Tuesday 18 January 2011

WAHASIBU WA SERIKALI KUHAMISHWA

Wahasibu wa serikali kuhamishwa

Lengo ni kudhibiti mapato ya serikali
Na Mwantanga Ame

UONGOZI wa Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, umeagizwa kufanya uhamisho wa wahasibu katika idara zote za serikali kwa vile baadhi yao wanaonekana kuchezea mapato ya serikali na kusababisha wananchi kutokuwa na imani nao.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Bwawani mjini Zanzibar, wakati akizungumza na wahasibu wa serikali kutoka katika maidara na mashirika ya serikali.

Omar alisema ni lazima Mhasibu Mkuu wa serikali achukue hatua ya kuwabadili wahasibu waliopo katika maidara yote ya serikali kwa kile kinachoonekana kuwepo baadhi yao kuchezea mapato ya serikali.

Alisema wahasibu kuachwa kukaa kwa muda mrefu katika mawizara tayari baadhi yao wamekuwa wakibuni njia za kuiibia serikali kwa kuanzisha vitabu vyao binafsi vya risiti bandia huku wengine wakionekana kuwa na maisha ya hali ya juu yasiyolingana na mishahara yao.

Waziri huyo alisema kwa mfumo wa sasa ambao serikali ya awamu ya saba imekuja nao, haiwezekani wahasibu waliopo wakaendelea kuchwa kutumikia idara kwa muda mrefu na ni vyema wakapanguliwa mapema iwezekanavyo.

Alisema inasikitisha kuona serikali ikibebeshwa mzigo mkubwa wa madeni yasiokuwa na msingi ya watumishi wa umma eneo ambalo wahasibu wamelidharau kabisa kiasi cha kusababisha baadhi ya watumishi kufikia kudai fedha zinazowastahikia kwa mawaziri.

Kinachosikitisha zaidi Waziri huyo alisema kuona madai ya madeni yanayotolewa na watumishi hao kwa serikali ni yenye kiwango kidogo sana kwani baadhi yao wanadai hadi shilingi 50,000 au 20,000 fedha ambazo wizara ama idara ina uwezo wa kuzilipa.

"Jamani hii ni aibu mtu afikie kudai kwa waziri shilingi 50,000 mmekwenda skuli kuweni 'creative' (wabunifu) kudondoa madeni ya wafanyakazi, MTF inawaruhusu kufanya malipo madogo madogo lipeni na muangalie namna ya kulia makubwa," alisema Yussuf.

Alisema madeni yanaonekana kuwepo mengi zaidi katika tasisi zenye watumishi wengi ikiwemo ya Wizara ya Kilimo, Afya, Elimu ambapo madeni mengi zaidi ya likizo.

"Mna wasahau watumishi wa umma, mtu anadai shilingi milioni moja ya likizo anateswa hapewi anawekwa mienzi, lakini inapotokea kuanzishwa semina na posho za safari zinatolewa mabilioni ya pesa, hapa mnajisahau," alisema.

Alisema ni vyema kwa watumishi hao kuona udhaifu wanaoisababishia serikali mzigo wa madeni na kama wapo wataokua wameshindwa kuwajibika waamue kuacha kazi kwa hiari yao na sio kuanzisha vitu ambavyo vina sababisha uwajibikaji mbovu.

Waziri huyo alisema tayari anayo majina 140 ya baadhi ya wahasibu katika idara za serikali ambao wamekuwa na tabia ya kuchota fedha za serikali kwa mambo yao binafsi hata hivyo hakutaka kuyataja majina hayo.

Akiyageukia mashirika ya umma Waziri huyo alisema nayo kumejaa uozo ambapo baadhi yake yanaonekana kutofanya vizuri.

Waziri huyo aliwataka wahasibu hao kuona wanafanya kazi kwa pamoja kwa kusaidiana mawazo kati ya wizara na idara nyengine huku wakitafuta nafasi za masomo zaidi ambapo alimuagiza Mhasibu Mkuu awapatie fursa za kusoma wahasibu wake.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Mussa alisema atahakikisha anasimamia maagizo hayo ikiwa ni pamoja na kuwataka wahasibu hao kutayarisha bajeti zao mapema kwa kuwa baadhi ya wizara zimekuwa na tabia ya kuchelewa.

Akitaja moja ya wizara hizo, alisema ni ya Afya ambapo bajeti humalizika kupitishwa mwezi Julai lakini inapofika mwezi Januari mwaka unaofuata hupokea tena maombi ya kutolewa fedha nyengine ambazo huwa hazimo katika matumizi ya bajeti iliyopitishwa.

Naye Mhasibu Mkuu wa serikali Omar Hassan King, alisema suala la masomo kwa watumishi wa kada hiyo, serikali imekuwa ikijitahidi ambapo hivi sasa wahasibu wengi wameweza kupatiwa nafasi za masomo sehemu mbali mbali.

No comments:

Post a Comment