Friday, 14 January 2011

MAISHA BAADA YA KUSTAAFU INAWEZEKANA

‘Maisha baada ya kustaafu inawezekana’

Na Halima Abdalla, Asha Bakari (MUM)

MTANGAZAJI mstaafu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar Amour Khalfan, amesema maisha baada ya kustaafu yanawezekana endapo mtumishi wa umma atafanya matayarisho mapema.

Amour Khalfan, alieleza hayo jana kwenye hafla fupi ya kuagwa yeye na wastaafu wenziwe waliokuwa watumishi wa STZ, iliyofanyika katika ukumbi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (S.T.Z).

Katika hafla hiyo mtangazaji huyo mkongwe aliwatoa hufu watumishi akiwaeleza kuwa maisha baada ya kustaafu inawezekana bila ya kusumbuka ila yanahitaji maandalizi ya mapema na kujipanga.

“Inatakiwa uwe na maandalizi na kujipanga mapema kabla ya kustaafu, hapo ndipo utakavyoweza kumudu maisha”,alisema Khalfan.

Alifahamisha kuwa kustaafu ni jambo la lazima ukapofikia muda, kueleza furaha yake kuwa amemaliza utumishi wake kwa salama na amani.

Alifahamisha kuwa utumishi wa umma ni changamoto ambapo kila mmoja anatakiwa kupambana nao, ili kufikia katika maendeleo na kuwataka wafanyakazi waliomakazini kuwa wastahamilivu na kuzidisha mashirikiano ili kuongeza ufanisi.

Nae Mkurugenzi Mstaafu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (S.T.Z), Yussuf Omar Chunda, aliwapongeza wafanyakazi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar wa Unguja na Pemba, kwa kumpa kila aina ya ushirikiano katika kipindi chote cha uongozi wake.

Alisema anaamini kazi yake ingekuwa ngumu sana kama angekosa ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi hao.

Aidha aliwataka wafanyakazi wa taasisi hiyo kumpa ushirikiano mzuri Kaimu Mkurugenzi, Hassan Vuai ambaye atashika nafasi hiyo mpaka hapo atakapoteuliwa Mkurugenzi mwengine.

Waliostaafu ni pamoja na Mkurugenzi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar, Yussuf Omar Chunda, Amour Khalfan, Thabit Majaaliwa, Ali Hassan, Hassan Yussuf Saleh, Suleiman Mrehi na Zuhura Mgeni.

Akitoa Shukrani kwa niaba ya wafanyakazi Mtangazaji Sauti ya Tanzania Zanzibar Mohammed Suleiman (Tall), aliwapongeza wastaafu hao kwa kushirikiana katika kipindi chote cha kazi walichokuwa pamoja na kuwaomba kusameheana kwa yale waliokoseana.

No comments:

Post a Comment