Friday, 21 January 2011

TANZANIA KUIANDALIA SERA YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA

Tanzania kuiandalia sera Teknolojia ya Nyuklia

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Tanzania inajiandaa kutayarisha sera ya Teknologia ya Nyuklia ambayo itaiwezesha nchi kutumia nishati hiyo kwa shughuli za kimaendeleo.

Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknologia Tanzania, Dk. Raphael Chibuuda alieleza hayo alipokuwa akizungumza na uongozi Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Alisema dhamira ya serikali ya kutayarisha sera hiyo itahakikisha kuona nishati hiyo inasaidia katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo kilimo, nishati, elimu na hospitali ambapo hivi sasa wamekuwa wakitumia nishati hiyo katika mionzi.

Naibu huyo alisema Tanzania imekuwa ikitumia nishati hiyo ya nyuklia kwa kiasi kidogo kutokana na kutokuwa na sera mahususi ambayo inasimamia matumizi salama ya nyuklia kwa maendeleo ya jamii.

Aliwatoa hofu wenye hofu ya kutumika vibaya kwa teknolojia hiyo na kueleza kuwa lengo ni kusukuma mbele maendeleo ya taifa.

Alisema ghofu ambayo ilijitokeza nchini Irani baada ya kuamua kutumia nishati hiyo haina haja ya kulinganishwa na dhamira ya Tanzania katika matumizi ya nishati hiyo kwani hivi sasa tayari inatumia nishati hiyo katika shughuli za utibabu.

Aidha, Dk. Raphael alisema, taasisi yake imeamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni moja ya mipango itayoweesha kukuza shughuli za kisanyasi ambapo mbali ya sera hiyo pia inajiandaa na sera ya Mawasiliano ya simu (ICT).

Alisema sera hiyo lengo lake ni kuona mawasiliano ya simu yanawekewa mazingira mazuri kutokana na hivi sasa kuimarika huku makampuni ya simu yakionekana kutokuwa na muongozo imara.

Kutokana na mipango hiyo Dk. Raphael, alisema ipo haja kwa kitengo cha utafiti katika Chuo Kikuu cha Taifa SUZA kikajiimarisha zaidi kwa vile kinachoonekana hivi sasa kutokuwa tayari kwa watu kujituma kufanya tafiti kwa visingizo vya ukosefu wa fedha.

Alisema ni kweli sababu hiyo ipo lakini haina haja ya kuwafanya kuacha kutayarisha tafiti kwa vile tafiti zenyewe zikifanyia zinauwezo mkubwa wa kuwaingizia fedha kutokana na kila tafiti itayofanywa inakiwango cha asilimia nane kwa fedha zitazotengwa kwa utafiti mzima.

Dk. Raphael, aliwataka wasimamizi wa Chuo hicho kuona wanakuza utafiti wa sayansi kwani Zanzibar ipo chini katika kufanya tafiti za aina hiyo, huku watafiti wake kushindwa kutumia masoko ya nje na badala yake kubakia wakisubiri tafiti za hapa nchini pekee.

Nae Mkurugenzi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknologia Tanzania Hassan Mahmoud Mshunda alisema Chuo Kikuu cha Taifa SUZA kitapewa nafasi ya kipekee kuona inawasomesha zaidi walimu wake na wanafunzi wataotaka kujiunga na fani ya utafiti ambapo hivi sasa tayari wizara hiyo imewasomesha Wazanzibari watano.

Mkurugenzi huyo alisema matatizo yaliowahi kujitokeza ya kuwapo kwa malalamiko ya kutopewa nafasi za masomo kwa Wazanzibari waliowahi kuomba Wizara yake itayashughulikia kuona hayatatokea tena.

“Kwa hili nduguzanguni ninawaombeni radhi kwani aliefanya hivi naamini hakufahamu nini majukumu yetu sasa ninachokuombeni leteni maombi yenu na tutayafanyia kazi kwani tayari tuna Wazanzibari watano tumeshawapa nafasi hizo”, alisema Mkurugenzi huyo.

Kauli ya Mkurugenzi huyo imekuja baada ya mmoja Mkurugezi wa Utafiti katika Chuo Kikuu cha SUZA, Dk. Mohammed Ali Sheikh, kuueleza uongozi wa wizara hiyo wa kuwapo kwa matatizo yaliowahi kumkuta ya kukataliwa ruhusa ya fedha za kufanya utafiti ambao aliomba kwa Wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment