Thursday 13 January 2011

MAALIM SEIF ALIA NA POLISI OMBA OMBA

Maalim Seif alia na Polisi omba omba

• Amtaka Nahodha kuondosha aibu hiyo jeshini
Na Abdi Shamnah

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Sharrif Hamad, amechukizwa na tabia inayoofanywa na baadhi ya askari polisi katika viwanja vya ndege na bandarini, kuwa omba omba kwa wageni wanaoingia nchini.

Maalim Seif alieleza hayo ofisini kwake Migombani, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye alifika kubadilishana mawazo na kupata ushauri juu ya changamoto mbali mbali zinazoikabili Wizara yake.

Alisema zipo taarifa za uhakika kuwa baadhi ya askari wasiokinai katika maeneo hayo, wamekuwa na tabia ya kuombaomba kwa wageni hasa watalii hali inayowafanya wageni hao wakose raha.

Alisema vitendo hivyo sio vinalitia aibu jeshi hilo bali pia vinaitia aibu nchi na vimeshazoeleka kwa askari hao na hushamiri zaidi katika misimu ya utalii.

Maalim Seif alitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya askari hao wachache ambao wanalitia aibu jeshi hilo, na kutaka uwepo mfumo maalum wa kuwatafuta askari wenye tabia njema na kuwapanga katika maeneo hayo.

Aidha alipendekeza uwepo utaratibu wa kuwahamisha mara kwa mara askari wanaokaa katika maeneo hayo, ikiwa ni njia moja ya kuondosha tabia hiyo.

Maalim Seif pia alitumia fursa hiyo kumueleza Waziri Shamsi kuwa jeshi la Polisi hasa kikosi cha Usalama Barabarani kinanuka rushwa kwa kuvikamata vyombo vyenye makosa na kufanya nao mazungumzo badala ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Alisema haoni mantiki yoyote kwa askari kumkamata dereva kutokana na kosa la usalama barabarani na baadae kukaa kando na dereva wakizungumza kwa masaa kadhaa.

Alisema hatua hiyo inachangia ongezeko la ajali na idadi ya vyombo vibovu, ambavyo huachiliwa kutembea barabarani.

Katika hatua nyengine Maalim Seif alisema moja ya changamoto inayoikabili Zanzibar wakati huu ni wimbi la uingiaji wa wageni, bila ya kujulikjana uraia wao na hivyo kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa kitambulisho cha Kitaifa.

Nae Waziri Shamsi alisema suala la Kitambulisho cha Kitaifa limo katika mchakato wa kumpata mkandarasi wa kutengeneza, ambapo utekelezaji wake utakuwa kwa awamu mbili tofauti.

Alisema awamu ya kwanza itakuwa kwa watu ambao taarifa zao zinafahamika, kama wafanyakazi na utekelezaji unatarajiwa kuanza Juni, mwaka huu wakati awamu ya pili itawahusu watu ambao taarifa zao hazifahamiki, uliolengwa na wataalamu kutekelezwa 2014.

Hata hivyo kutokana na suala lenyewe kuwa la muda mrefu pamoja na umuhimu wake, alishauri kuangalia uwezekano wa muda huo kufupishwa hadi 2012.

Aliainisha kuwa pale mradi huo utakapokamilika, kila Mtanzania atastahiki kupata kitambulisho hicho, hivyo Wazanzibari watakuwa na vitambulisho viwili ikiwemo kile cha Mzanzibari.

Akizungumzia uimarishaji wa jeshi la Polisi, Shamsi alisema hivi sasa kuna programu maalum ya muda mfupi iliyoandaliwa kuimarisha jeshi hilo kwa kulipatia nyenzo bora za kisasa pamoja na taaluma kwa watendaji wake, hususan ile ya sheria na kada ya upelelezi.

Alisema kumeibuka wimbi la makosa ya wizi wa fedha kupitia mitandao na kuwa kuwa hilo ni eneo moja ambapo Wizara yake inalenga kulishughulikia mapema iwezekanavyo, kwa kuamini kuwa sekta ya fedha ndio mhimili mkuu wa uchumi wa nchi.

Akizungumzia juu ya uhalifu wa kutumia silaha na ujambazi, Shamsi aliiomba Serikali kulinda mafanikio makubwa yalioifikiwa wakati wa awamu ya sita ya Uongozi katika kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo.

No comments:

Post a Comment