Mfungwa wa Russia afariki Zanzibar
Na Khamis Amani
RAIA mmoja wa Russia, aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar amefariki dunia.
Inarserger Othirov, amefariki dunia Januari 9, mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja ambapo alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa za Daktari kutoka Hospitali hiyo ya Mnazimmoja, marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya homa, kifua kikuu (TB), pamoja na uvimbe uliojaa maji katika pafu lake la upande wa kulia.
Staff Ofisa wa Vyuo vya Mafunzo, Makao Makuu Kilimani wilaya ya Mjini Unguja, Makame Kombo Ame, alithibitisha kutokea kifo cha mwanafunzi huyo wa Chuo cha Mafunzo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake, Staff Ofisa huyo, huyo alisema kuwa, marehemu amefariki siku tisa mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo kwa matibabu.
Alisema kuwa, kabla ya kifo chake Ivan Ochirov kama jina lake la umaarufu alilokuwa akijulikana nalo Chuoni humo, alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Chuoni humo, lakini baadae alilazimika kupelekwa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja baada ya hali yake kuwa mbaya.
Akiwa hospitalini hapo kwa matibabu, Januari 9 mwaka huu majira ya saa 12:15 za asubuhi Ivan alifariki dunia, kwa mujibu wa Staff Ofisa huyo.
Alifahamisha kuwa, mara baada ya kifo hicho mwili wake ulikabidhiwa wazee wake wote wawili waliokuwepo hapa nchini, chini ya usimamizi wa Balozi wa Russia nchini Tanzania kwa taratibu za mazishi.
Kwa mujibu wa Staff Ofisa huyo, mazishi ya marehemu huyo yalifanyika Zanzibar saa nane mchana, katika ufukwe wa pwani ya Migombani ngazi mia, kwa kuuchoma moto mwili wa marehemu huyo.
Ivan alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi wawili wanaotumikia kifungo cha maisha Chuo hicho cha Mafunzo, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi kijana mwenzao raia wa Russia kwa kumchoma moto, tukio ambalo lilitokea Zanzibar mwaka 1998.
Kabla ya adhabu hiyo, Ivan na mwenzake huyo (jina halikupatikana), ambaye naye pia ni raia wa Russia, Mei 31, 2001 walihukumiwa kutumikia Chuo hicho kwa muda wa miaka 15, baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila ya kukusudia katika kesi ya jinai namba 14/1998 iliyokuwa ikiwakabili Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Lakini hata hivyo, Aprili 23, 2004 jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, ilitengua adhabu hiyo na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa, baada ya kuonekana kuwa wameua kwa makusudi.
Adhabu hiyo imetolewa baada ya kushindwa kwa rufaa yao waliyoiwasilisha mahakamani hapo, kwa kupinga adhabu hiyo ya miaka 15 Chuo cha Mafunzo iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Hata hivyo, aliyekuwa Rais wa Zanzibar kwa wakati huo Dk. Amani Abeid Karume, Novemba 12, 2002 aliwapatia msamaha kutoka adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kifungo cha maisha.
Kwa mujibu wa Staff Ofisa huyo, pamoja na kutumikia kifungo cha maisha Chuoni hapo, hali ya mwanafunzi mwenzake bado inaendelea vizuri.
Thursday, 20 January 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment