Friday 14 January 2011

WAELIMISHENI WACHONNGA MATOFALI KUHIFADHI MAZINGIRA -- FEREJ

Waelimisheni wachongaji matofali kuhifadhi mazingira - Ferej



Na Raya Hamad, OMKR

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej, ameitaka Idara ya Mazingira Pemba, kuwapatia elimu wachongaji wa matofali ili kuokoa maeneo mengine yasiendelee kuharibiwa.

Waziri huyo alitoa agizo hilo alipotembelea eneo la Kwareni Vitongoji ambalo ni maarufu kwa uchongaji wa matofali na kujionea hali mbaya ya uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

“Naelewa kuwa tayari kuna watu wengi hasa vijana wanaendesha maisha yao na kujipatia rizIki kupitia sehemu hii, inakuwa vigumu kutoa uamuzi wa haraka kuwahamisha vijana, lakini kwa hatua ya mwanzo lazima Idara ya Mazingira mchukue jukumu la kuwapa taaluma juu ya namna gani wanapaswa kuendeleza shughuli zao bila ya kuathiri mazingira”, alisisitiza Fatma.

Aidha waziri huyo aliwataka wachimbaji hao kuhahakikisha wanafuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa Mazingira juu ya namna ya uchongaji wa matofali na kufukia mashimo mara wanapomaliza shughuli zao.

Waziri huyo alisema njia bora ambayo inaweza kutumiwa na wachongaji wa matofali hayo ni kupanda miti ya kutosha ikiwemo migomba, kudumisha usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi pamoja na kujali afya zao.

Nae Mwenyekiti wa eneo hilo la Kwareni, Kombo Ali Abdalla maarufu Mbunge, alisema Idara ya Mazingira imekuwa ikiwapatia mafunzo ambayo yamekuwa yakiwasaidia kufanya shughuli zao kwa uangalifu tofauti na awali.

Moja kati ya mambo ambayo walitakiwa kuyatekeleza ni kuyafukia mashimo na baadae kupanda miti kama mivinje, migomba, na bustani za mbogamboga jambo ambalo tayari wameshaanza kulitekeleza.

Aidha alisema wapo tayari kuachana na kazi hiyo endapo watapata miradi mbadala itakayowawezesha kuendesha maisha yao.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Ali Juma Hamad, alisema wamewapatia miongozo wachimbaji hao ambayo itasaidia kupunguza uharibifu uliopo ikiwa ni pamoja na shimo moja kutozidi mita tano.

“Hii ni maliasili na watu wanaitumia tumewapa muongozo wa uchimbaji wanapochimba shimo basi lisizidi mita tano kwenda chini, kufanya hivyo kuna uwezekano wa kupasua mwamba na maji yakaingia katika mashimo na hivyo kusababisha maafa tusiyoyatarajia”, alisema Mkurugenzi huyo.

Takriban zaidi ya watu 4,000 wamejiajiri katika eneo hilo ambalo limejitenga na mji wakiendesha shughuli za uchimbaji wa udongo na kuchonga matofali ya ujenzi.

No comments:

Post a Comment