Monday, 24 January 2011

WAKAGUZI KUTUMWA KUCHAKACHUA HESABU ZFA.

 Wakaguzi kutumwa kuchakachua hesabu ZFA

 Wizara yakiri kuwepo ukiukwaji katiba, ubabaishaji
Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, imesema inakusudia kupeleka wakaguzi wa hesabu katika ofisi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ili kupitia matumizi na taratibu zote za kifedha ndani ya chama hicho.

Waziri wa wizara hiyo Abdilahi Jihad Hassan, alisema hayo alipokuwa akijibu suala la nyongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Nassor Salum Ali 'Jazeera', kwenye kikao cha jana asubuhi.

Mwakilishi huyo alitaka kujua hatua zilizochukuliwa na wizara hiyo dhidi ya Katibu Mkuu wa ZFA ambaye alimtaja kuwa ndiye anayepaswa kubeba dhima juu ya mizengwe iliyofanyika katika chama hicho kufuatia uchaguzi wake mkuu.

Akizungumzia kadhia hiyo, Jihad alikiri kuwa kuna matatizo mengi katika uendeshaji wa kazi za ZFA, hasa mambo yahusuyo fedha, hivyo akasema wizara yake itapeleka wakaguzi wa hesabu katika ofisi zote za chama hicho Unguja na Pemba.

Aidha alibainisha kuwa wizara yake inafahamu kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa katiba katika utendaji wa chama hicho, pamoja na kuendesha vikao bila kufuata taratibu.

Hata hivyo, alisema baada ya Ofisi ya Mrajis kuingilia kati kadhia hiyo na kutumia uwezo iliopewa kisheria, iliamua kusimamisha mara moja uchaguzi mkuu wa marudio ambao ZFA ilipanga ufanyike Januari 19, huko Nungwi Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

"Kwa mamlaka aliyopewa katika kifungu cha sheria namba 19 (a,b,d), Mrajis ameamuru uongozi wa zamani urudi madarakani na kwamba shughuli zote zifanyike kwa maandishi na kuwasilishwa kwake, kwa sasa mambo yanakwenda, tusubiri uchaguzi ufanyike kati ya wiki ya mwisho ya Februari na mwanzoni mwa Machi", alieleza Waziri Jihad.

Alieleza katika hali ya sasa ambapo ZFA inaendelea na kazi zake kwa agizo la Mrajis kuwarudisha viongozi wa zamani, wizara yake imeona iendelee kuupitia kwa kina mgogoro huo ambao kwa kiasi kikubwa unamuhusu Katibu Mkuu kabla haijaamua kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kumuondosha kama wengi wanavyopendekeza.

Chama cha Soka Zanzibar kilikumbwa na mtafaruku mkubwa tangu baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Pemba Januari 31, kufuatia Rais aliyeshinda Ali Ferej Tamim kukatiwa rufaa kwa madai ya kutowasilisha cheti cha elimu ya sekondari, hali iliyoibua pia matatizo mengine ambapo ilibainika baadhi ya wajumbe waliopiga kura hawakustahiki.

No comments:

Post a Comment