Thursday 13 January 2011

DK. SHEIN TUSIKUBALI KUVUNJIWA UMOJA , AMANI ILIYOPO

MAADHIMISHO MIAKA 47 MAPINDUZI

Dk.Shein: Tusikubali kuvunjiwa umoja, amani iliyopo
• Mabadiliko makubwa yaja utumishi wa umma
• Huduma bora bila ubaguzi ni haki ya kila mwananchi
Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inajiandaa na mabadiliko makubwa ya utumishi wa umma na kuendeleza mambo ya msingi kwa kulibakisha suala la kusimamia ardhi kuwa mali ya serikali na utoaji huduma ya afya na elimu bila ya ubaguzi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika uwanja wa Amaan Mjini Unguja.

Dk. Shein, alisema malengo ya Mapinduzi yaliyowekwa 1964, likiwemo la kusimamia ardhi, utoaji huduma za elimu na Afya kutolewa bila ya ubaguzi kwa wananchi wa Zanzibar huku serikali ikijiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya utumishi wa umma.

Alisema serikali inajiandaa kutekeleza mpango huo baada ya kukamilika kwa sheria mpya ya utumishi wa umma yenye lengo la kuleta ufanisi kazini ili kuwafanya watumishi wa umma kupata huduma bora wananchi bila ya upendeleo.

Dk. Shein alisema mapendekezo hayo ya sheria yatafikishwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, katika kikao cha karibuni ambapo pia itaangalia suala la kuwapa haki wafanyakazi kutokana na kutimiza wajibu wao.

Alisema serikali inachukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya kuweka vyema maadili ya utumishi wa umma ambapo awamu ya saba inakusudia kulisimamia hilo kwa watendaji waliopewa majukumu ya kutumikia umma kuanzia ngazi ya viongozi waliochaguliwa walioteuliwa na watumishi wa kawaida.

"Huduma bora yenye kutolewa kwa msingi ya uadilifu ni haki ya wananchi wote ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma nzuri na kwa uadilifu serikali ya awamu ya saba itatekeleza mpango mkubwa wa mabadiliko katika utendaji wa utumishi wa umma" alisema Dk. Shein.

Alisema malengo ya serikali yatafikiwa kutokana na ishara zilizojionesha kuwepo mafanikio kupitia mpango wake wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUZA), ikiwa ni hatua ya kutekeleza malengo ya milenia na ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya dira ya 2020.

Alisema sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa zimeiwezesha serikali kuongeza pato la taifa pamoja na kupanuka kwa huduma za usafirishaji, mawasiliano, uimarishaji wananchi, kuongezeka kwa kiwango na ubora wa elimu, huduma za afya, kuimarika miundombinu, huduma za ustawi wa jamii pamoja na demokrasia na utawala bora.

Alisema serikali inafurahia kuona kiwango cha mapato kimeongezeka kufikia asilimia silimia 17 kutoka mwaka 2008 hadi 2009 na kuonesha ukuaji wa uchumi kukua kwa asilimia 7.

Dk Shein alisema eneo jengine ambalo serikali italiangalia ni la miundombinu kwa kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ambazo zinaendelezwa Unguja na Pemba zenye kilomita 247.4 zitazojengwa ndani ya miaka mitatu ijayo ambazo zitakuwa na urefu wa kilomita 152.9 huku ikizijenga barabara za maeneo ya kilimo na mjini na vijijini.

Akiiyataja maeneo mengine ambayo serikali inakusudia kuyafanyia kazi, Dk. Shein alisema ni kuimarisha uwanja wa ndege wa Zanzibar kuongeza utoaji wa huduma bora za mawasiliano ya simu kupitia mtandao wa mkonga wa baharini wa mawasiliano ya haraka mabapo utaweza kusaidia kukuwa kwa mawasiliano.

Alisema sekta ya umeme imeonesha mafanikio makubwa ndani ya miaka 47 ya mapinduzi ambapo imewapatia wananchi huduma zake kwa asilimia 90 lakini bado serikali inakabiliwa na changamoto ya kuona huduma hiyo inawafikia wananchi kutokana na baadhi yao kutomudu gharama za kuunganisha.

Katika maandalizi hayo, Dk. Shein, alisema serikali pia inakusudia kuweka sheria ya viwango itakayowasilishwa barazani katika kikao kijacho pamoja na sheria ya biashra ya mwaka 2006 kufanyiwa maptio.

DK. Shein alisema serikali itahakikisha inalinda haki za binadamu pamoja na kukabiliana na baadhi ya changamoto kufikiwa kuondoa kero za Muungano.

Ili kufanikisha malengo hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuogeza ushirikiano na serikali yao kwa kutoa mchango wao katika kuhakikisha wanalinda amani ya nchi na kujenga mshikamano.

Mapema Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi Aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki sherehe hizo na kuwataka kuendelea kudumisha amani ya nchi.

Kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi, kilihudhuriwa na vongozi kadha akiwemo Rais Jakaya Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

Wengine ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine ni Marais wastaafu akiwemo Dk. Amani Karume,Mzee Ali Hassan Mwinyi, Dk.Salmin Amour, Waziri kiongozi mstafu Shamsi Vuai Nahodha, Ramadhan Haji Faki, Waziri mkuu mstaafu Tanzania Edward Lowasa, Frederick Sumaye, pamoja na mabalozi wa nchi mbali mbali nchini Tanzania na watendaji wakuu wa mawizara ya serikali ya Zanzibar na Muungano.

No comments:

Post a Comment