Tuesday 25 January 2011

WAZIRI FEREJI AITAKA JAMII KUSAIDIA VITA DAWA ZA KULEVYA.

Waziri Ferej aitaka jamii kusaidia vita dawa za kulevya

Na Aboud Mahmoud
Jumatano 26,Januari 2011

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, imesema itaendelea na juhudi na kutoa kila aina ya msukumo kuongeza kasi katika kukabiliana na usafirishaji, uingizaji na utumiaji wa dawa ya kulevya nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej, ameeleza hayo kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Jumuia ya Vijana waliooacha matumizi ya dawa ya kulevya pamoja na wazee katika ukumbi wa Baitul Yamin uliopo Malindi mjini hapa.

Waziri Fatma, alisema serikali na taasisi zake itaendelea kuchukuwa hatua katika kukabiliana na suala la dawa za kulevya na hivyo kuomba mashirikiano ya pamoja katika kukabiliana na vita hivyo.

Aidha Waziri huyo alisema matumizi ya dawa za kulevya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, kutokuwepo mani, magonjwa ya akili , UKIMWI na hata vifo ambapo jamii imekuwa ikishuhudia.

Alifahamisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanachangia kudumaza maendeleo na mustakabali wa vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa dawa hizo.

“Vijana na wazazi tuliopo hapa sote ni mashuhuda wa haya na ndio maana tupo hapa hivyo nina imani maazimio na majadiliano yetu yatakuza ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na vijana”,alisema Waziri huyo.

Aliiomba jamii kutowatenga wale walioamua kuachana na matumizi ya dawa hizo na kuwa nao karibu kwa vile wanahitaji msaada wa kifamilia na kupata huduma zinazotahili.

Katika mkutano huo Waziri Fatma alimkabidhi Nishani maalum kijana Abdurahman ambaye ametimiza mwaka mmoja bila ya kutumia dawa za kulevya, ambaye anaishi katika nyumba za kurekebisha tabia na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ‘Sober House’ iliyopo Tomondo.

Mkutano huo umedhaminiwa na Taasisi ya American International Health Alliance (AIHA) ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Dk. Omar Dadi Shajak, Mkurugenzi wa Idara ya Kupambana na Dawa za kulevya, Wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za kupambana na Dawa za kulevya kutoka Tanzania Bara pamoja na wazazi wa walioacha madawa ya kulevya.

No comments:

Post a Comment