Tuesday, 25 January 2011

WIZARA YAANDAA MUONGOZO MATUMIZI YA DAWA.

Wizara yaandaa muongozo matumizi ya dawaNa Fatma Kassim, Maelezo
Jumatano 26, Januari 2011
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mohammed Saleh Jidawwi, amesema kuwa kuwepo kwa muongozo wa dawa muhimu katika hospitali, kutasaidia kufanikisha matumizi mazuri ya dawa na kutoa matibabu bora na ya uhakika.

Akizindua kitabu cha nne cha muongozo wa orodha ya dawa muhimu huko Wizara ya Afya, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa kitabu hicho ni muhimu katika suala zima la upatikanaji wa dawa muhimu ambazo zinahitajika hapa nchini.

Alifahamisha kuwa lengo kuu la kuwepo kwa kitabu hicho ni kuweza kujua aina ya dawa ambazo zinatumika hapa nchini na kuziwezesha kufanya marekebisho kwa dawa ambazo hazitumiki na kuingiza zile ambazo kwa wakati huu zinazoonekana zinafaa.

Aidha alisema shabaha ya serikali ni kuwapatia wananchi wake matibabu yaliyobora na ya uhakika, ambapo lengo halitofikiwa iwapo hakutakuwa na utaratibu unaokubalika katika kutekeleza kwa vitendo sera ya afya pamoja na sera ya dawa.

Alisema katika kuzifahamu dawa ambazo zinatumika hapa nchini ni vyema washirika wa maendeleo kutoa misaada yao kwa dawa ambazo zimo katika orodha ya dawa muhimu kwa lengo la kuepuka dawa ambazo hazitohitajika katika mahospitali.

Nae Mfamasia Mkuu wa Wizara ya Afya, Habib Ali Sharif alisema katika kufanikisha huduma za utoaji dawa katika visiwa vya Unguja na Pemba, wana mpango wa kuwa na bohari kuu zaidi ya dawa kwa lengo kutoa huduma zenye ufanisi zaidi.

Alisema kuzinduliwa kwa kitabu hicho cha nne cha muongozo wa dawa ni kujua mahitaji ya dawa katika hospitali na vituo vya afya.

Kitabu hicho hadi kukamilika kwake kimedhaminiwa chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA).

No comments:

Post a Comment