Wednesday 19 January 2011

MASHARTI YA KUWANIA USPIKA WA BARAZA YAREGEZWA.

Masharti ya kuwania Uspika wa Baraza yaregezwa

 Serikali yasema ni utanuzi wa demokrasia
Na Mwantanga Ame


SERIKALI imeregeza masharti ya kanuni yatayowapa fursa wananchi kugombania nafasi ya Uspika wa Baraza la Wawakilishi.

Wananchi watapewa fursa hiyo baada ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi jana kurekebisha kanuni hiyo muhimu ambayo itampata kiongozi wa Baraza hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, aliwasilisha marekebisho hayo ambapo alilieleza Baraza hilo kuwa serikali imeamua kuzipitia kanuni hizo ili ziweze kutoa nafasi zaidi katika ufanyajikazi serikalini.

Aidha waziri huyo alisema serikali imewasilisha marekebisho hayo ili kutoa nafasi zaidi utanuzi wa demokrasia katika baadhi ya shughuli zake.

Alisema kutokana na hali hiyo Waziri, huyo alisema vipengele kadhaa mvimeamualiwa kufutwa na kuandika upya vikiwemo ambayo vimekuwa vikitoa nafasi ya kuwania nafasi ya Uspika ambapo hapo awali nafasi hiyo ilikuwa inawaniwa hadi mtu apate udhamini wa wajumbe watano wa Baraza hilo.

Alisema sharti hilo kwa kiasi kikubwa lilionekana kwenda kinyume na katiba ambapo imekuwa ikitoa nafasi ya nafasi hiyo kuwaniwa na mtu mwenye sifa baada ya kuthibitishwa na Chama chake bila kigezo hicho cha kupata Wajumbe watano.

Alisema mabadiliko mapya ya kanuni hayo katika kifungu cha tano yatabakia kama yalivyo ya kutaka idadi ya Wajumbe wa Baraza hilo kumuunga mkono kwa watano itabakia lakini itatolewa nafasi kwa wagombea kuweza kuungwa mkono na watu watano wasio wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Alisema kanuni hiyo mpya itawapa uhuru wa kuweza kujieleza mbele ya Baraza na kuwapa uhuru wajumbe wa Baraza hilo kuuliza masuala yasiyozidi matatu kwa kila mgombea ikiwa pamoja na kazi ya kuhesabu kura kufanywa bila ya kuwapo kwa Mjumbe wa Tume ya uchaguzi.

Eneo jengine ambalo alilitaja ni pamoja na kuanzisha nafasi ya Mnadhimu Mkuu wa serikali badala ya utaratibu wa sasa wa mnadhimu Chama Tawala na Upinzani ambapo zinafutwa nafasi hizo na watendaji hao na kubakishwa kuwa ni wanadhimu wa vyama.

Waziri huyo alitaja eneo jengine litahusu kanuni ya lugha ambazo zitaweza kubadili baadhi ya lugha zilizokuwamo katika kanuni hizo.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi, Ali Abdalla Ali, alisema kuwa marekebisho hayo ni muhimu kufanyika kwa vile yataweza kuweka uwiano katika mihimili mikuu ya dola.

Akitoa maelezo yake hayo alisema suala la kuweka mshauri wa Baraza kuwa na uzoefu wa kisheria unaofanana na uteuzi wa Majaji na makaimu Jaji unaowataka kuwa na uzoefu wa miaka saba, jambo ambalo litaweza kuleta uwiano kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Wajumbe wa Baraza hilo Omar Shehe Mwakilishi wa Chake-chake, Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan na Mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni Hamza Hassan Juma, walisema marekebisho yaliofanywa katika kanuni hizo ni ya msingi ambapo yataweza kwenda sambamba na Katiba ya Zanzibar.

Walisema uhuru uliotolewa wa kuingizwa kwa wagombea wa nafasi Uspika katika baraza hilo kutaweza kuwapa uwezo wajumbe kuwahoji wagombea ikiwa ni hatua itayowawezesha kupima uwezo kwa wagombea.

Hata hivyo wajumbe hao walitoa tahadhari ya kuwekwa sawa baadhi ya vifungu hivyo kuona namna ya kuweka vigezo vitavyoweza kuzuiya watu ambao wataonekana kuwania nafasi hizo huku wakiwa hawana vigezo halisi.

Waziri Aboud, akijibu hoja za wajumbe hao alisema kuwa atahakikisha kuwa kanuni hizo zinafanya kazi vizuri ambapo Wajumbe wa baraza hilo tayari wamezipitisha.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinatarajiwa kuendelea tena leo ambapo Wajumbe hao watafanya kazi ya kuijadili hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment