Tuesday, 25 January 2011

MAREKANI KUIWEZESHA TANZANIA KATIKA KILIMO.

Marekani kuiwezesha Tanzania katika kilimo

Na Premi Kibanga, Dar es Salaam

Tanzania imeteuliwa kuwa moja ya nchi nne duniani itakayofaidika na mpango maalum wa serikali ya Marekani unaojulikana kama Feed The Future (FTF).

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso E. Lenhardt alimueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam.

“Huu ni mpango maalum unaolenga katika kuendeleza na kukuza kilimo, kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza uhaba wa chakula”, Balozi Lenhardt alimueleza Rais Kikwete.

Balozi huyo alimuhakikishia Rais Kikwete kuwa Marekani imekusudia kushirikiana na Tanzania katika juhudi za kuinua kilimo.

Balozi Lenhardt, alisema mpango huu sio tu utaongeza upatikanaji wa chakula nchini, lakini pia utaongeza uwezo wa Tanzania katika kufanya mambo mengi zaidi katika sekta ya kilimo.

"Mpango huu utaipatia Tanzania vitendea kazi na kuiwezesha kujenga uwezo wa kuzalisha zaidi na kutengeneza fursa nyingi zaidi", aliongeza Balozi huyo.

Nchi zinazolengwa katika mpango huu ni Tanzania, Ghana, El Salvador na Ufilipino.

Balozi Lenhardt alisema Tanzania na nchi hizo zimechaguliwa kutokana na juhudi zake katika utawala bora, juhudi za kukuza kilimo, kuwa ardhi ya kutosha, na maji.

Balozi Lenhardt alisema

maeneo yatakayoanza kufaidika na mpango huu ni Zanzibar, Morogoro, Dodoma, Manyara, na maeneo ya kanda za juu Kaskazini na za Kusini mwa Tanzania.

Kwa upande wake Rais Kikwete, aliishukuru serikali ya Marekani na alimueleza Balozi Lenhardt kuwa msaada huu ni muhimu kwa Tanzania katika sekta ya kilimo ambayo inabeba asilimia 80 ya ajira yao.

"Tukiongeza uzalishaji katika kilimo tutaweza kuwafikia Watanzania kwa asilimia 80 ambao wanategemea kilimo, na huo ni msaada na juhudi kubwa sana”. Rais alisema.

No comments:

Post a Comment