Tuesday 18 January 2011

MAWASILIANO YAZINDUA UJENZI WA BARABARA ZA NDANI MAKUNDUCHI

Mawasiliano yazindua ujenzi barabara za ndani Makunduchi


Na Ali Mohamed, Maelezo

UJENZI wa Barabara mbili za ndani katika jimbo la Makunduchi umezinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano, Issa Haji Ussi na Mwakilishi wa jimbo hilo Haroun Ali Suleiman.

Akizungumza na Masheha wa shehia sita za Makunduchi itakayopita barabara hizo, Naibu Waziri alisema maandalizi ya ujenzi huo yamekamilika na tayari kwa kuanza ujenzi mezi huu wa Januari

“Fedha tayari zimetengwa kutoka mfuko wa barabara wa Zanzibar kwa ajili ya ujenzi huu na utafiti umefanyika, hivyo tupo tayari kuanza kazi siku ya Jumapili mwezi huu,"Alisema Naibu Waziri.

Aidha aliwataka masheha hao na wananchi kushiriki vya kutosha kwa kuwapa ushirikiano mafundi wa ujenzi huo katika kipindi chote cha kazi na kuepuka kufanya ghila ikiwemo wizi wa vifaa vya ujenzi.

Alisema azma ya serikali ni kuwapunguzia wananchi makali ya maisha kwa kujenga miundombinu itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za msingi na mahitaji ya maisha ya kila siku.

Nae Mwakilishi wa jimbo hilo, Haroun Ali Suleiman alisema barabra hizo zinajengwa na serikali na kusema zikikamilika zitamaliza sehemu ya kero la usafiri wa ndani linalowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Alisema ingawa fedha zilizopo ni chache kwa ujenzi huo lakini atafanya kila liwezekanalo kupata fedha zaidi ili ujenzi huo ukamilike kwa lengo la kuwaondolea dhiki ya ya usafiri wananchi hasa katika kipindi cha mvua.

Msheha wa shehia hizo kwa niaba ya wananchi wao wameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa wahusika ili kuhakikisha barabara hizo zinamalizika katika muda muafaka uliowekwa.

Barabara hizo zitajengwa kutoka Koba kwenda Kajengwa na kutoka Koba kwenda Tasani na Nganani na ujenzi huo utakuwa chini ya usimamizi wa Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini ambapo mafundi watapiga kambi hadi kazi hiyo itakapomalizika na huduma zote zitatolewa na viongozi wa jimbo.

Wakati huo huo Mbunge na Mwakishi wa jimbo hilo la Makunduchi walipata fusa ya kutembelea jimbo hilo kwa kuagalia maendeleo ya wananchi katika shughuli zao mbali mbali na pia kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi ambapo waliahidi kuyapatia ufumbuzi kwa njia ya ushirikiano.

Mbunge wa jimbo hilo, Samia Suluhu Hassan alisema uchimbaji wa visima hivyo ni miongoni mwa ahadi za viongozi wa jimbo hilo za kuwaondolea kero wananchi.

No comments:

Post a Comment