Thursday, 20 January 2011

MARUBANI KUJIANDA KUGOMA

. Marubani wajiandaa kugoma

 TATP yadai kuchoshwa kudai maslahi bora kwao
 Wadai rushwa yatumika kusajili marubani wageni
Na Kunze Mswanyama,Dar es salaam

HUKU migomo ikiendelea kurindima kwenye Vyuo Vikuu, Taifa linaweza kusimamisha shughuli za usafiri wa anga, kutokana na Marubani nao kujiandaa kuingia kwenye mkumbo huo.

Marubani hao wanajiandaa kuingia kwenye mgomo wa kususia kuzipaisha ndege angani, wakiishinikiza serikali kuwaboreshea maslahi yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Marubani (TATP), Kepteni Khalal Iqbar, alibainisha kuwepo kwa mgomo huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema dhamira kubwa ya kutaka kuingia kwenye mgomo wa kutozirusha ndege hizo angani ni kutokana na kuitaka serikali kujali maslahi yao badala ya kuwapendelea marubani wa kigeni.

Kepteni Khalal, alisema marubani wazalendo wamekuwa wakinyanyaswa hasa pale wanapofuatilia madai yao, akisema tayari wamefungua kesi mahakamani na hivyo wanasubiri kuarifiwa siku ya kuanza kesi hiyo.

TATP, ilisajiliwa mwaka jana, ambapo kilianzishwa rasmi mwaka 1961 na kwamba mwaka 1984 kilianza kupoteza mwelekeo na kilikuwa kikifanya kazi pasipokuwa na usajili wa kisheria jambo ambalo ni kinyume na sheria ya Tanzania.

"Mnajua kila wanataaluma wanakuwa na chama chao cha kutetea maslahi yao, walimu wana CWT tena ni walimu wazawa tu, Madaktari wana chama chao, walinzi na kila taaluma, na sisi tumesajili cha kwetu, lakini tunalazimishwa kuwaingiza wageni ili kuwa na kauli, katika chama hicho, hatutaki", alisema katibu huyo.

Alisema Wizara zinazohusika na maslahi yao, zimekuwa zikiwadharau na hata kuwaandikia barua zinazoonesha dharau jambo linalowaweka katika wakati mgumu, ilhali wao walikuwa wakifanya kazi katika Shirika la ndege la serikali la ATC lililokosa uwezo wa kuwaajiri.

"Nawaambia kuna mashirika ya ndege hayana rubani Mtanzania hata mmoja na mengine yanatumia marubani wasiokuwa na uzoefu tena hawana hata leseni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni za kitaifa na kimataifa za urushaji ndege", alisema.

Khalal alisema yapo mashirika ya ndege ambayo pia yanatumia rushwa kupata leseni za marubani wa ndege zao, ambao pia wanashirikiana na Maofisa wa wizara katika kupatikana kwa leseni hizo.

Alisema wao walisomeshwa kwa pesa za walipa kodi wa Tanzania lakini hawatumiki kwa maslahi ya taifa kwa kuwa tu kuna urasimu katika mamlaka ya ndege na hata kwa baadhi ya maofisa wa wizara wanaotumika kutoa vibali vya kufanya kazi kwa kulaghaiwa kwa pesa na wageni hao wasiojali maslahi ya taifa.

Chama hicho kina majina ya Marubani wasaidizi wanaofanya kazi pasipokuwa na vibali na hawajatimiza masaa 360 ya kurusha ndege ili kupata ajira sehemu yoyote jambo linalofanya kuwa na hatari zaidi ya kupata ajali nyingi za ndege na hivyo wao wanajiandaa kupinga hali hiyo kwa kutumia mbinu zozote.

Naye Kepteni William Silaa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama hicho, alisema kuna vijana wengi tu wa Tanzania ambao hawana kazi lakini wamesoma na kufaulu elimu ya urubani na nafasi zao kuchukuliwa na wageni ilihali wote wana elimu sawasawa.

Silaa alisema,"Najisikia uchungu sana kuona kuwa nchi inataka kuingia kwenye hali mbaya watakapotangaza, serikali inawajali wageni wakati watoto wa hapa tunatumika kwa mashirika ya nje tena yanayotunyanyasa na serikali ikifahamu hilo hata haichukui hatua zozote",alisema Ofisa huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi.

"Wanasema eti sisi hatuna elimu ya kutosha na umakini wetu ni mdogo. Pia wanadai eti sisi ni walevi, wao wanaendesha ndege wakiwa na vileo vyao pembeni na wakitua tu wanakimbilia baa, sasa nani mlevi kati yetu na wao?” alihoji Silaa ambaye ni baba wa Meya wa Ilala.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mgogoro wa chini kwa chini baina ya serikali na marubani hao jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa taifa na hata kuzorotesha usafiri wa anga ambao pia hutumika kuwasafirisha watalii na hivyo kuongeza mapato ya taifa.

No comments:

Post a Comment