Friday, 14 January 2011

PAKISTANI KULETA UJUMBE MAALUM ZANZIBAR

Pakistani kuleta ujumbe maalum Zanzibar

 Kuangalia maeneo ya uwekezaji, utalii

Na Rajab Mkasaba

NCHI ya Pakistani imesema itazidisha uhusiano wake wa kihistoria na Zazibar, ambapo imeazimia kuleta ujumbe maalum kuangalia maeneo ya kuwekeza pamoja na utalii.

Balozi wa Pakistani nchini Tanzania, Tajammul Altaf aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

Balozi Altaf alimueleza Dk. Shein kuwa Pakistani italeta ujumbe huo ambao utakuja kuangalia maeneo ya uwekezaji kwa lengo la kukuza biashara kwa maslahi ya wananchi wa nchini hizi.

Aidha Balozi Altaf, alisema Pakistani itainga mkono Zanzibar kwenye mpango wake wa kukifufua kilimo, ili kiweze kuleta mafanikio zaidi katika kuchangia uchumi wa Zanzibar.

Alisema Pakistani imeamua kuiunga mkono Zanzibar kwenye kilimo kutokana na kuwepo mpango mzuri wa kukiimarisha kilimo cha umwagiliaji maji.

Sekta nyengine ambao Balozi huyo alisema nchi yake inaweza kuisaidia Zanzibar ni suala zima la utafiti ambalo ndiyo nguzo na chachu kubwa ya kuendeleza taifa kimaendeleo.

Balozi Altaf alisema Pakistani, itatoa nafasi za masomo kwa Wazanzibari kwenda nchini humo kwa ajili ya kujifunza kada mbali mbali za kitaaluma.

Balozi Altaf alisema kuwa nchi yake inaona umuhimu mkubwa wa kushirikiana pia, katika sekta ya biashara kwa kutambua kuwa Zanzibar nayo ina uzoefu mkubwa katika sekta hii na kueleza umhimu wa kushirikiana pamoja kati ya wafanyabiasahara na wenye viwanda wa hapa Zanzibar na Pakistan.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walizungumza juu ya uimarishaji wa Chuo cha afya Mbweni ambapo Balozi Altaf alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake iko tayari kusaidia uimarishaji wa Chuo hicho.

Aidha Balozi huyo alitoa salamu za pongezi kwa Dk. Shein kwa kufanikisha vyema sherehe za miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika hivi karibuni.

Nae Dk. Shein alimpongeza Balozi Altaf wa Pakistani kuwa Zanzibar ina uhusiano wa kihistoria katika sekta mbali mbali za kiuchumi na huduma za kijamii.Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar imo katika mchakato mzima wa kuimarisha sekta ya kilimo hasa kilimo cha umwagiliaji maji na kusisitiza kuwa kutokana na Pakistani kupiga hatua katika sekta inaweza kuisaidia sana Zanzibar.

Alisema kuwa juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha kilimo kinapewa kipaumbele kwa kuweza kukiimarisha zaidi kwa kuwepo vitendea kazi vya uhakika ikiwemo matrekta.

Alisema kuwa mbali ya uimarishaji wa sekta hiyo pia, serikali ina mpango wa kukiimarisha zaidi chuo chake cha kilimo kilichopo Kizimbani kwa kusomesha masomo ya Diploma na hata Diploma ya juu ili kuweza kutoa wataalamu wazuri wa kuweza kusaidia kuimarisha sekta hiyo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa suala la utafiti pia, limepewa kipaumbele na serikali yake anayoiongoza na kumuhakikishia Balozi Altaf kuwa juhudi za makusudi zinachukuliwa katika kuhakikisha utafiti unapewa kipaumbele katika sekta zote.

Dk. Shein alisema kuwa serikali imekusudia kukiimarisha chuo cha Afya kilichopo Mbweni, ili kiweze kutoa kada zaidi za masomo na kueleza matumaini yake makubwa iwapo nchi hiyo itasaidi kukiimarisha chuo hicho kutokana na mafanikio na uwelewa zaidi juu ya sekta ya afya.

Katika maelezo hayo, pia Dk. Shein alimueleza Balozi huyo wa Pakistan kuwa Zanzibar imo katika uimarishaji wa sekta yake ya uwekezaji na kueleza kuwa inawakaribisha waekezaji na wafanyabiashara wa Pakistan kuja kuekeza katika sekta ya utalii, biashara na sekta nyenginezo.

No comments:

Post a Comment