Saturday, 22 January 2011

PINDA AWATAKA WABUNGE CCM KUSHIKAMANA

Pinda awataka Wabunge CCM kushikamana

Na Mwandishi Maalum

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM amewataka wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na umoja na kuacha malumbano kwani kwa kufanya hivyo wataiyumbisha nchi.

Pinda ametoa rai hiyo jana asubuhi (Jumamosi, 21 Januari 2011), alipofungua semina ya siku tatu ya wabunge wa CCM iliyoanza jana hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema lengo la semina hiyo ni kuwasaidia wabunge watambue wajibu wao wakiwa Bungeni. “Mada kuu ya jana ni Kanuni za Kamati ya Wabunge wa CCM na kesho tutajadili wajibu wa Wabunge wa CCM katika Bunge la Vyama Vingi, na hii itaendelea hadi Jumatatu,” alisema.

Akihimiza kuhusu ushiriki wao Bungeni, Waziri Mkuu alisema: “Kila mbunge anapaswa kusoma vizuri Kanuni za Bunge na kuzielewa ili waweze kuchangia kwa umakini mijadala ya bungeni. Kila mbunge ana wajibu wa kuhudhuria vikao vyote vya Bunge na kipimo kizuri cha Mbunge ni jinsi anavyoweza kuchangia mijadala katika Bunge…”.

Aliwataka wabunge hao wawe wepesi kusoma machapisho na kufanya tafiti ili waweze kuwa na hoja nzito wakati wanapotoa michango yao Bungeni.Alitumia fursa hiyo kuwahimiza mawaziri wote wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kuwa makini na ratiba za vikao vya Bunge ili wahakikishe wanakuwepo bungeni katika kipindi chote cha Bunge.

Pia alimshukuru Spika wa Bunge, Anna Makinda kukubali ofisi ya Bunge igharimie semina hiyo pamoja na semina nyingine ambazo zitafanyika kwa wabunge wa vyama vingine.

Alisema leo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete atahudhuria semina hiyo na kwamba anatarajiwa kuifunga Jumatatu mchana.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Pinda ameahidi kutoa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuchangia ununuzi wa kompyuta 24 zinazohitajiwa na kituo cha kulea watoto yatima cha SOS kilichopo barabaraya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam.

Pinda alitoa ahadi hiyo alipotembelea kituo hicho na kukagua miundombinu ya kituo hicho ikiwemo pia madarasa ya shule ya awali pamoja na nyumba wanazoishi watoto hao.

Waziri Mkuu alitoa mchango huo baada ya kuelezwa kuwa kituo hicho kina mpango wa kuanzisha darasa maalum la kompyuta (computer lab) ili watoto hao waweze kupata mafunzo ya teknolojia ya habari (IT) na kwamba kituo kinahitaji kompyuta 24.Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu katika kituo hicho. Mkurugenzi wa Taifa wa SOS Children Villages, Rita Kahurananga, alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika hilo lina vituo vingine kama hivyo huko Zanzibar na Arusha na kwamba wana mpango kuanzisha vituo vingine Iringa, Bagamoyo na Mtwara ifikapo mwka 2016.

Naye Mkurugenzi wa Kijiji hicho, Dk. Alex Lengeju alimweleza Waziri Mkuu kwamba kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji 500 vya SOS vya kulea watoto yatima vilivyopo katika nchi mbalimbali duniani ambavyo vinatumia mfumo wa familia mbadala.

“Inaumiza kuona watoto wakiishia mitaani, tunachofanya ni kuwachukua watoto ambao hawana ndugu kabisa, tukiwaleta hapa wanaishi watoto 10 katika nyumba moja chini ya uangalizi wa mlezi ambaye ndiye mama wa familia hiyo, wanakuwa na kaka na dada wa familia miongoni mwao… tunawalea wakitambua mfumo wa kuishi kama familia na kuishi kama wanakijiji wakitambua uwepo wa majirani zao,” alisema.

Alisema kijiji hicho kina nyumba 13 zenye uwezo wa kuchukua watoto 130 lakini hadi sasa wana watoto 123 ambao wanasoma shule mbalimbali za jijini lakini wengi wao wako shule ya awali iliyopo ndani ya kijiji hicho. “Shule ya awali ina watoto 83 wenye miaka kati ya mitatu na sita ambao 55 kati yao wanatoka familia za jirani hapa Mwenge na Sinza.”

Alisema Kijiji cha SOS kimeanzisha pia Mpango wa Kuimarisha Familia (Family Strengthening Programme) kwa kutoa huduma kwa walengwa wanaoishi nje ya kituo hicho kwa kuwalisha, kuwaelimisha na kuwaandaa wajitegemee kimaisha na kwamba hadi sasa wanahudumia watoto 200 na watoa huduma 53.

Alisema kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo kwenye jamii, wana mpango wa kuhudumia watoto 1,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Alisema kutokana na majukumu hayo, kama watapata eneo la kutosha, kituo kina mpango wa kujenga shule ya msingi, shule ya sekondari, shule ya ufundi na hospitali ambavyo alisema vitatoa huduma kwa jamii inayowazunguka.

No comments:

Post a Comment