Tuesday 25 January 2011

WAWAKILISHI WACHOSHWA UINGIZAJI BIDHAA MBOVU

Wawakilishi wachoshwa uingizaji bidhaa mbovu

Wataka wanaoingiza wasifumbiwe macho
Na Mwantanga Ame

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka serikali kutowaonea haya wafanyabiashara wadanganyifu wanaoingiza nchini bidhaa zilizopitwa na wakati.

Wajumbe hao walieleza hayo jana walipokuwa wakichangia Mswada wa Sheria ya kuweka masharti ya uendelezaji, ukuzaji na uwekaji wa Viwango na Ubora wa Bidhaa, uliowasilishwa na Waziri wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui.

Wajumbe hao walisema wakati wa kufumbiwa macho waingiza bidhaa zisizo na viwango kwa kuangalia misingi ya udugu, ujamaa na urafiki umepitwa na wakati.

Walisema hatua ya serikali kuuwasilisha mswada huo wa sheria ni jambo la msingi kwani awali walishindwa kulifanyia kazi suala la bidhaa hizo, kutokana na baadhi yao kutishiwa maisha na kufukuzwa kazi na wanaowalinda wahusika hao.

Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisema kuliwahi kutishiwa maisha kwa watu watakaowachukulia hatua waingiza bidhaa mbovu nchini.

Alisema wakati serikali ikiwa katika hatua ya kuisubiri sheria kufanya kazi zake ingepaswa kuwabana wafanyabiashara wa soko la ndani kutengeneza biashara zao katika viwango, kwani inawezekana kabisa wafanyabiashara wasipowekewa masharti wakasababisha bidhaa za wengine zikashindwa kutumia masoko ya nje kama ilivyojitokeza katika biashara ya embe iliyozuiliwa Dubai kutokana na kupigwa moto.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahmoud Mussa alisema ni vyema serikali wakati ikipitisha sheria hiyo kuviangalia vipengele vilivyomo visiweze kumtia hasara mfanyabiashara wa Zanzibar, kutokana na uzembe wa baadhi ya mawakala.

Akifafanua kauli hiyo alisema baadhi ya mawakala wamekuwa wakiingiza mizigo ya watu bila ya kuzingatia nchi inakokwenda, jambo ambalo linaweza kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wa Zanzibar itapobainika kuwa bidhaa alizobeba si zake na hazina kiwango.

Kwa upande wake Mwakilishi Abdalla Juma, alisema ni vyema kwa serikali baada ya kupitishwa sheria hiyo ibadilike katika kulisimamia tatizo hilo, kwani Zanzibar imegeuzwa jaa la utupaji wa vyakula vibovu pamoja na vifaa visivyofaa kutumiwa vikiwemo vya ujenzi.

Alisema hivi sasa kuna bidhaa za asilimia 80 katika maduka ya Zanzibar zimeonekana hazina viwango hasa mchele jambo ambalo tayari limewasababishia baadhi ya watu kuuguwa ugonjwa wa magoti na kushindwa kutembea.

Nae Mwakilishi Suleiman Hamad, alisema kuna tatizo kubwa la baadhi ya watendaji wanaopewa majukumu katika kusimamia vitengo vya biashara kutowajibika ipasavyo jambo ambalo litahitaji kuangaliwa.

Alisema Mkemia Mkuu baada ya kupitishwa sheria hiyo inatarajiwa kuona anatekeleza majukumu yake vyema bila ya kufanya uzembe ambao utasababisha matatizo hayo kuendelea kutokea nchini.

Mwakilishi wa Mfenesini, Ali Abdalla Ali, alisema usimamizi wa sheria hiyo ni moja ya jambo la msingi ambalo litahitaji kufanyiwa kazi ili kuweza kuondolewa shaka kwa Idara itayopewa jukumu kusimamia eneo hilo.

Mwakilishi wa Viti Maalum, Raya Hamad Suleiman, alisema licha ya serikali kuliangalia tatizo hilo pia italazimika kuviangalia vitu vinavyoingizwa nchini hasa mitumba ambayo inaingizwa ikiwa imechoka kimatumizi.

Mapema Waziri wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, alisema sheria hiyo imebeba maeneo mengi yatayoweza kuleta mabadiliko ya msingi katika kuifanya Zanzibar kuwa yenye kuendesha vyema sekta ya biashara.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo, Salmin Awadh Salmin, alisema hali ya uingizwaji wa bidhaa Zanzibar bado sio nzuri kutokana na kutokuwa na uthibitisho rasmi wa kukaguliwa na zile zinazotoka nchini kwenda nje.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema inawezekana yaliojitokeza juu ya kusimamia shughuli hizo kunasababishwa na migongano ya sheria jambo ambalo sio zuri kuachiwa kuendelea kwa hivi sasa kwa vile inawezekana ndio chanzo cha kutokea yanayojitokeza sasa.

Mwenyekiti huyo alisema wakati serikali inaendelea kuandaa mazingira mazuri ya usimamizi wa viwango ni vyema ikaenda sambamba na kuandaa sheria itayokuwa inamhusu Mkemia Mkuu wa serikali ili kumuwezesha mfanyabiashara asieridhika na ukaguzi iwe anaweza kukata rufaa kwa Mkemia Mkuu.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kitaendelea tena leo ambapo wajumbe hao watayapitia masuala na majibu ya Wajumbe hao na kuyapatia ufafanuzi kutoka kwa watendaji wakuu wa serikali.

No comments:

Post a Comment