Thursday 6 January 2011

BALOZI SEIF ATAKA WATOTO WASRITHISHWE ELIMU.

Balozi Seif ataka watoto warithishwe elimu

Asema itawajengea mustakbali mwema
Na Mwantanga Ame
Alhamisi 6 Januari 2011.

MBUNGE wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi amewaasa wazazi na walezi kusimamia vyema elimu kwa watoto wao.

Balozi Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema hayo alipokuwa akiwakabidhi wananchi wa Jimbo la Kitope zaidi ya shilingi milioni 4.8, ikiwa ni hatua ya kuchangia harakati za maendeleo jimboni humo.

Alisema hakuna urithi mzuri wa kuwapa watoto kama elimu, hivyo wazee na walezi wana jukumu la kuwasimamia vijana wao waweze kuipata elimu ambayo itawaongoza kwenye maisha yao.

Balozi Iddi alisema suala la elimu ni moja ya jambo la msingi hivi sasa na ni vyema kwa wazazi kuthamini michango inayotoa kwa kuhakikisha wanawahimiza watoto wao kujisomea zaidi.

Alisema anatoa mchango huo ambao utasaidia kuvuta umeme katika skuli ya Mgambo kutokana na hivi sasa wanafunzi wa skuli hiyo kupata tabu hasa pale wanapotaka kuweka kambi ya masomo wakijitayarisha na mitihani.

Mbunge huyo aliwataka wazazi kuitumia fursa hiyo kwa kuhakikisha wanawaasa watoto wao kuona washiriki katika masomo kwani haitapendeza baada ya huduma ya umeme kuwapo skuli hiyo ikawa haifanyi vizuri katika mitihani ya taifa.

"Dunia ya sasa ni elimu, nyumba unaweza kumrithisha mtoto wako lakini elimu huwezi kumrithisha ukifa unaondoka nayo, sasa haitapendeza baada ya sisi kufanya jitihada hizi kisha huku wazazi mkashindwa kuwahimiza watoto wenu kusoma na kila mkifungua mabuku yao mkaona mayai yametawala hivi sivyo", alisema Balozi Iddi.

Alisema uongozi wa Jimbo hilo kwa kutambua umuhimu wa elimu utahakikisha kila panapohitaji kutolewa msaada inafanyika kwa vile ni moja ya nguzo muhimu itayolifanya jambo hilo kuwa na maendeleo zaidi.

Nae Mwakilishi wa Jimbo hilo Makame Mshimba, aliwataka wananchi kushiriki katika vikao vya kamati za maendeleo ili kuelezea matatizo yao badala ya kukimbilia katika vyombo vya habari.

Alisema hatua ya wananchi kudai maendeleo katika vyombo vya habari ni inamsikitisha sana na kumuumiza moyo kwa vile tayari wamekuwa wakiitisha vikao vya kutaka wananchi kutoa maoni yao juu ya kero zinazowakereketa lakini jambo la kusikitisha kuona hawajitokezi.

Katika ziara hiyo, Balozi alikabidhi shilingi 700,000 ambazo zitatumika kuungia umeme katika skuli ya Mgambo, ambapo huko Upenja alikabidhi shilingi 400,000 za kumalizia ujenzi wa jengo la skuli.

Eneo jengine ambalo Balozi alitimiza ahadi yake ni pamoja na kuwapatia Kamati ya siasa ya Kaskazini 'B' shilingi 360,000 ikiwa ni kukamilisha shilingi 2.5 milioni zilizotumika kwa ajili ya ujenzi tawi la CCM la Kitope 'B'.

Fedha nyengine ambazo alitoa ni kwa kikundi cha Ulezi kazi ambapo aliwapatia shilingi 200,000 huku akiwapatia waananchi wanne shilingi 400,000 waliounguliwa nyumba zao baada ya kuzuka moto usiojulikana chanzo chake.

Sheha wa Shehia hiyo, Maulid Masoud, akielezea tukio hilo alisema hadi sasa wanaendelea kulifanyia uchunguzi kwa vile linaonekana uchunguzi wake kuwa ni wenye kutatanisha.

No comments:

Post a Comment