Tuesday, 18 January 2011

UNYANYASAJI WAFANYAKAZI MAHOTELINI

Unyanyasaji mahotelini utamalizwa kwa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao’

Na Juma Khamis

WAFANYAKAZI wengi wa mahotelini na utalii hawajaona umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi kiasi ambacho inavifanya vyama hivyo kushindwa kufuatilia kesi zao za unyanyasaji unaofanywa na waajiri katika sehemu zao za kazi.

Katibu Mkuu wa Chama cha wafanyakazi wa utalii, mahoteli, hifadhi, majumbani na kazi nyengine Zanzibar (ZATHOCODAWU) Maalim Makame Launi, amesema changamoto hiyo inawafanya wafanyakazi wa mahoteli na utalii kuendelea kuumia bila ya kuwa na mtetezi wa kuwasaidia.

Alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakisimamishwa kazi, kufukuzwa na mikataba yao kuvunjwa ovyo lakini vyama vya wafanyakazi vinashindwa kuwatetea kwa kukosa nguvu kisheria kwa sababu sio wanachama wake.

Alisema unyanyasaji huo zaidi unafanywa na mahoteli yanayomilikiwa na wawekezaji wa kigeni kwa sababu wanajifanya vipofu kabisa mbele ya sheria.

“Wazungu wanajifanya wako ‘blind’ na sheria kwa hivyo wanafanya wanavyotaka,” alisema Katibu Mkuu huyo.

“Hawawajali wafanyakazi, wanawanyanyasa, wananyanyapaa na kuwakandamiza,” aliongeza.

Lakini alisema changamoto kama hizo huwakuta waajiri wa sekta hiyo pia ambapo wafanyakazi hukimbia na kuhamia mahoteli mengine bila ya kutoa taarifa kama inavyotaka sheria ya mahusiano kazini ya mwaka 2004.

Alitoa mfano wa hoteli ya Ngalawa ambayo imekimbiwa na wafanayakazi wake sita bila kutoa taarifa kwa mwajiri.

Katibu Mkuu huyo alisema, changamoto nyengine husababishwa na mameneja wa mahoteli kwa kutozifahamu sheria za uongozi kwa sababu wengi wao hawakupitia mafunzo ua utawala.

Aidha alimwambia mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Kikwajuni kwamba waajiri pia hawataki wafanyakazi wao waanzishe matawi ya vyama vya wafanyakazi katika sehemu zao za kazi kwa sababu wanaona ni tishio kubwa kwao.

Mbali na hayo, alisema licha ya utalii kuwa kazi ya kudumu lakini waajiri wamekuwa wakitoa mikataba ya miezi sita tu ili wamtumie mfanyakazi bila ya kumlipa haki zake muda wake utakapomalizika na pale atakapomuhitaji tena atamuajiri kama mfanyakazi mpya.

Kwa upande wake, afisa wa hoteli ya Ngalawa, ambae hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa yeye si msemaji, alisema wafanyakazi hao walitimka bila kutoa taarifa zozote na kukimbilia hoteli ya jirani kwa kile alichokiita kufuata maslahi bora.

Alisema tofauti ya mishahara kati ya hoteli moja na nyengine inawafanya wafanyakazi kuhama kutoka hoteli moja kwenda nyengine, lakini kibaya wanachokifanya ni kutotoa taarifa. Lakini kwa bahati mbaya wanaoonekana zaidi ni waajiri pale wanapoamua kuwafukuza wafanyakazi kwa tabia mbaya ikiwemo wizi wa vifaa.

Changamoto hizo zinakuja wakati serikali ikijaribu kuimarisha sekta ya utalii kwa kukazia mashirikiano kati ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZTC) na Bodi ya Utalii Tanzania, TTB.

Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Dk. Ali Saleh Mwinyikai alisema lengo la serikali ni kuimarisha utalii ikiwa ni pamoja na kulifufua Shirika la Utalii Zanzibar, ambalo lilionekana kufa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Dk. Aloyce Nzuki alisema mashirikiano ndiyo yatakayoimarisha sekta ya utalii.

Hata hivyo, kwa upande wao wafanyakazi wa utalii na mahoteli wamesema uhamasishwaji mdogo pamoja na kutofahamu kwa undani faida watakazopata iwapo watajiunga na vyama vya wafanyakazi, imekuwa sababu ya kushindwa kujiunga navyo.

Wamesema viongozi wa vyama hivyo, wamekuwa kimya sana kufuatilia matatizo yanayowakabili, badala yake wanawasubiri wafanyakazi wa utalii na mahoteli wawapelekee ofisini.

“Mimi binafsi si mwanachama wa ZATHOCODAWU kwa sababu sijui nitafaidika na kitu gani nikiwa mwanachama, hata hapo zilipo ofisi za jumuiya mimi sipajui,” alisema Khatib Ishaka mfanyakazi wa baa katika hoteli moja kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment