Thursday, 6 January 2011

WANACHOHITAJI WENYE ULEMAVU NI MFUMO UNAOTOA FURSA SAWA.

‘Wanachohitaji wenye ulemavu ni mfumo unaotoa fursa sawa’

Na Ismail Mwinyi
 Alhamisi Januari 6, 2011


JAMII imetakiwa kuachana na mawazo mgando kwamba watu wenye ulemavu wanahitaji huruma kutoka kwa watu wengine badala yake wanahitaji mfumo bora wa kijamii ambao unatoa fursa sawa na makundi mengine.

“Dhana hii tuipige vita kabisa kwa sababu shilingi 300 utakazompatia kwa sababu yuko barabaran hazimsaidii, anachohitaji ni upatikanaji wa fursa sawa kama makundi mengine,” alisema Dk. Charles Sokile, wakati wa mafunzo ya kuripoti habari za watu wenye ulemavu kwa waandishi wa habari, yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Dk. Charles alisema jamii inaamini kwamba ulemavu ni ugonjwa na ndio sababu serikali imekuwa ikiwaweka watu wenye ulemavu chini ya Wizara zinazowahudumia wagonjwa (Wizara ya Afya), mtazamo ambao unapaswa kupigwa vita.

Akizungumzia chanzo cha ulemavu, Dk. Charles alisema chanzo chake kikuu ni umaskini, ambao unasababisha kutopata matunzo mazuri kwa mtoto wakati akiwa tumboni, kutofikiwa na huduma za utengamano na kwa pamoja hali hizo husababisha ulemavu.

Aidha alisema takwimu zinaonesha zaidi ya watu milioni 600 wana ulemavu na kati yao asilimia 70 wanapatikana katika nchi zinazoendelea hasa katika familia duni, lakini ni asilimia mbili tu ndio wanaopata huduma na nyenzo muhimu.

Dk. Charles aliongeza kuwa asilimia 80 ya watu wenye ulemavu hawana ajira au chanzo cha mapato kinachoeleweka.

Kwa upande wa takwimu za kitaifa, mtaalamu huyo wa masuala ya watu wenye ulemavu alisema Tanzania Bara kuna idadi kubwa ya walemavu ikilinganishwa na Zanzibar, ambapo kwa ujumla asilimia 7.8 ya Watanzania wana ulemavu.

Akigusia masuala ya kuripoti habari za watu wenye ulemavu, alisema matumizi ya lugha kwa watu wenye ulemavu bado ni tatizo sugu kwa waandishi wa habari.

Aliwaasa waandishi wa habari kutanguliza utu kwanza wanaporipoti habari za watu wenye ulemavu badala ya kuangalia ulemavu wao sambamba na kuzipa kipaumbele habari za watu wenye ulemavu.

Mafunzo hayo ya siku moja yamewahusisha waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali kutoka Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment