Tuesday 25 January 2011

VIKUNDI VYA WEZA VYAPIGWA JEKI MILIONI 33

Vikundi vya WEZA vyapigwa jeki milioni 33

Na Mwandishi Wetu
Jumatano 26.Januari 2011


WANAVIKUNDI 189 wa mradi wa WEZA kisiwani Pemba, wamechangisha jumla ya shilingi 33,145, 000 kupitia washirika wa maendeleo kwa ajili ya kukuza miradi yao midogo midogo.

Afisa Muwezeshaji wa WEZA, Pemba, Zuwena Khamis Omar, aliwataja wafadhili hao kuwa ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mradi wa Ushirikishaji na Uwezeshaji (PADEP) na Mpango wa Msaada wa Huduma za Kilimo (ASSP).

Alisema PADEP waliweza kuchangia shillingi 23,045,000, TASAF ilitoa shilingi 9,000,000 na ASSP ilichangia shilingi 1100000.

Alisema fedha hizo zimewafaidisha wanavikundi kutoka Shehia za Mtemani Wingwi wanachama 76, Njuguni 18, Tumbe mashariki 10, Tumbe magharibi wanachama 10, Ukunjwi wanachama 60 na Ole wanachama15.

Kwa upande wake Bimkubwa Omar Othman, Mratibu Shehia ya Mtemani, alisema kikundi cha “WEZA ROHOYO”, kimepata mbuzi 34 na jumla ya shilingi milioni nne taslim kutoka kwa PADEP, mbuzi hao wapo katika hali nzuri na wengine wameanza kuzaa.

Alisema utaalamu wa kuchangisha fedha umewasaidia katika kutafuta wafadhili kwenye miradi yao inayowasaidia kujikwamua kwenye dimbwi la umasikini.

Naye msaidizi mratibu wa Shehia ya Njuguni, Fatma Juma alisema wanavikundi wamebadilika na kwamba wanafanyakazi kutafuta wafadhili kuimarisha miradi yao.

Hata hivyo alisema kuna umuhimu wa kuongezewa ujuzi wa kuchangisha fedha ili wanawake waimarike zaidi kiuchumi.

No comments:

Post a Comment