Operesheni yaangaamiza kunguru 200,000
Na Mwantanga Ame
KUNGURU 200,000 wameuwawa baada ya Idara ya Mazao ya Biashara, Matunda na Misitu kuendesha operesheni maalum ya kuwaangamiza ndege hao, ambao wamekuwa wakisababisha uharibifu mkubwa.
Kunguru weusi ni ndege ambao mbali ya kusababisha hasara ya mamilioni kwa makampuni na watu binafsi, pia wamekuwa ni ndege wenye kuharibu mazingira.
Idara hiyo imechukuliwa hatua ya kuwaangamiza ndege hao, baada ya kubainika kuwepo kwa ongezeko kubwa la ndege hao kiasi ambacho wanashindwa kujitosheleza haja ya kimaumbile na kuwafanya kuwa wezi kwa kiasi kikubwa huku wakiisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na wizi wanaoufanya.
Akizungumza na Zanzibar Leo Mkuu wa operesheni hiyo Yussuf Kombo, alisema operesheni hiyo ilianza Januari 2010 tayari wameweza kuwaangamiza kunguru 200,000 hadi kufikia mwezi Disemba mwaka jana katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema hivi sasa kunguru hao wamekuwa wakionekana katika maeneo mbali mbali wakizagaa nyakati za asubuhi ambapo hufa baada kuwekewa dawa kwenye nyama maalum ambazo huwekwa sumu na kutupwa katika mapaa ya nyumba.
Alisema wameamua kutumia mapaa ya nyumba kuweka nyama hizo kutokana na kulinda mazingira ardhi pamoja na viumbe vyengine visiweze kufikia vyakula hivyo ambapo kunguru wanapojaribu kula huwachukua masaa 13 kuweza kufariki na ndio maana hufa wakati wa usiku wanapolala.
Akifafanua kauli hiyo alisema wizi mkubwa ambao wamekuwa wakiufanya ni kuiba mapapai, mahindi pamoja na wakiiba macho ya ndama wa ng’ombe kwa kuwatofoa na kuwasababishia vidonda.
Wizi mwengine ambao wamebainika kuufanya ni wa mabendeji ya wagonjwa yanayotupwa katika Mahospitali ambapo baadae wanapogundua kuwa hayaliki huyatupa mitaani jambo ambalo husababisha uchafuzi wa mazingira.
Aidha aliutaja wizi mkubwa ambao huufanya kunguru hao Afisa huyo alisema ni katika makampuni ya simu ambapo huiba moja ya kifaa muhimu cha mawasiliano ambavyo huwa ndani ya minara ya simu.
Alisema tayari kampuni ya simu ya Zantel imekuwa inapoteza milioni 30 kwa nusu saa inapotokezea kuibiwa kwa kifaa hicho na kunguru hao ambapo husababisha kukosekana kwa mawasiliano nchi nzima.
Akiendelea Afisa huyo alisema hivi sasa baada ya kuwepo kwa operesheni hiyo baadhi ya kunguru wameanza kuitambua na kuamua kuukimbia Mji na kuhamia Kiwengwa na Nungwi jambo ambalo limekuwa likiwafanya kulazimika kufukuzana nao.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu wa kutekeleza zoezi hilo kwa vile hulazimika kutumia gharama kubwa ya kukimbizana nao kutokana na watendaji kutokuwa na chochote vikiwemo usafiri wa kutosha na baadhi ya vifaa muhimu vya kufanyia kazi hiyo ikiwemo ya ununuzi wa nyama inayotumika kuwategeshea ndege hao.
Alisema mradi huo fedha ambazo umetengewa kutumia ni shilingi milioni 12 kutoka katika mfuko wa mradi wa usimamizi wa Mazingira wa ukanda wa Pwani (MACEMP).
Alisema kwa mwaka huu mradi hautaweza kuwashirikisha watoto kwa kukamata makinda ya ndege hao ama mayai kutokana na kujitokeza watoto wengu kuanguka katika miti na kuwasababishia kupata athari katika viungo vyao.
Kutokana na kuwepo kwa kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuendesha kampeni hiyo Afisa huyo aliwataka wananchi, wafanyabiashara na makampuni ya simu kuona haja ya kutoa michango yao itayoweza kufanikisha kazi hiyo.
“Kama mfanyabiashara mwenye kujali biashara yake anapata hasara ya shilingi milioni 30 kwa nusu saa kwa nini asishirikiane nasi kusaidia japo milioni 2 au 3 ama kutoa ng’ombe mmoja tukapata nyama ya kutegeshea tungekuwa mbali tunaomba wenye uwezo wasaidie hili kwani kunguru watatumaliza” Alisema Afisa huyo.
Alisema wengi wa wakulima hivi sasa wameanza kukata tamaa kutokana na uharibifu wa ndege hao kiasi cha kuwafanya kushinda mashambani muda mwingi kuwainga baada kukimbia mjini na kuhamia mashambani kwa hofu ya kuuliwa.
Afisa huyo aliwataka wananchi kutokuwa na hofu ya zoezi hilo kutokana na kuwabaini kunguru hao nyakati za asubuhi kwa vile dawa wanayoitumia sio ya kunyunyiza katika anga hutupwa katika nyama na ndege hao hula asubuhi.
Kunguru ni moja ya ndege walioapizwa na Nabii Nuhu, baada kushindwa kurudi kutoa majibu sehemu aliyotumwa kutokana na kukuta mizoga ya vyakula mbalimbali ambapo Nabii huyo, alimuapiza kuhangaika maisha yake.
Historia kunguru hao kuja Zanzibar inaelezwa ni zawadi iliyoletwa kwa watawala wa zama hizo.
Thursday, 20 January 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment