Monday 10 January 2011

MBUNGE ATAKA KUFICHULIWA WAPORA SILAHA

Mbunge ataka kufichuliwa wapora silaha

Na Jumbe Ismailly,Manyoni
Jumanne 11, Januari 2011

WAKAZI wanaoizunguka hifadhi ya taifa ya wanyamapori ya Rungwa, tarafa ya Itigi, wilayani Manyoni, wametakiwa kuwafichua wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya kupora silaha za askari wa wanyamapori.

Mbunge wa jimbo la Manyoni Magharibi (CCM), John Paulo Lwanji, waliwito huo kwenye sherehe za kupongezwa na wananchi wa kata ya Rungwa kufuatia kushinda kiti hicho katika jimbo hilo.

Mbunge huyo alisema suala la kufichuliwa kwa wapora silaha hao ni la lazima kwani wananchi ndio wanaowafahamu kwani wanaishi nao kwenye jamii.

Alisema kumezuka vitendo vya uporaji wa bunduki zinazotumiwa na askari wa wanayapori, vitendo vinavyohatarisha maisha ya askari, wanyamapori na raia wema.

Mbunge Lwanji aliwataka wananchi kutowaficha waporaji wa silaha hizo, kwani wanachofanya ni kitu chenye kuhatarisha amani na usalama sio wa wanyama bali pia wa wananchi.

"Mwaka jana kuna watu walichana hema la mtalli mmoja na kumwibia vifaa vyake vya uwindaji, hivi juzi tena kumetokea tukio la askari wanyamapori kuporwa bunduki, vitendo hivi vinaleta picha mbaya sana katika hifadhi”, alisema Mbunge huyo.

Alisema matukio kama hayo yakiendelea yanaweza kupunguza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo ambapo pato la taifa nalo litaporomoka.

“Mnaweza mkafika mahali mkailazimisha serikali kuhamisha vijiji vyenu na hapo mtakuwa mnajikosesha wenyewe faida lukuki zinazotokana na uwindaji wa kitalii", alisema Lwanji.

Aidha alisema zoezi la kuwafichua waporaji wa silaha halina budi liende sambamba na kuwafichua wawindaji wote haramu (majangili), ili na wao waweze kushughulikiwa kikamilifu na kwa mujibu wa sheria zilizopo.

No comments:

Post a Comment