Waingiza bidhaa mbovu Zanzibar kukiona
Mswaada wa sheria kuwasilishwa Barazani
Kuswekwa jela, faini nzito
Na Mwantanga Ame
KIYAMA cha waingiza vyakula vibovu kipo ukingoni baada ya serikali kuweka adhabu mbali mbali kwa wataobainika kukiuka sheria ya viwango, ikiwa pamoja na kufungwa miaka mitano jela na faini ya shilingi milioni 30,000.
Hatua hiyo ya serikali kukomesha tabia hiyo imeanishwa kwenye mswada mpya wa sheria ya kuweka Masharti ya Uendeshaji ukuzaji na uwekaji wa viwango na ubora wa Bidhaa na Usimamizi wa huduma zinazolingana na hizo, utakaowasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Kikao hicho kinatarajiwa kujadili mswaada huo pamoja na ule wa sheria kuweka miundo, uendeshaji na usimamizi wa Utumishi wa Umma Zanzibar, ambao tayari umeshawasilishwa kwa wajumbe wa Baraza hilo.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya mswada huo, umeweka taratibu mbali mbali za usimamizi wa viwango vya bidhaa zinazoingizwa nchini ikiwa pamoja na masharti ya utoaji wa leseni za biashara.
Aidha mswaada huo pia umebainisha adhabu za kifungo Chuo cha Mafunzo, kutozwa faini na mali zitazokamatwa zisizo na viwango kurejeshwa zilikotoka ndani ya kipindi cha wiki moja.
Adhabu nyengine zilizoanishwa kwenye mswada huo kwa mtu atayetiwa hatiani kwa kosa la bidhaa zisizo na viwango zitazokuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5 atawajibika kutozwa faini si chini ya kiasi hicho na sio zaidi ya shilingi milioni 3, au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na si zaidi ya miaka mitano, ama adhabu zote kwenda sambamba.
Aidha mswaada huo umebainisha adhabu nyengine zitakazo tolewa kwa mtu atakayeingiza bidhaa zitakazo kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja, lakini haizidi shilingi milioni 5, atawajibika kutozwa faini sio chini ya shilingi 500,000 na sio zaidi ya shilingi milioni 5 au kifungo kwa kipindi sio zaidi ya mienzi sita ama dhabu zote kwa pamoja.
Adhabu hizo kwa mujibu wa mswaada huo zitakuwa chini ya usimamizi wa kifungu cha 26. (1), ambapo kitabeba vifungu (2), (3), (4) ambapo kifungu cha (3), kinaipa Mamlaka Mahakama baada ya mtu huyo kutiwa hatiani kwa makosa hayo, Mahakama licha ya kutekeleza adhabu hizo itaweza kutoa ama kuagiza mali yote au sehemu ya bidhaa hizo itaifishwe na mali hiyo itaondoshwa ikiwa mahakama itaona busara kufanya hivyo.
Aidha masharti mengine ndani ya mswaada huo yatameelekezwa kwa watendaji ambapo watalazimika kuyafuta ikiwa pamoja na utendaji wa bodi itayoundwa kusimamia taasisi hiyo.
Madhumuni halisi ya serikali kuweka mswada huo imeelezwa kuwa ni kutunga sheria itayoweka masharti uendelezaji, ukuzaji na usimamizi wa viwango na ubora wa bidhaa ili kuiwezesha serikali kusimamia bidhaa za biashara kwa kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa hizo kwa afya za watumiaji na jamii.
Aidha mswaada huo umeeleza kuwa madhumuni ya kuanzishwa kwake ni kuweka sheria inayopendekezwa inaweka mazingira mazuri katika mfumo wa ushindani wa biashara na kushajiisha uzalishaji wa bidhaa za ndani za biashara na kuiwezesha sekta binafsi kwenda sambamba na kufuata masharti ya viwango vya kimataifa kwa kuzingatia mpango wa usafirishaji bidhaa nje ya nchi (NES).
Mswada huo utawasilishwa katika kikao cha Barza hilo ambacho kinatarajiwa kuanza Jumatano ijayo na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui.
Hatua hiyo ya serikali inachukuliwa kutokana na kujitokeza kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya kuwepo vyakula ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu.
Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi mwaka jana ilifanya operesheni kadhaa za kukamata vyakula na vipodozi visivyofaa kwa matumizi ya jamii.
Friday, 14 January 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment