Tuesday, 25 January 2011

HAJA BINAFSI YA TUNDU LISSU YAIVA

Hoja binafsi ya Tundu Lissu yaiva

Na Jumbe Ismailly, Singida

MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, amedhamiria kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho cha Bunge, ambayo ina madhumuni ya kutaka iundwe kamati ya Bunge kuchunguza matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI).

Mbunge ambaye ni mwanasheria maarufu, alitangaza azma hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hoteli ya Aque Vitae, iliyopo mjini Singida.

Alisema katika hotuba ya Waziri mkuu aliyoitoa katika kikao cha Bunge cha mwezi Juni, mwaka jana, serikali kupitia Bunge hilo ilitenga fedha nyingi kwa ajili ya Mkoa wa Singida kugharamia sekta ya elimu.

Alisema katika fedha hizo zilizoidhinishwa na Bunge hadi kufikia mwezi Machi mwaka jana ni shilingi 1,187,000 ndizo zilizokuwa zimetumika na kwamba 905,000,000 zilirudishwa hazina baada ya kukosa kazi ya kufanya.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili Mkoa wa Singida umerudisha Hazina zaidi ya shilingi 1,350,000,000 zilizokuwa zigharamie sekta ya elimu huku akihoji kwa nini wananchi wachangishwe wakati fedha zinarejeshwa hazina.

"Watanzania wangependa kujua hizi fedha zimerudi kweli hazina au zimetumika kwa mambo mengine tusiyoyajua, ndiyo sababu nyingine ya kupeleka hoja binafsi ya kutaka Bunge lichunguze hii ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, ili Bunge linalotoa fedha liridhike kwamba kweli hii fedha haijatumika visivyo”,alisema Lissu.

Mbunge huyo alihoji sababu zilizofanya zisitumike wakati Watanzania wanachangishwa fedha kwenye elimu kwa nguvu bila kuwepo sheria na utaratibu.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Dar-es-Salaam, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Singida,Yusufu Kipengele alikanusha habari hizo na kuongeza kwamba mpaka sasa ofisi yake inadaiwa na wazabuni wadogo wadogo shilingi milioni 16.

"Mimi mwenyewe nadaiwa na wazabuni wadogo wadogo shilingi milioni kumi na sita kwani mpaka sasa hupatiwa fedha kidogo tu za kuendeshea ofisi na ninavyofahamu mimi ni kwamba kila Halmashauri inadaiwa na wazabuni wa aina hiyo siyo chini ya shilingi milioni ishirini kila moja", alisema.

No comments:

Post a Comment