Thursday, 6 January 2011

WAZAZI CCM WAJENGA MATUMAINI KWA DK. SHEIN.

Wazazi CCM wajenga matumaini kwa Dk.Shein

Na Rajab Mkasaba
Alhamisi Januari 6, 2011

JUMUIYA ya Wazazi CCM Taifa imeeleza kuridhika kwake na uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na kueleza matumaini yake makubwa katika uongozi huo kwa maendeleo ya Zanzibar.

Akitoa salamu za shukurani kwa niaba ya ujumbe wa uongozi huo uliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa madhumuni ya kuzungumza na Rais, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa Othman Juma Mhina alieleza kuwa Jumuiya ya Wazazi imefarajika na ushindi wa Dk. Shein.

Mhina alieleza kuwa mbali ya kuridhika na ushindi wa Dk. Shein pia, Jumuiya hiyo imefarajika kwa kiasi kikubwa na mafanikio yaliopatikana katika uchaguzi mkuu uliopita ambao ulikuwa huru na wa haki.

Aidha, viongozi hao walieleza kuwa kufanyika kwa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki kumepelekea kudumishwa kwa amani na utulivu uliopo nchini.

Pamoja na hayo viongozi hao walimueleza Dk. Shein kuwa Jumuiya yao ina mpango wa kuziimarisha zaidi skuli zao ikiwemo ile iliyopo Dole Unguja na Dodeani kisiwani Pemba, licha ya changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Walieleza kuwa Jumuiya yao itaendelea kuimarisha sekta ya elimu kwani mafanikio makubwa yamepatikana kwa kuweza kupasisha watoto wengi katika skuli zao.

Katika maelezo yao viongozi hao pia, walimueleza Dk. Shein kuwa wana mpango wa kuanzisha programu zitakazokuwa zinatoa mafunzo juu ya malezi, maadili na desturi za Kizanzibari katika vyombo vya habari vya hapa nchini.

Walieleza kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na kuona malezi, desturi na maadili ya Kizanzibari yanatoweka.

Kwa upande wake Dk. Shein alitoa shukurani kwa Jumuiya hiyo kwa ujio wao huo na kueleza kuwa mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na ushindi wa CCM yametokana na juhudi za pamoja.

Alieleza kuwa hatua za kufanya uchaguzi uliokuwa wa huru na haki umeijengea sifa kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.

Dk. Shein alisema kuwa nchi mbali mbali duniani pamoja na washirika wengine wa maendeleo wameahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kuendeleza amani na utulivu uliopo.

Pamoja na hayo Dk. Shein alieleza kuwa kuendelea kudumu kwa amani na utulivu nchini kunatoa mwanga wa matumaini na mafanikio makubwa ya maendeleo.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa imeanza vyema na inaendelea vizuri katika mchakato mzima wa kujenga mustakabali mwema wa wananchi na kuleta maendeleo endelevu kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment