Tuesday, 25 January 2011

MAALI SEIF ATAKA KUMALIZWA UTEGEMEZI WA CHAKULA.

Maalim Seif ataka kumalizwa utegemezi wa chakula

Na Abdi Shamnah
Jumatano 26, Januari 2011
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ameitaka Wizara ya Kilimo na Maliasili kuhakikisha inapunguza kasi ya utegemezi wa chakula kutoka nje.

Maalim Seif alitoa changamoto hiyo jana huko Maruhubi alipokuwa akizungumza na watendaji na wataalamu wa Wizara hiyo ambapo pia alielezwa majukumu na changamoto mbali mbali zinazoikabili wizara hiyo.

Alisema wakati umefika kwa wataalamu wa wizara hiyo kuhakikisha wanamaliza tatizo la utegemezi wa chakula kwa kukuza uzalishaji nchini pamoja na kuiepusha nchi na balaa la njaa.

Alifahamisha kuwa jukumu la Wizara hiyo kuhakikisha kuwa wananchi wa Unguja na Pemba hawafi kwa njaa na kutaka kuwepo mipango itayohakikishia kunakuwepo chakula kutosha na ikiwezekana akiba.

Aidha Maalim Seif, alitaka kuwepo umakini katika matumizi ya ardhi, kwa kigezo kuwa Zanzibar ina eneo dogo la ardhi, linalokaliwa na watu wengi huku kukiwa na mahitaji mengi yakiwemo kilimo, ujenzi, uwekezaji na viwanda.

Aliitaka Wizara hiyo kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha maeneo ya ardhi yanatumika kama ilivyoanishwa, vinginevyo katika kipindi kifupi kijacho kutakuwa hakuna tena eneo la kilimo.

Katika hatua nyingine Maalim Seif aliitaka wizara hiyo kufanya utafiti wa kutosha kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao yanaozalishwa nchini, ikiwemo yale ya matunda na biashara.

Akitoa mfano wa zao la karafuu, Maalim Seif alisema kuna nchi nyingi duniani kama vile Brazil, Indonesia na Comorro zinazozalisha zao hilo kwa wingi, ikilinganishwa na Zanzibar inayozalisha wastani wa tani 6,000 kwa mwaka, hivyo alitaka utafiti huo uimarishe thamani ya karafuu za Zanzibar ili iweze kushindana katika soko la dunia.

Akizungumzia madai ya vijana kuikimbia sekta ya kilimo, alisema mazingira yaliopo katika sekta hiyo hayavutii na kuamini kuwa upo uwezekano wa kupata kiwango kikubwa cha mapato.

Alisema wakati umefika kwa kilimo kuondokana na matumizi ya zana za kizamani na kuelekea katika zana za kisasa sambamba na matumizi ya mbegu bora.

Mapema Waziri wa wizara hiyo, Mansour Yussuf Himid alimueleza Makamu huyo kuwa moja ya tatizo linaloikabili Wizara hiyo ni uhaba mkubwa wa mabwana shamba, ambapo wastani wa mtaalamu mmoja huwatumikia wakulima 1,500 badala ya 450 kama inavyokubalika.

Alisema lililo baya zaidi ni kuwa wataalamu wengi katika fani hiyo wana umri mkubwa, ambao siku zao za kutaafu kazi zinahesabika.

Naye Naibu Katibu mkuu Maliasili Bakar Aseid alisema moja ya changamoto inayoikabili sekta hiyo ni hulka ya binadamu ya kuwinda wanyama na ndege wa asili kiasi cha kutoweka kabisa.

Katika ziara hiyo Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali ya kilimo ikiwemo mradi wa minazi Kijichi, kitengo cha Utafiti wa kilimo Kizimbani, Chuo cha kilimo, pamoja na mashamba ya viungo.

No comments:

Post a Comment