5bn/-zalipwa fidia upitishaji umeme Fumba, Mtoni
Na Mwanajuma Abdi
SHILINGI Bilioni tano zimetumika kuwalipa fidia wananchi watakaoathirika wakati wa uwekeji waya wa pili wa umeme kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar wenye uwezo wa kuchukua megawati 100.
Akizungumza na gazeti hili, Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Salum Abdallah Hassan amesema fidia hiyo imeshakabidhiwa wananchi watakaoathirika wakati utakapoanza mradi huo.
Alifafanua alisema kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 2.6 zimetolewa na wafadhili wa mradi huo Shirika la Changamoto la Mellinium (MCC) la Marekani ambazo zimelipwa kwa wananchi wataoathirika na upitishaji wa waya mpya wa umeme wa baharini kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba na kutoka Fumba kupelekwa Mtoni wa watu wanaoishi upande wa Magharibi.
Aidha, alieleza kuwa Shilingi Bilioni 2.4 zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuwafidia wananchi na vipando vyao walioko upande wa Mashariki kutoka Fumba hadi Mtoni ambapo kutahamishiwa waya wa umeme wa kati uliokuwepo Magharibi kwa sasa.
Afisa huyo wa shirika la umeme alifahamisha kuwa, matayarisho ya kazi ya uwekaji wa waya huo mpya, wenye uwezo wa megawati 100 yanaendelea, ikiwemo ujenzi wa vituo vya umeme huko Ras Kiromoni Tanzania Bara.
Alisema kazi ya utengenezaji wa waya huo inaendelea nchini Japan, ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2012.
Mradi wa utengezaji waya wa pili wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar unafanywa na kampuni ya VISCAS ya Japan, ambao utagharimu Dola za Marekani 28,210,400, ambapo fedha hizo zitatolewa na MCC.
Kukamilika kwa mradi huo, Zanzibar itaongeza kiwango cha umeme kutoka megawati 45 zilizokuwepo sasa hadi kufikia megawati 100, ambazo zitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
Tuesday, 18 January 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment