Zanzibar yang’ara Sherehe za Mapinduzi
• Washerehekea bila kujali mvua, jua Amaan
Na Mwanajuma Abdi
WANANCHI wa Zanzibar bila ya kujali hali ya hewa, na itikadi zao za kisiasa, jana walifurika kwenye sherehe za kutimiza miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Sherehe hizo zilifanyika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliwaongoza wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwenye maadhimisho hayo.
Sherehe zilizofanyika jana ziliendelea kuziweka pembeni itikadi za kisiasa walizokuwa nazo Wazanzibari na kuendelea kujenga utamaduni wa umoja kwani wafuasi wa vyama vyote vya siasa walikuwa wakishereke huku nyimbo za kuyasifia Mapinduzi zikiwatoka.
Mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yalianza na jua lililoambatana na joto kali majira ya asubuhi, na baadae kufuatiwa na mvua ndani ya kiwanja hicho hayakuwazuia wananchi hao kusherekea kwa jinsi wapendavyo.
Wakiwa kwenye hali ya utulivu kiwanjani hapo, wananchi walikuwa wakiimba nyimbo za Mapinduzi huku pia wakipata midundo ya brass bendi za vikosi vya ulinzi na usalama.
Shangwe lilianza baada ya kuanza kuingia kwa viongozi mbali mbali wakiwemo viongozi wa wastaafu ambapo kila walipokuwa wakiingia wananchi hao waliwashangiria.
Dk. Shein aliingia kiwanjani hapo huku msafara wake ukiongozwa na mapikipiki ambapo vikosi vya ulinzi na usalama vilimpa heshima yake na kupigwa mizinga 21.
Kumalizika kwa tukio hilo, kulifuatiwa na vikosi hivyo kupita mbele ya mgeni rasmi kwa gwaride, ambalo lilipita kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka.
Wananchi hao walivishangiria vikosi hivyo kila vilipokuwa vikionesha ueledi wa kuchapa mguu na kucheza gwaride hilo kwa umahiri.
Utamu zaidi wa sherehe za jana ulinogeshwa na maandamano ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar ambao walipita mbele ya mgeni rasmi huku mvua ikinyesha wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wakishindikizwa na ngoma za utamaduni.
Usiku wa kuamkia jana wananchi wengi katika mji wa Zanzibar walilazimika kulala usiku mkubwa kusubiri upigwaji wa fash fash pamoja na mizingira.
Sherehe hizo zilihudhuriwa viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Jamhuri wa Muungano Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Viongozi wa kitaifa, viongozi wa vyama vya siasa na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.
Wakati wa mchana viongozi hao walishiriki katika dhifa ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, Ikulu Mjini Zanzibar.
Thursday, 13 January 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment