Thursday, 20 January 2011

SEKTA YA USAFIRI DUNIANI KUKUTANA ZANZIBAR.

Sekta ya usafiri duniani kukutana Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi

ZANZIBAR kwa mara ya kwanza itaandaa mkutano wa kimataifa utaowashirikisha wadau wa usafirishaji, uchukuzi na usambazaji kutoka nchi mbali mbali duniani, ambao utaanza kufanyika mwezi Machi mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mkutano huo, ambae pia ni Meneja Mkuu wa Bandari Kavu kupitia kampuni ya Azam jijini Dar es Salaam, Ashraf Khan, alisema hayo katika Ofisi ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Malindi mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Khan alisema mkutano huo wa kimataifa utakuwa wa siku mbili ambapo utaanza Machi 8 na ambapo wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na nje watajadili uendeshaji wa majukumu yao.

Alisema mkutano huo ni wa kwanza kufanyika Zanzibar na utafanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, itawashirikisha washikiri kutoka katika Bara la Afrika, Ulaya, Asia na Tanzania ambao utatoa fursa kwa wadau kubadilishana mawazo na kupata taaluma inayohusiana na kazi zao.

Alieleza mkutano huo utatoa nafasi ya wadau kujifunza jinsi ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa, ambapo mada mbali mbali zitajadiliwa ikiwemo ya usalama wa anga, usalama wa usafirishaji wa majini.

Hata hivyo, alisema mada nyengine zitakuwa ni usalama wa barabarani, ambao ni muhimu katika kupunguza ajali, taaluma ya usafirishaji na uchukuzi na uendeshaji na usalama wa reli.

Nae Katibu Mkuu wa The Chartered Insitute of Logistics and Transport (CILT), Tanzania, Ramadhani Sawaka alisema mkutano huo umeandaliwa na Taasisi hiyo ya Kimataifa yenye makao makuu yake Uingereza.

Alifahamisha kuwa, kufanyika kwa mkutano huo Zanzibar pia itasaidia katika kuitangaza kiutalii katika kukuza uchumi wa nchi, sambamba na kutanuka kwa huduma za usafirishaji.

Alisema wadau hao watakapokuwepo nchini watazungumzia kwa undani masuala mazima ya usalama katika usafirishaji, uchukuzi na usambazaji

No comments:

Post a Comment