Tuesday, 18 January 2011

BARAZA LASAKA WAFADHILI UJENZI OFISI ZA WAWAKILISHI

Baraza lasaka wafadhili ujenzi ofisi za wawakilishi


Na Mwantanga Ame

OFISI ya Baraza la Wawakilishi imesema iko mbioni kutafuta wafadhili watakaoweza kusaidia uwezekano wa kupatikana fedha kwa ajili ya kujenga Ofisi za wajumbe wa Baraza hilo majimboni mwao.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ibrahim Mzee, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake Mbweni, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Katibu huyo alisema serikali imeanza kuchukua hatua mbali mbali kufanikisha mpango huo, lakini bado haijafanikiwa kutokana na wafadhili waliopelekewa maombi kutotoa jibu la uhakika.

Alifahamisha kuwa Ofisi yake, inaona aibu kuwaona wananchi hawa njia ya kuwapata viongozi wao wakiwa majimboni, huku wengine wanaobahatika kuzigeuza nyumba za viongozi hao kuwa ndio maskani zao.

Alisema hali hiyo haipendezi kwa vile masuala ya wananchi katika majimbo yalihitajika kufanyika katika ofisi za Jimbo na sio katika nyumba za viongozi hao kwani zinakuwa zinaingilia utawala binafsi.

Alisema sehemu kubwa ya maombi ambayo yanatumwa, baadhi ya wafadhili wamekuwa wakiangalia zaidi kusaidia maeneo ya utoaji wa elimu mbali mbali kwa wajumbe hao lakini hilo bado halijafanikiwa.

katibu huyo alisema hivi serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kunapatikana mafanikio ya kuwapata wafadhili kwani ndio njia pekee itayowawezesha wawakilishi kuwajibika vizuri kwa wananchi wao kwa vile watatumia afisi hizo kujadili shughuli za Baraza hilo.

Alisema hivi sasa moja ya tatizo kubwa ambalo wanalipata ni la kuona hata miswaada wanayoitoa huenda ikawa unapata michango hafifu ya wananchi kutokana na kuwa wanaopata nafasi kutoa mawazo yao sio wote.

Alisema kwa vile tayari Bazara hilo linatambua umuhimu wa kuwapo kwa ofisi hizo itaendelea kutoa ushawishi kwa wafadhili ili kuweza kupata msaada wa hilo.

Kuhusu suala la mfuko wa majimbo kuanza kufanya kazi alisema hivi sasa bado hakuna sheria inayosimamia kufanya kazi hiyo lakini ipo ahadi ya serikakali kupitia bajeti yake ijayo kutoa fedha kuingiza katika shughuli za maendeleo katika Majimbo.

Alisema mfumo wa kutumia mfuko wa majimbo ni muhimu kuwepo kwake kwa vile tayari baadhi ya nchi zimeanza kufaidika nao ikiwemo Kenya na Tanzania bara ambapo Zanzibar italazimika kuliona suala hilo ili kuweza kupunguza kero za wananchi kutimizwa.

No comments:

Post a Comment