Saturday 8 January 2011

WANAOUZA EKA TATU WANASALITI DHAMIRA YA MAPINDUZI -- BALOZI SEIF.

Wanaouza eke tatu wanasaliti dhamira ya Mapinduzi – Balozi Seif

Na Mwantaga Ame

MKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, amesema wananchi wanaoiuza ardhi ya eka tatu walizopewa na serikali baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, ni sawa na kuisaliti dhamira ya Mapinduzi hayo.

Balozi Iddi aliyasema hayo kwenye uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha Mafunzo ya kusindika matunda na viungo huko Kizimbani Wilaya ya Magharibi Unguja.

Alisema dhamira ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, kutoa eka tatu kwa kila mwananchi ilikuwa ni hatua ya kumiliki ardhi baada ya hapo awali kukosa fursa hiyo kutoka kwa watawala wa kikoloni.

Alisema muasisi wa Mapinduzi hayo, alifanya hivyo kwa lengo la kuwafanya wananchi kutumia ardhi hiyo kwa uzalishaji wa kilimo ili kiwasaidie katika ujenzi wa maisha yao kwa kutambua wengi wa wananchi walikuwa ni wakulima na wanaishi vijijini.

Balozi alisema malengo hayo mema yaliyowekwa na Mzee Karume, wapo baadhi ya wamekuwa na tabia ya kuisaliti dhamira hiyo kwa kuziuza eka tatu hizo, huku pia wakikibali kuwa vibarua wa kuyalima kutoka kwa waliowauzia.

Makamu huyo alisema huo ni sawa na utumwa ambao ulipingwa na Marehemu Mzee Karume, na ni vyema walioanzisha tabia hiyo kuacha kufanya hivyo ili wandeleze dhamira njema ya kiongozi huyo.

Alisema ingawa sekta hiyo imeonekana kupatwa na matatizo katika kuimarisha kilimo lakini serikali ya awamu ya saba tayari imeandaa mikakati itayowawezesha wakulima wa Zanzibar kuwa na tija.

Katika hafla hiyo, Balozi huyo alifahamisha kuwa hatua ya serikali ya Korea kuamua kuanzisha majengo yatayotumika kusindikia matunda na viungo ni moja ya ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar, na ni mafanikio ya matunda ya Mapinduzi katika miaka 47.

Alisema serikali ya Awamu ya Kwanza iliweza kuanzisha viwanda vingi lakini ilisahau umuhimu wa kuwapo kiwanda cha aina hiyo ambapo kimewasababishia wakulima wengi kukosa matunda ya mazao wanayoyazalisha na kubakia yakiwaozea bila ya kujua nini cha kufanya.

“Inatupasa tuone umuhimu wa kutunza misaada hii, hapa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa shilingi milioni 600 lakini wenzetu kwa udugu tulionao wametupa pesa nyingi sasa lazima tuthamini na kutunza mradi huu sio wakiondoka mradi unakufa maana katika vichwa vyetu hatuna tabia ya kufanya marekebisho”, alisema Balozi.

Alisema serikali itawazesha wahitimu watakaopata mafunzo hayo kwa kupatiwa fedha kwa ajili ya kuanzisha viwanda vyao vidogo vidogo ili waweze kuwa na ajira pamoja na kuondokana na umasikini.

Balozi Iddi, aliipongeza serikali hiyo ya Korea kwa msaada wake kuendeleza kilimo cha Umwagiliaji maji katika bonde la Kibokwa na kuwataka watendaji wa Wizara kuithamini miradi hiyo ili iwajengee matumaini wafadhili wazidi kuisaidia Zanzibar.

Mapema Waziri wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid, alisema kuwapo kwa kituo hicho kitaweza kupunguza tatizo la masoko kwa bidhaa zinazozalishwa na wakulima hapa nchini na kuongeza thamani zaidi.

Nae Blozi wa Korea nchini Tanzania, alisema serikali yake inafurahi kwa kiasi kikubwa kuanzisha mradi huo kwa vile utaweza kukuza udugu na wananchi wa Zanzibr.

Alisema serikali yao imeamua kutoa msaada huo kwa kutambua eneo kubwa la Wazanzibari ni wakulima na ili wafanane na wezao wa korea ni jambo la msingi kuwapatia vitu muhimu vitavyowawezesha kukuza sekta hiyo ambapo tayari wameanza kuliimarisha eneo la kilimo huko Kibokwa.

Balozi huyo pia aliwapongeza wanawake wa Zanzibar kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika sekta hiyo ya kilimo na kuwatak kuendeleza jitihada hizo.

Mradi huo unatarajia kutumia dola za kimarekani 2.3 ambapo serikali ya Zanzibar imechangia milioni 600 ambapo baada ya kukamilika utaweza kutoa mafunzo na kusindika matunda kwa kutengeza juisi na bidha nyengine, muhogo, na kupeki viungo ikiwa pamoja na kuwa na maabara ya kuangalia viwango vya mazao tayayoingizwa kwenye kiwanja hicho.

No comments:

Post a Comment