Tuesday, 25 January 2011

WATAKAONYANYASA WAFANYAKAZI KUPIGWA 'STOP'

Watakaonyanyasa wafanyakazi kupigwa ‘stop’ Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema haiko tayari kuwavumilia wawekezaji watakaowanyanyasa wafanyakazi katika sekta ya utalii kwa kukiuka sheria za nchi.

Hotuba ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdallah Shaaban ilieleza.

Taarifa hiyo ilitolewa katika Mahafali ya Chuo cha The African Utalii College iliyowajumuisha wahitimu 69 wa Diploma na Cheti, yalifanyika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Alisema serikali haitowavumilia wawekezaji wenye tabia hiyo, wakiwa wa nje ama wa ndani, ambao kwa kufanya hivyo watakuwa wanakiuka sheria zilizowekwa katika sekta hiyo ili kuweza kupata haki zao, sambamba na wale wanaofukuzwa kazi ovyo.

Kauli hiyo aliitoa kufuatia wanafunzi hao kusema kwamba kero kubwa inayoikabili sekta ya utalii ni kukatishwa kwa mikataba ghafla, kufukuzwa ovyo pamoja na kunyanyaswa.

Alisema serikali inatoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji kuja nchini kuwekeza ili uchumi uweze kuimarika lakini haipo tayari kuona watu wake wananyanyasika.

Aidha alifahamisha kuwa, mahafali hayo yawe kichocheo kwa kuimarika sekta utalii, ambayo inachukuwa nafasi kubwa katika kukuza uchumi na pato la taifa, hivyo aliwataka wahitimu hao kujituma zaidi ili kufikia malengo ya Zanzibar kuwa na wataalamu katika kada mbali mbali.

Maalim Seif alisema kuanzishwa kwa Chuo hicho Zanzibar ni ishara njema ya kukuzwa kwa viwango vya elimu katika sekta hiyo pamoja na kufikia malengo ya kuwa na utalii wenye mazingira bora ya utoaji wa huduma.

Alisema Zanzibar inasifika duniani kote kwa watu wake wanaheshimu mila na desturi zao na kutoa ushirikiano kwa wageni wanaofika nchini, jambo ambalo linasaidia kuongezeka idadi ya watalii mwaka hadi mwaka.

Hata hivyo, aliwashauri wahitimu hao kuvitumia vyeti hivyo wenyewe kwa vile ndio wataoweza kuvifanyia kazi na sio kuwapa watu wengine wasiohusika kunaweza kukasababisha mzigo kwa muajiri.

Mapema Mkuu wa Chuo hicho, Sostenes Mugeta Mafuru aliomba Serikali iendelee kuipa ushirikiano sekta binafsi na kupewa kazi wanazoweza kuzifanya wazalendo badala ya kupewa kipaombele wageni.

Risala ya wahitimu, iliyosomwa na Fatma Khamis iliiomba Serikali kuwaangalia wawekezaji katika sekta ya utalii, wanaowanyanyasa wafanyakazi wachukuliwe hatua.

Wahitimu 60 walitunukiwa vyeti vyao kwa kufaulu masomo ya kutembeza watalii, masomo ya lugha kama ya kihispania, kingereza, kitaliana na kiarabu, mafunzo ya mawasiliano ya kompyuta, mapischi na utoaji wa huduma za vinywaji na kutunza vyumba.

No comments:

Post a Comment