Matayarisho sherehe za Mapinduzi yakamilika
Balozi Seif atembelea kiwanja cha Amaan
Wananchi wajiandaa na mkesha
Na Abdulla Ali
Jumanne 11, Januari 2011
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi amesema maandalizi ya kilele cha sherehe za Mapinduzi yanayotimiza miaka 47 hapo kesho, yamekamilika.
Balozi Seif alieleza hayo jana katika kiwanja cha Amaan mjini hapa, alipofanya ziara ya kukitembelea kiwanja hicho kuangalia matayarisho ya sherehe hizo.
Mbali ya Balozi kuridhishwa na matayarisho hayo, aliwataka viongozi wahusika wazidishe bidii katika kuchunga muda na kuheshimu taratibu zilizowekwa ili sherehe hizo zifanyika vizuri.
Katika jaribio la mwisho kiwanjani hapo Makamu wa Pili na ujumbe wake waliangalia gwaride lililopita kwa mwendo wa Pole na wa haraka mbele ya jukwaa kuu.
Wakati huo huo Kamati ya Sherehe na Mapambo Taifa imekataza kabisa kupitisha ndege za shamra shamra au vipeperushi katika mikusanyiko ya watu hasa kiwanjani Amani bila ya ruhusa kutoka katika vyombo vinavyohusika.
Wakati huo huo Mwantanga Ame anaripoti, Wananchi wa Zanzibar na wageni mbali mbali waliopo wanajiandaa kuushuhudia mkesha wa sherehe za Mapinduzi ifikapo saa 6:00 usiku.
Shamra shamra hizo zinatarajiwa kupamba moto zaidi katika mkesha huo itapofika muda huo ambapo Jeshi la Wananchi wa Tanzania Nyuki Brigedi 101 KV (JWTZ), wataporusha fash fash katika mji wa Zanzibar zitazoambatana na kupigwa mizingi 21.
Aidha meli zitazokuwa katika Bandari ya Zanzibar na magari katika Barabara nazo zinatariwa kupamba mkesha huo kwa kupiga honi mfulilizo pamoja na ving’ora.
Kutokana na hali hiyo ya sherehe hizo tayari vikundi kadhaa vya burudani vya ndani ya nchi na Tanzania Bara vimetangaza adhma yao ya kutoa burudani ya taarab na mziki wa dansa katika kumbi mbali mbali za starehe zikiwemo za mjini na mashamba.
Tayari Mji wa Zanzibar tangu kuanza kwa sherehe hizo Januari 5, 2011 umeonekana kuwa na mabadiliko kwa mapambo ya aina mbali mbali zikiwemo shuguli za usafi wa mji.
Usafi huo umefanyika kwenye majengo ya serikali ambapo mengi yake yamepambwa kwa bendera ya Zanzibar na taa kuwaka katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar.
Sherehe hizo kesho zinatarajiwa kufikia kilele chake katika uwanja wa Amaani Mjini Unguja, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Dk. Shein, katika sherehe hizo atapokea gwaride rasmi la vikosi vya ulinzi na usalama, na kupokea maandamano ya wananchi kutoka Wilaya za Unguja na Pemba, taasisi za serikali, Mashirika, Wizara za serikali na wanafunzi wa vyuo.
Viongozi mbali mbali wanatarajiwa kushiriki akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na mabalozi wanaofanya kazi zao nchini Tanzania.
Jumla ya miradi 45 ya maendeleo imefunguliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika maadhimisho ya sherehe hizo katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Monday, 10 January 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment