Wednesday, 19 January 2011

MTAALAM ATAJA CHANGAMOTO ZA KUPAMBANA NA KICHOCHO ZANZIBAR

Mtaalamu ataja changamoto za kupambana na kichocho Z’bar


Na Mwanajuma Abdi

JAMII imeshauriwa kuepukana na utamaduni wa kujisaidia haja ndogo na kubwa katika mito, mabwawa na madimbwi ya maji ili kuepukana na vijidudu vinavyoeneza maradhi ya kichocho nchini, maradhi ambayo bado tatizo nchini.

Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Mpango wa kupambana na maradhi Dk. Khalfan A. Mohammed wakati akizungumza na gazeti hili Mianzini Lumumba mjini hapa.

Alisema maradhi ya kichocho bado yanaisumbua jamii na hasa watoto Unguja na Pemba, ambapo maambukizi yake kwa mujibu wa mtaalamu huyo yanapatikana zaidi kwenye mito na maji yaliotuama.

“Maradhi haya husababishwa na vijijidudu vinavyoitwa “Schistosome haematobium, ambavyo hutokana na konokono wanaoishi katika sehemu hizo ambapo kupitia katika haja ndogo (Urinary Schistosomicesis),” alieleza Dk. Khalfan.

Aidha, alieleza maradhi hayo licha ya kupungua kutoka asilimia 60 hadi 40 katika miaka ya 90 lakini kwa sasa ugonjwa huo umefikia asilimia 10 hadi 15, yakiwa bado yanaendelea kuisumbua jamii.

Aliyataja maeneo yaliyokithiri kwa maradhi hayo, ambapo kwa upande wa Pemba yanapatikana takriban sehemu zote nakwa Unguja baadhi ya maeneo kama Kinyasini, Fuoni, Mwera na Chaani, ambapo Wilaya ya Kusini ndio pekee iliyokuwa haina ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema mradi wa miaka minne hadi mitano unaofadhiliwa na Mfuko wa Bill na Melinda wa Marekani unatarajiwa kuanza mwaka huu, ambapo mkutano wa kujadili hatua zitazochukuliwa katika kupambana na maradhi hayo unatarajiwa kufanyika Februari nane na tisa mwaka huu, huko Pemba.

Alifahamisha kuwa, mkutano huo utajadili jinsi ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii, kugawa dawa maskulini na kuwatokomeza konokono kwa kupiga dawa katika maeneo yaliyokithiri ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment