Thursday, 20 January 2011

WAWAKILISHI KUJADILI HUTUBA YA DK. SHEIN KUBADILISHA KANUNI.

Wawakilishi kujadili hotuba ya Dk. Shein, kubadilisha kanuni

Na Mwantanga Ame

BARAZA la Wawakilishi la Zanzibar linatarajiwa kuanza kikao chake leo ambapo kitajadili hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoitoa katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Baraza la Nane.

Wajumbe hao watajadili hotuba hiyo baada ya kuitafakari kwa muda sasa kutokana na hotuba hiyo kuzungumzia masuala mbali mbali ya kimsingi na maelekezo ya kutosha kuhusu dira na mwelekeo wa serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Sehemu kubwa ya hotuba hiyo inaelekeza jinsi gani serikali itatekeleza ahadi ya kuimarisha utoaji wa huduma bora za jamii, kukuza elimu hasa ya sayansi, utekelezaji mpango wa mapinduzi ya kilimo na uvuvi.

Aidha katika hotuba hiyo, Wawakilishi watajadili masuala ya muungano na nia ya kuimarisha kwa manufaa ya pande hizo mbili, kushughulikia uanzishwaji wa viwanda pamoja na kujadili matatizo ya kibiashara.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee, alisema moja ya ajenda itakayowasilishwa katika kikao hicho kitachodumu takriban wiki mbili kitaijadili hotuba hiyo.

Alisema baraza limeamua kuweka ajenda hiyo kwa vile Rais baada ya kuisoma haikupata kujadiliwa kwa sababu kikao hicho kilikuwa cha muda mfupi na kuamuliwa kujadiliwa katika kikao cha pili.

Aidha kikao hicho kimepokea maswali 145 ambapo watendaji wakuu wa serikali watayajibu na kuyatolea ufafanuzi.

Mbali na kazi hiyo pia, baraza hilo litazipitia kanuni za Baraza hilo ikiwa ni hatua ya kuzifanyia mabadiliko ili ziende sambamba na mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa ambapo maeneo kadhaa yatalazimika kufanyiwa mabadiliko.

Mabadiliko ambayo yanahusisha kuondolewa nafasi za wakuu wa Mikoa ndani ya kanuni hiyo, kuondoa nafasi ya Waziri Kiongozi na kuingiza Makamu wa Pili wa Rais kuwa ndie Mkuu wa shughuli za serikali na kanuni ambazo zitakuwa zinaelekeza namna ya uwakilishi kupitia kamati za Baraza badala ya mfumo wa sasa kutumia Mawaziri Kivuli pamoja na kuweka Mnadhimu Mkuu wa serikali badala ya wanadhimu wa Vyama.

Baraza hilo litakuwa ni la kwanza katika muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa kuanza mjadala wake ambapo wajumbe wake hawatakaa kwa utaratibu uliozoeleka hapo awali wa Chama tawala kukaa upande wa kulia na upinzani kushoto na badala yake watachanganyika huku Mawaziri na Manaibu wake watakuwa katika safu za mbele.

No comments:

Post a Comment