Monday, 10 January 2011

DK. MWINYIHAJI AWATAKA MADIWANI KUTOJIHUSISHA YASIOWAHUSU

Dk. Mwinyihaji awataka madiwani kutojihusisha yasiyowahusu

NA Luluwa Salum, Pemba
Jumanna 11, Januari 2011

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, amewataka Madiwani kisiwani Pemba kutojishughulisha na kazi zisizowahusu.

Dk. Mwinyihaji alitoa kauli hiyo huko Chake-Chake, alipokuwa akilizindua rasmi Baraza ka nne la Mji wa Chake-Chake huko Chachani.

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi yanayodaiwa Madiwani kufanyakazi zisizo wahusu ikiwemo suala la uuzaji wa viwanja kiholela usiozingatia sheria.

Waziri huyo alisema ili kuepukana na matatizo hayo ni vyema wakaacha kuingia kazi zilizo nje ya uwezo wao hali itakayoepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.

Aidha Waziri huyo aliwataka Madiwani hao kuwa wakweli katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kuwajibika katika kuwahudumia wananchi ili waweze kuondokana na matatizo waliyonayo.

Dk.Mwinyihaji aliwataka Madiwani hao wa mji wa Chake-Chake, kuwa na mashirikiano katika kazi, jambo ambalo litakuwa chachu ya kuiletea Zanzibar maendeleo na kuuwezesha mji huo kubadilika.

Alisema haiba ya Mji wa Chake-Chake imeondoka kutokana na Mji huo kuwa mchafu hivyo na kuwataka Madiwani hao kutafuta njia mbadala ya kuurejeshea hadhi mji huo, kwa kukabiliana na suala la usafi.

Alibainisha kuwa suala la ukusanyaji wa mapato limeshuka na kuwataka madiwani hao kubuni vyanzo vipya vya mapato ili mji huo uweze kujiendesha vyema.

Kwa upande wao Madiwani hao wamemuhakikishia Dk.Mwinyihaji kuwa watafanya kazi kwa kufuata sheria na kwa kuzingatia usawa bila ya kujali itikadi za vyama sambamba na kusema watayatekeleza yale yote aliyowaagiza ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa uangalifu zaidi suala zima la mapato yanayopatikana.

Walisema kama ilivyo dhamira ya serekali ya awamu ya saba kuwaletea wananchi wake maendeleo kwa kuondosha tofauti zilizokuwepo na wao pia wameahidi kufanya mabadiliko makubwa ili kwenda sambamba na sera ya serekali ya kuleta mabadiliko.

No comments:

Post a Comment