Saturday 22 January 2011

DK. SHEIN WAHITIMU VYUO VIKUU WASAIDIE MAENDELEO YA NCHI.

Dk.Shein: Wahitimu Vyuo vikuu wasaidie maendeleo ya nchi

 Ni katika kuelimisha sayansi, teknolojia mashambani, uvuvi
 Afungua milango zaidi kwa wawekezaji sekta ya elimu
Na Rajab Mkasaba

VYUO Vikuu duniani vimetakiwa kufungua matawi yao Zanzibar kutokana na kuwepo mazingira mazuri ya kuwekeza katika elimu, pamoja na soko kubwa la wanafunzi wa ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipohutubia katika mahafali ya tano ya Chuo Kikuu cha Elimu cha Zanzibar kilichopo Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Dk.Shein amevitaka Vyuo hivyo kutumia mafanikio makubwa yaliyopatikana na Chuo Kikuu cha Elimu cha Zanzibar, ambacho kiko chini ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika cha Khartoum kama kigezo cha mazingira bora yaliyopo Zanzibar.

Katika kufungua matawi hayo, Dk.Shein alisisitiza umuhimu wa matawi hayo kuwekwa katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambamo pia mbali ya faida zitazopata vyuo hivyo, kuna usalama, utulivu na ushirikiano mkubwa.

‘Tayari Serikali yangu imeshafungua milango ya uwekezaji katika sekta ya elimu, napenda kurudia tena leo kusisitiza tena mje kuwekeza na kuahidi ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini’ alisema Dk.Shein.

Dk. Shein alikipongeza na kukishukuru Chuo Kikuu cha Elimu cha Zanzibar kwa kuweka gharama za mafunzo bei zenye kuzingatia watu masikini, pamoja na kutaka kuongezwa kwa unafuu ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu kulipia masomo hayo, jambo ambalo amesema pia lifanywe na Vyuo Vikuu vingine hapa nchini.

Dk.Shein alikipongeza Chuo hicho cha kuzingatia uwiano wa kijinsia, ambapo alisema inafurahisha kuona katika mwaka wa tatu kina wanafunzi 152, ambapo wanawake ni 84, huku mwaka wa kwanza ukiwa na wanafunzi 307 ambapo 185 ni wanawake n 122 wanume.

Katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Zanzibar, Dk.Shein alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupatikana walimu wa sayansi na teknolojia kama wanaotolewa na chuo hicho, ili waweze kusaidia kuelimisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaoendesha viwanda.

‘Kuna haja ya wahitimu wa sayansi na teknolojia, kutumia muda wenu wa ziada kuelimisha wakulima, wavuvii, wafugaji na wananchi wetu katika kutumia njia bora za kuimarisha shughuli hizo’ alisisitiza Dk.Shein.

Dk.Shein alisema chuo hicho ni mdau mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha malengo ya Mapinduzi hasa katika kuimarisha elimu na kuwapatia elimu bora wananchi.

Alisema mahafali hayo yametokea wakati muafaka, ambapo Zanzibar inaadhimisha miaka 47 ya Mapinduzi yake matukufu, pamoja na kushukuru kupewa fursa kuwa mgeni rasmi akiwa katika muda mfupi wa uongozi wake Zanzibar.

Rais Shein alisisitiza umuhimu wa kupatikana walimu wengi katika kufanikisha malengo ya Serikali kuimarisha elimu katika ngazi mbali mbali ikiwemo maandalizi, msingi, sekondari na vyuo, ndio maana ikaweka sera ya kushirikiana na sekta binafsi ili kufanikisha mpango huo.

Aliipongeza na kuishukuru sekta binafsi ikiwemo Jumuiya ya African Muslim Agency kwa kuiunga mkono serikali kuitikia wito wa kusaidia katika kuinua elimu nchini.

Pia, Dk.Shein alikipongeza chuo hicho, pamoja na vyuo vikuu vingine viwili vilivyopo Zanzibar kwa kutoa Digrii za sayansi, ambazo amesema ni tegemeo kubwa kwa maendeleo ya Zanzibar katika kipindi hichi ambapo ulimwengu unaendeshwa kwa sayansi na teknolojia.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alikipongeza chuo hicho kwa kuanzisha mipango yake ya kuwa Chuo Kikuu Kamili katika kipindi kifupi kijacho.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Chuo hicho, Dk. Abdulrahman Al Muhala akitoa taarifa fupi ya chuo hicho alisema malengo ya wananchi wa Quwait kuwasaidia ndugu zao wa Zanzibar kupata maendeleo katika utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) na Dira ya Maendeleo 2020 yanafanikiwa kila uchao kwani tayari chuo hicho kimezalisha walimu wengi katika fani ya sayansi, jamii na kiarabu ambao wanatumika katika sekta mbali mbali.

Alisema wananchi wa Quwait wanaisaidia Zanzibar ili kuimarisha urafiki na udugu baina ya nchi hizo mbili, pamoja na kulipa fadhila ambazo wananchi wa Quwait walifanyiwa Zanzibar siku za nyuma wakati walipokuwa wakifika Zanzibar kwa shughuli mbali mbali ikiwemo usafiri wa baharini na biashara.

Akizungumzia mafanikio ya Chuo hicho, Dk. Abdulrahman alisema kwamba chuo hicho kimepiga hatua kubwa ikizingatiwa kuwa kimeanza kwa kuwa na wanafunzi 25 miaka 12 iliyopita na kufikia 1054 hivi sasa.

Aidha, alitaja maendeleo mengine kuwa ni kuongezeka kwa fani zinazosomeshwa hapo, pamoja na walimu wa kufundisha masomo mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti huyo aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar na Serikali yao kwamba kiwango cha elimu kinachotolewa chuoni hapo kitaongezeka kila muda ukienda, kwani tayari kumeshatekelezwa Mpango Mkakati wa kuhakikisha hilo.

Alisema mpango huo utaongeza uzalishaji wa walimu bora, ambapo pia alikaribisha walimu wanaotaka kujiendeleza kujiunga na chuo hicho, katika masomo ya Jografia, Historia, Physics, Hesabu, Baolojia na Chemistry, pamoja na kiarabu na masomo ya dini ya kiislamu.

Jumla ya wanafunzi 177 wamehitimu na kutunukiwa Digrii zao kwenye mahafali hiyo ya tano, wakitoka katika fani za sayansi, sayansi jamii na kiarabu.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha Afrika kutoka Sudan, Profesa Mahd Satti, aliahidi kutoa nafasi zaidi za masomo kwa Zanzibar kama hali itavyoruhusu na akakipongeza Chuo cha Elimu Chukwani kwa kuwa balozi bora wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, aliwataka wahitimu wa mahafali hiyo kuwa wazalendo na kubakia kufanya kazi nyumbani kwao, ambako mchango wao unahitajika sana.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mabalozi wadogo wa nchi mbali mbali wanaofanya kazi zao Zanzibar na viongozi wa taasisi mbali mbali za kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment