Thursday 20 January 2011

ADB KUIPIGA TAFU SEKTA BINAFSI.

ADB kuipiga tafu sekta binafsi

Na Mwantanga Ame

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (ADB), imeahidi kuendeleza kutoa misaada yake kwa sekta binafsi, kutokana na kuridhishwa na hatua za kimaendeleo zilizofikiwa.

Mwakilishi wa Benki hiyo nchini Tanzania, Mary Muduuli, alieleza hayo kwenye mazungumzo yake na uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi, Mipango na Maendeleo, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu.

Mwakilishi huyo alisema Benki yake imeridhishwa na utekelezwaji wa miradi ya kimaendeleo hapa Zanzibar inayofadhiliwa na benki hiyo.

Alisema kutokana na kuridhishwa na hatua hizo ADB, iko tayari kuendeleza kutoa michango yake kwa Zanzibar kwa kuiangalia zaidi maeneo ya sekta binafsi kwani ndio yenye kutoa mchango mkubwa kwa taifa.

Alisema Benki yake itaiangalia sekta hiyo ikiwa ni moja ya mikakati ya kutekeleza mpango wa kupambana na umasikini MKUZA, ambao una mahitaji mengi katika kuleta maendeleo ya nchi na kuinua hali za wananchi.

Aidha Marry alisema, inafurahisha kuona serikali ya Zanzibar, imekuwa ikifanya jitihada mbali mbali za kutekeleza mpango huo, ambao ni muhimu katika kukuza maisha ya wananchi.

Alisema Benki hiyo hivi sasa inaangalia maeneo muhimu yatakayoweza kusaidiwa chini ya mpango huo sambamba na kujua mahitaji.

Akiyataja maeneo ambayo benki yake itayapa kipaumbele katika kusaidia ni pamoja na mafunzo ya amali ambayo ndiyo yatayoweza kufungua milango ya kuondoa matatizo katika kupambana na umasikini.

Alisema Zanzibar imekuwa ikipiga hatua vyema kwenye miradi ya utoaji wa huduma kama vile maji barabara na mawasiliano.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Mussa Omar, aliishukuru Benki hiyo kutokana na michango yake inayoitoa kwa Zanzibar, kwani imewezesha nchi kupiga hatua za kimaendeleo.

Aliitaja miradi hiyo ni pamoja na msaada wa miradi ya maji, sekta ya Afya ikiwa pamoja na kujenga jengo la maabara katika Chuo cha Afya, ujenzi wa nyumba za madaktari na maeneo mengine ya huduma za kijamii.

Alisema Changamoto ambayo serikali hivi sasa inakabiliana nayo ni ukuzaji wa sekta binafsi kutokana na hivi sasa ndio yenye mahitaji mengi kutokana na kukosa miundo mbinu ya kufanyia shughuli zao, mitaji masoko na ukosefu wa teknologia.

No comments:

Post a Comment