Tuesday 25 January 2011

ABBAS KUIBEBA ZANZIBAR OCEAN VIEW AFRIKA

Abbas kuibeba Zanzibar Ocean View Afrika

Na Salum Vuai
Jumatano  Januari 26, 2011.
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimemruhusu kocha wa timu za vijana Abdelfatah Abbas, kuungana na benchi la ufundi la wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Zanzibar Ocean View, kuisaidia katika resi za kusaka ubingwa.

Msaidizi Katibu wa ZFA Masoud Attai, amesema chama chake kimeridhia ombi la mabingwa hao wa soka Zanzibar kwa vile kinatambua ushiriki wake kwenye mashindano hayo, ambapo itakuwa ikipeperusha bendera ya Zanzibar.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo Hashim Salum, amesema baada ya kutafakari ugumu wa michuano hiyo, uongozi wa klabu yake umeona ni vyema umpate kocha huyo ili kuliongezea nguvu benchi la ufundi, na kwa kuwa inaamini ana uwezo mkubwa wa kuisaidia ili iweze kufanya vizuri.

Hata hivyo, amefafanua kuwa kocha huyo raia wa Misri, atafanya kazi na kikosi chake kwa ajili ya mashindano hayo tu kwa kadiri itakavyoendelea, na baada ya hapo atarudi kushughulikia kazi iliyomleta nchini kuzinoa timu za taifa.

Aliongeza kuwa, Mmisri huyo ambaye tayari ameanza kibarua hicho tangu Jumatatu iliyopita, atashirikiana na makocha wa timu hiyo Said Omar Kwimbi pamoja na Saleh Ahmed ‘Machupa’, kuiandaa timu hiyo inayokabiliwa na kazi ngumu ya kuwatoa wawakilishi wa DRC AS Vita, kwenye kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza na gazeti hili jana asubuhi kwenye uwanja wa Mao Tsetung ambako kikosi hicho kinafanya mazoezi yake,

Abbas alisema amefurahishwa mno na uonozi wa timu hiyo kumuona anafaa kutoa mchango wake, na kuahidi kuwa atashirikiana vyema na wenzake kuhakikisha wanaleta mafanikio.

“Ingawa nimeletwa kufundisha vijana wa timu za taifa, lakini kwa kuwa niko Zanzibar najiona ni miongoni mwa raia wa nchi hii, hivyo niko tayari wakati wowote kuisaidia klabu yoyote itayonitaka hasa kwenye michuano ya kimataifa”, alifafanua Mmisri huyo.

Hiyo itakuwa mara ya tatu kwa kocha huyo kuzisaidia klabu za Zanzibar zinaposhiriki mashindano ya klabu barani Afrika, ambapo mwaka jana aliibeba Miembeni ilipoikabili Petro Jet ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho,

Aidha mwaka huohuo, alikwishaanza kuinoa Mafunzo iliyokuwa ikijiandaa kwa mashindano ya Kombe la Kagame, lakini akaiacha njiani kutokana na suitafahamu iliyoibuka kati yake na benchi la ufundi la timu hiyo.

Zanzibar Ocean View inaanza kutupa karata yake ya kwanza Jumapili Januari 30, kwenye uwanja wa Amaan, kwa kuikaribisha AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kabla kurudiana nayo wiki mbili baadae mjini Kinshasa.

No comments:

Post a Comment