Saturday, 8 January 2011

NYUMBA YA MAKAAZI YA WAZEE SEBLENI YATEKETEA KWA MOTO.

Nyumba ya mkaazi ya wazee Sebleni yateketea moto

Na Mwanajuma Abdi


MOTO uliozuka majira ya saa 4:45 usiku wa kuamkia jana, umeteketeza nyuma nambari tano ya makaazi ya wazee Sebuleni.

Moto huo ulioteketeza jumba hilo, pamoja na kuharibu mali za wazee hao hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Akizungumza na gazeti hili, Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, Gora Haji Gora, alisema mara baada ya kuanza kwa moto huo, wazee wakishirikiana na wananchi walianza kuuzima jambo ambalo lilisababisha kusambaa kwa kasi.

Alisema taarifa alizipata zisizo rasmi kutoka kwa wasamaria wema waliokuwa wakitoa kuangalia mpira katika kiwanja cha Amaani majira ya saa 5:30 usiku, ambapo magari matatu ya kikosi hicho yalifika katika eneo la nyumba hizo na kuiona nyumba hiyo ikiwa tayari imeshateketea ghora yote ya juu pamoja na paa lake.

Alieleza moto huo ulikuwa unawaka kwa kasi kutokana na vifaa vilivyotumika kujengea ambapo ni mbao za saprasi ambazo ni rahisi kushika moto.

Alisema baada ya kikosi chake kuingia kwenye eneo hilo, walikabiliana nao ambapo hadi majira ya saa 10:00 alfajiri ya jana ndipo walipofanikiwa kuuzima.

Naibu Kamishna huyo, alifahamisha kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, lakini yapo madai kuwa chumba kilichoanza moto huo mwenyewe alikuwa amewasha taa ya kibatari.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za ajali za moto zinapotokea na waache tabia waliyojingea kusema gari za Zimamoto zinapohitajika hazina maji, jambo ambalo halina ukweli.

Nae Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed, ambaye alitemebelea eneo hilo, alisema moto ulianza katika chumba cha Mzee Rajab majira ya 4:45 usiku ambae alikuwa anavuta sigara na amewasha kibatari, ambapo alilala na majirani ndio waliuona na kwenda kumuamsha baada ya kuzuka kwa moto huo.

Alisema nyumba hiyo inakaliwa na familia 10, ambapo shehemu ya juu ilikuwa inafamilia nne ambazo ndizo zilizoathirika na moto huo kwa vile hawakuwahi kuokoa kitu chochote isipokuwa wao wenyewe.

“Familia nne zilizokuwa zinaishi ghorofa ya kwanza ndio zilizoathirika na moto kwa kuungua kwa vifaa vyao vyote pamoja na vyakula vya akiba na sita zilizokuwa zinaishi chini hawakuathirika hata kidogo”, alieleza Waziri Zainab.

Aliongeza kusema moto huo ulizimwa na gari ya Zimamoto kwa kushirikiana na Polisi, ambapo familia hizo zote zimeshapatiwa makaazi katika sehemu nyengine za nyumba hizo ambazo zilizokuwa hazina watu.

Aidha alifahamisha kuwa, hadi sasa harasa ya ajali hiyo haijulikana.

Viongozi kadhaa akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili Balozi Seif Ali Iddi walifika kuwafariji wazee hao.

Nyumba za Wazee wa Sebleni ni moja ya matunda ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zilizojengwa na Muasisi wa Mapinduzi hayo, marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

1 comment:

  1. Mistari ya mwisho ni propaganda.Yaani tumepata tunda la nyumba na kupoteza utaifa mzima wa nchi yetu.

    ReplyDelete