Tuesday, 25 January 2011

KENNEDY CENTER KUWAFUNDA WASANII ZANZIBAR

 Kennedy Center kuwafunda wasanii Zanzibar

Na Aboud Mahmoud
Jumatano Januari 26, 2011
TAASISI ya kimataifa ya sanaa ‘Kennedy Center’ ya Marekani, imeandaa mafunzo maalumu kwa wadau wa sanaa wa Zanzibar, yaliyopangwa kufanyika Februari 12, katika ukumbi wa Makumbusho ya Kasri Forodhani.

Mratibu wa semina hiyo ambae pia ni mwanafunzi wa kituo hicho Kheri Abdullah Yussuf, amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuendeshwa na Rais wa taasisi hiyo Michael M. Kaiser.

Alifahamisha kuwa, mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu juu ya nyanja mbalimbali za kisanaa, ikiwemo kustawisha taasisi za sanaa zinazojitegemea, mikakati ya sanaa ya muda mrefu, utafutaji wa rasilimali ya kuendeshea kazi hizo, pamoja na utendaji bora kwenye bodi za sanaa.

Kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo, Kheri alifahamisha kuwa, semina hiyo itawashirikisha wadau mbalimbali miongoni mwa viongozi wa sanaa nchini kutoka katika taasisi za kiserikali na binafsi.

Kheri alieleza kuwa kufanyika kwa semina hiyo ya mafunzo hapa Zanzibar, kutaleta faraja kubwa katika tasnia ya sanaa ambayo ni miongoni mwa mambo yanayoitangaza nchi kimataifa.

Mbali na Zanzibar, Kheri alisema mtaalamu huyo wa sanaa, ataendesha kozi kama hizo katika nchi nyengine nne za Afrika ambazo ni Nigeria, Uganda, Kenya na Zimbabwe ambazo zote zina wanafunzi wa kituo hicho.

Kheri ni mwanafunzi pekee Mtanzania katika kituo hicho kilichoko Marekani, tangu ajiunge nacho mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment