utoaji wa huduma za afya kuimarika na kuirejeshea hadhi yake Zanzibar ya kuwa kituo bora cha utoaji wa huduma katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwemo ufanyaji wa operesheni kubwa na kuwa wa kwanza kwa kuwa na sheria ya afya mwaka 1905.

Dk. Shein, alisema serikali tayari hivi sasa inaupitia upya mfumo wa utumishi serikalini ambao utaweza kuangalia pamoja na maslahi ya wafanyakazi pamoja na kuweka mazingira bora ya kuwajibika kwa kuhakikisha kila sekta inakuwa na vitu muhimu vya kufanyia kazi

Alisema kinachohitajika hivi sasa ni kuwepo mabadiliko katika utoaji wa huduma za afya jambo ambalo linawezekana ili kuleta maisha bora kwa wananchi wa Zanzibar.

Aliwapongeza viongozi wa Wizara hiyo pamoja na baadhi ya wafadhili waliojitolea kujenga jengo hilo ikiwemo serikali ya Oman pamoja na Benki ya maendeleo ya Afrika (ADB).

Nae Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, alisema sekta ya fya Zanzibar imepiga hatua kubwa kwa kufanikiwa kujenga vituo vya afya vingi huku serikali ikiwasomesha madaktari wake.

Waziri huyo aliiomba serikali ifanye utaratibu wa kuwaajiri wanafunzi wanaohitimu masomo yao kwa haraka kwani ni moja ya jambo linalowafanya kukimbilia kutafuta ajira Tanzania bara.

Duni pia aliwataka wanafunzi wanaochukua masomo yao kuhakikisha wanabakia nchini.

Naye Balozi wa Oman, Majid al Abbadi, akitoa salamu zake alisema serikali yao chini ya utawala wa Sultan Qaboos itaendeleza udugu uliopo kwa kutoa misaada zaidi kwa serikali ya Zanzibar na watu wake.

Hata hivyo Balozi huyo aliwasihi wanafunzi wa Chuo hicho kuona baada ya kumaliza masomo yao wabakie kuitumikia nchi yao kwa vile serikali yao haipendezwi na tabia ya wanafunzi wa Zanzibar kukimbia nchi yao na lazima wawe wazalendo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Saleh Jidawi, alisema Chuo cha Mbweni hivi sasa kimepiga hatua na kimo katika matayarisho ya kujiimarisha kwa kutoa taaluma ya juu zaidi kufikia ngazi ya digrii.

Alisema hivi sasa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho imeongezeka kutoka wanafunzi 200 wa mwaka 2006 hadi kufikia 450 na 2010 wamefikia 980.

Katibu huyo alisema majengo ya Chuo hicho yanayofadhiliwa na serikali ya Oman yanagharimu dola za kimarekani milioni 2.363 ambayo yatakuwa na vyumba vya wanafunzi wa kiume na kike pamoja na wasimamizi.

Mapema Dk. Hakim Gharib Bilal, akitoa salamu za wanafunzi alisema Chuo hicho licha ya kuwa na mafanikio makubwa kinakabiliwa na matatizo ya maslahi madogo kwa walimu na matatizo makubwa ya kupata mikopo.

Katika sherehe hizo viongozi mbali mbali walishiriki akiwemo Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Dk. Balozi Seif Ali Iddi na Mke wa Rais, Mama Mwanamwema Shein na Mawaziri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano.

Sherehe za Mapinduzi zitaendelea tena leo ambapo viongozi mbali mbali wa serikali wanatarajiwa kufungua na kuweka mawe ya msingi ya miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment