Saturday, 8 January 2011

JIHAD AZITAKA TAASISI ZA HABARI KUSAIDIA UKUZAJI MAENDELEO.

Jihad azitaka taasisi za habari kusaidia ukuzaji maendeleo

Na Issa Mohammed

WAZIRI wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan, amewataka wafanyakazi wa vyombo vya habari, kutanguliza uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao, ili azma ya kuijenga Zanzibar mpya ifikiwe.

Alisema wafanyakazi wa sekta ya habari wana nafasi, uwezo na mchango mkubwa katika maendeleo ya kuijenga Zanzibari inayohitajiwa na wananchi.

Waziri Jihad, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Idara ya Habari Maelezo na Shirika la Magazeti, hapo Rahaleo mjini Zanzibar.

Alisema uzalendo unahitajika katika utekelezaji wa kazi zao ambazo ni muhimu katika kustawisha maendeleo kwenye sekta mbali mbali visiwani Zanzibar.

Alihimiza kuwepo na mashirikiano katika kutekeleza majumu hayo, hasa ikizingatiwa kwamba ushirikiano ndiyo siri kubwa ya kufikia malengo yanayokusudiwa.

Waziri Jihad, aliwaahidi wafanyakazi hao, kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa wizara atajitahidi kuvisimamia na kubiimarisha vyombo vya habari sambamba na kuvipatia vitendea kazi.

''Nimepewa dhamana ya kuvisimamia vyombo vya habari nitajitahidi kuhakisha vinaimarika hata ikibidi ni kwa kuviombea misaada kutoka nje'',alisema Waziri Jihad.

Nae katibu mkuu wa wizara hiyo Ali Mwinyikai akizungumza kwenye mkutano huo aliwahakikishia wafanyakazi hao kwamba serikali iko katika mipango ya kutengeneza maslahi mazuri ya wafanyakazi wa vyombo hivyo.

Hata hivyo alisema wakati serikali ikijiandaa kutekeleza azma hiyo ni vyema wafanyakazi kwa upande wao wakiwemo waandishi wa habari,watangazaji na mafundi mitambo wajitahidi kufanya kazi kwa bidii kwa.

Katika mkutano huo wafanyakazi hao walilalamikia zaidi uhaba wa vitendea kazi pamoja na maslahi yao kuwa duni yasiyolingana na ugumu wa kazi zao.

No comments:

Post a Comment