Thursday, 20 January 2011

WAZIRI ABOUD ATAKA WATOTO WAFUNZWE HISTORIA.

Waziri Aboud ataka watoto wafunzwe historia

Na Yunus Sose, STZ

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, amewataka wazee wa kijiji cha Kizimkazi Mkunguni, kutafuta mbinu za kuwafundisha watoto wao umuhimu wa kuielewa na kuitunza historia ya skuli yao.

Aboud alisema kueleweka hitoria hiyo kutakuwa kivutio kwa watalii na kuwa kielelezo cha historia kwa vizazi vijavyo.

Alisema Zanzibar ni moja ya visiwa vyenye rasilimali nyingi za kihistoria hivyo, wananchi wa sehemu hizo wanapaswa kuziendeleza rasilimali hizo kwa kuzitunza na kuzijengea mazingira ambayo wageni wanaweza kuvutika.

Waziri Aboud aliyaeleza hayo alipozungumza na wajumbe wa kamati ya maendeleo ya kijiji cha Kizimkazi Mkunguni, kamati ya Shehia, kamati ya skuli baada ya kukabidhi shilingi milioni 1.5.

Fedha hizo alikabidhi kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alizoahidi kusaidia ujenzi wa jengo jipya la skuli ya Kizimkazi katika sherehe za kutimia miaka mia moja kwa skuli hiyo zilizofanyika mwishoni mwa Disemba alipohudhuria akiwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo.

Alisema serikali kwa upande wake itaendelea kuwaunga mkono wananchi wanapoanzisha miradi ya maendeleo, kuhakikisha inamalizika kwa wakati.

Alizipongeza kamati za kijiji cha Kizimkazi kwa kuwa na nguvu moja na kuonesha mshikamano, hali ambayo wananchi wa kijiji hicho wamekuwa mfano katika harakati za kujiletea maendeleo

"Serikali inatambua mchango wenu wa kuendeleza miradi ya maendeleo lakini hili la kuendeleza historia ya skuli yenu msije mkalifanyia mzaha na ni vyema mkaliandalia utaratibu wa kufanyika sherehe za aina hiyo kila mwaka," alisema waziri Aboud.

Aliwafahamisha wananchi wa kijiji hicho ambapo ujumbe wake uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mustapha Mohamed Ibrahim kuielezea historia halisi ya wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ili nao wawe na upeo wa historia yao wasijekupotoshwa na watu wengine ambao wanatoka nje ya kijiji hicho.

Akitoa salamu za wanakamati za kijiji hicho, Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kijiji hicho, Hassan Mkadam Khamis ameipongeza ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kutochelewesha ahadi wanazozitoa jambo ambalo limekuwa likiwapa moyo mkubwa wananchi hasa wa vijijini.

No comments:

Post a Comment