Friday 21 January 2011

SERIKALI IZIBE MIANYA UVUJAJI MAPATO.

serikali izibe mianya uvujaji mapato



Mwanajuma Abdi


SERIKALI imeshauriwa kuchukua kila jitihada zitakazo hakikisha inaziba mianya yote ya uvujaji wa mapato.

Mwakilishi huyo alieleza hayo jana katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akichangia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliyoitoa katika uzinduzi wa Baraza la nane la Wawakilishi Zanzibar Novemba 11 mwaka jana.

Alisema mipango ya serikali kuawezesha wananchi kuondokana na umasikini itaweza kukamilika endapo serikali itakuwa na fedha za kutosha ambazo zitapatikana kwa kuzibwa mianya inayovujisha mapato hayo.

“Wananchi bado masikini wa kawaida wanamiliki kipato cha shilingi 60,000, hivyo miwanya ya uvujaji wa mapato ya serikali izidhibitiwe kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi”,alisema Mwakilishi huyo.

Aidha Hamza alishauri vyema ingefikiriwa kuundwa kwa baraza dogo la mawaziri ambalo lingeweza kufanya kazi katika kuwakomboa wananchi kutokana na umasikini.

Alifahamisha kuwa nchi ndogo na changa kama Zanzibar hakikupaswa kuwa na baraza kubwa liliopo hivi sasa ambalo limekuwa likitumia fedha nyingi.

Alisema Zanzibar ni nchi ndogo ambayo ina mawaziri wengi karibu 24 ukilinganisha na nchi nyengine duniani, jambo ambalo husababisha matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kuwahudumia.

Alisema pamoja na serikali iliyokuwepo madarakani kujikita zaidi katika maridhiano, lakini pia mkazo uwekwe katika kuangalia umasikini ambao umekuwa ukiwakabili wananchi wengi.

Akizungumzia uharibifu wa mazingira uweze kudhibitiwa ni lazima matumizi ya misumeno ya moto ipigwe marufuku na itumike kwa watu wenye vibali maalumu.

Nae Mwakilishi Mbarouk Jimbo la Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mussa alisema mahoteli yaliyopo nchini yaangaliwe upya juu ya utoaji wa ajira kwa kwani yamekuwa yakikwepa kuajiri vijana wazalendo pamoja na kuwa na sifa na uwezo.

Akizungumzia kiwanda cha Mahonda kilichokuwa kinazalisha sukari, ambapo ajira ya watu wengi katika Mkoa wa Kaskazini, alisema kiwanda hicho kimeshindwa kufanyakazi pamoja na kupata muwekezaji.

Naye Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansour Yussuf Himid alisema Korea Kusini imesaidia Dola za Marekani milioni 53 za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji maji.

Aliongeza kusema kwamba, Serikali imetenga ekari 8,521 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji, ambapo hadi sasa ni hekta 700 ndio zimetumika Unguja na Pemba na huku nyengine zikitumika kwa kilimo cha kutegemea mvua.

Sambamba na hilo alieleza Kitengo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani kitaimarishwa zaidi ili kufanyika kwa tafiti mbali mbali zinazohusiana na kilimo pamoja na kuongeza hadhi ya Chuo cha Kizimbani kwa kutoa kiwango cha Diploma, ambapo mkupuo wa kwanza utatoka mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment