Friday 21 January 2011

HUDUMA YA SHERIA WASAMBAZA DOZI YA KATIBA

Huduma za sheria wasambaza dozi ya katiba

Na Asya Hassan

HUKU wanaharakati wakipaza sauti kulilia mabadilisho ya katiba mpya nchini Tanzania, kituo cha huduma za sheria cha Zanzibar, kimeanza kutowa elimu ya katiba.

Mkurugenzi wa kituo hicho Is-haka Sharifu alisema kituo chake kimekuwa kikikusanya makundi mbalimbali katika jamii kuyapatia elimu hiyo.

Alifahamisha hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wananchi wengi pamoja na kulilia katiba mpya, lakini hawaielewi hiyo katiba ni kitu gani na nini kisichokubalika kwenye katiba hiyo.

Mkurugenzi huyo huyo alisema wananchi watakapo juwa umuhimu wa katiba ndipo watakapotoa mawazo sahihi na yenye mustakbali mwema kwa nchi wakati wa ukusanyaji wa maoni ya katiba utakapo wadia.

Aidha Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kwa kuwataka wananchi wa Zanzibar wajitokeze kikamilifu kutoa maoni yao wakati muida wa kamati ya kukusanya maoni utakapofika rasmi.

Alisema kituo chake mbali ya kufundisha katiba, pia kimekuwa kikijishughulisha na utoaji wa mafunzo mbali mbali yanayohusu sheria katika jamii.

Aliyataja miongoni mwa mafunzo yanayotolewa ni miongoni mwa taaluma ya sheria pamoja na huduma ya kwanza na mafunzo hayo yakiwafikia watu mbalimbali kama vile polisi, walimu na wananchi wa kawaida.

Hata hivyo alisema kwa mwaka 2010 wananchi waliopatiwa taaluma hiyo kwa upande wa Unguja walikuwa 1,549 na kwa upande wa Pemba walikuwa 2,671.

Aidha alisema katika mwaka huu watu mbalimbali hufika kituoni hapo kupatiwa ushauri wa mambo mbalimbali yanayohusu sheria.

No comments:

Post a Comment