Monday, 23 May 2011

DK. SHEIN ZIARANI MKOA WA KUSINI UNGUJA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akikagua shamba la mpunga Bambi katika ziara aliyoifanya jana huko wilaya ya kati. kushoto ni Waziri wa Kilimo na Maliasili Mansour Yussuf Himid na katibu mkuu wa wizara hiyo Affan Othman. (Picha na Ramadhan Othman, Ikulu).

TUREJESHE HADHI BONDE LA CHEJU- DK SHEIN

Tutalirejeshea hadhi bonde la Cheju – Dk. Shein

Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali anayoiongoza italiimarisha bonde la Cheju kwa kuliwekea miundombinu bora ili lirejee kwenye historia yake ya kuzalisha mpunga kwa wingi.
Dk. Shein alieleza hayo jana kwenye ziara yake ya wilaya ya Kati, ambapo alisema serikali itaendelea na malengo yake ya kufanyia mapinduzi kilimo ikiwa ni pamoja na kuwashirikiana na kuwasaidia wakulima kikamilifu.
Alisema ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni ambazo baadhi zimeanza kutekelezwa, zilikuwa ni za ukweli na zitawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi na wakulima wa bonde la Cheju.
Alifahamisha kuwa kilimo kinaweza kuimarika iwapo kutakuwepo kwa mbegu bora, mbolea, maji na utaalamu ambapo juhudi zitachukuliwa katika kuhakikisha wakulima wanapatiwa nyenzo hizo.
Dk. Shein alieleza kuwa serikali inaimarisha nguvu na kuwataka wakulima wasivunjike moyo na kuwahakikishia kuwa ndani ya miaka mitano sekta ya kilimo itabadilika.
Kwa upande wake Naibu waziri wa wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Issa Haji Ussi aliwahakikishia wananchi wa Cheju kuwa barabara yao kutoka Jendele hadi Unguja Ukuu imo katika mradi wa ujenzi ndani ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha ambao utaanza mwezi Julai.
Kwa upande wa huduma ya umeme, alisema umeshafikishwa katika bonde chini ya ushirikiano wa mradi wa PADEP ambao mashimo ya kusimamisha nguzo yameshachimbwa ambapo wakati wowote nguzo hizo zitawekwa yatawekwa kwa lengo la kupeleka huduma hiyo majumbani.
Nao wakulima wa Bonde la Cheju walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi zake alizozichukua za kuwatembelea na kusikiliza changamoto wanazozikabili pamoja na mafanikio makubwa waliyoyapata mwaka huu ambayo hayajawahi kutokea ndani ya miaka 15.
Katika ziara hiyo, alipokea taarifa ya mkoa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mustafa Ibrahim ambapo alieleza mafanikio yaliopatikana katika Mkoa huo pamoja na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa pamoja na changamoto zilizopo.
Baada ya taarifa hiyo ilianza kulitembelea Daraja la Mwera ambalo linaendelea na ujenzi ulioanza rasmi mwezi Januari mwaka huu ambalo linatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa Septemba ambapo ujenzi wa daraja hilo utagharimu shilingi bilioni 1.3.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Dk. Idd Lila na kampuni ya ujenzi wa daraja hilo, walieleza kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito hadi wa tani 160 kwa magari yenye line nne za matairi(4Axles),
Alisema daraja la zamani lililojengwa mwaka 1904 ambalo lilikuwa na uwezo wa kubeba tani 50 tu lilipokuwa jipya na sasa lina uwezo wa kubeba tani 5 kutokana na kuchakaa.
Akiwa katika shamba la kuku wa mayai Ubago, Dk. Shein alieleza haja ya kutolewa elimu kwa wafugaji wa kuku na kuelewa kuwa bado wapo wafugaji na wasambazaji wa kuku wazalendo ambao wanauwezo wa kuzalisha vifaranga na kuwauzia wafugaji hapa hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alizitembelea ujenzi wa skuli za sekondari za Wilaya ya Kati ikiwemo ile ya Uzini na ile ya iliyopo Jumbi ambapo zote hizo zinatarajiwa ujenzi wake kukamilika ndani ya mwaka huu na kuangalia ujenzi wa ofisi ya mkoa wa Kusini Unguja.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitembelea shamba la kuoteshea mbegu lililopo Bambi pamoja na shamba la JKU la mbogamboga na kupata maelezo juu ya uendelezaji wa mbegu mbali mbali ikiwemo mbegu ya mpunga ya Merica ambayo inachukua muda wa siku 90.

BALOZI WA UGANDA NORWAY WAIPONGEZA ZANZIBAR

Balozi wa Uganda, Norway waipongeza Zanzibar

Na Abdalla Ali
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi jana lifanya mazungumzo na Mabalozi wawili wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.
Makamu huyo awali alikutana na Balozi wa Uganda nchin Tanzania, Ibrahim Mukiibi, na baadae kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ingunn Klepsvik.
Katika mazungumo na Mabalozi hao, waliahidi kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo na kuipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa malengo yake ya kuweka maslahi ya watu wake mbele.
Kwa upande wake Balozi Mukiibi alisema uchaguzi wa nchini humo uliomalizika hivi karibuni ulikwenda vizuri na chama tawala kilishinda kwa zaidi ya asilimia 70 kwa ushindi wa jumla pamoja na Wabunge, ambao umewezesha kuwapa nguvu za utawala.
Aliziomba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuimarisha uhusiano wao wa kihistoria katika kuwaletea maendeleo watu wa nchi hizo.
Naye Balozi wa Norway, Klepsvik aliisifu Zanzibar kwa kuanzisha muundo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imesaidia kuleta utulivu nchini.
Kuhusu uundwaji wa serikali hiyo, Makamu wa Pili alisema hadi sasa ingawa ni muda mfupi lakini wanakwenda vizuri na wanaafikiana vyema katika malengo yao.
Alisema serikali ya imeundwa kwa mashirikiano na wameweka vipaumbele vya kilimo, afya na utalii ili kuimarisha uchumi na kuharakisha maendeleo ya ustawi wa wananchi.

WANANCHI WA MATEMWE WAKIWA NJE YA JENGO LA MAHAKAMA MFENESINI

MAALIM SEIF AIOMBA NORWAY ISAIDIE MAENDELEO

Maalim Seif aiomba Norway isaidie maendeleo

Asema matarajio ya wananchi makubwa mno
Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameiomba Norway, kuisaidia Zanzibar katika kukabiliana na changamoto za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii zinazovikabili visiwa hivi.
Maalim Seif, alieleza hayo jana kwenye mazungumzo yake na Balozi Norway nchini Tanzania Inguun Klespsivi, huko ofisini kwake Migombani mjini hapa.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, ni matarajio makubwa waliyonayo wananchi ya kupatikana haraka maendeleo na ustawishaji wa huduma za kijamii, huku uwezo wa serikali ukiwa hauwezi kukidhi haja hiyo kwa kipindi kifupi.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, hususan katika mkoa wa Mjini Magharibi, kutokana na miundombinu iliopo kuchakaa hali inayotia shaka usalama wa maji hayo pamoja na kumwagika ovyo.
Alisema mbali na msaada mkubwa kutoka Japan, kiasi cha shilingi milioni 163 zinahitajika ili kuondosha kabisa tatizo la maji safi na salama Unguja na Pemba.
Aidha alisema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kutoka Tanzania Bara kunakotokana na uchakavu wa waya wa baharini ni changamoto nyengine kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Hata hivyo Maalim Seif alimueleza Balozi huyo matumaini yaliopo kufikia ufumbuzi wa tatizo hilo kupitia mradi wa malengo ya Changamoto za Milenia (millennium challenge), hapo mwakani (2012).
Aidha Maalim Seif alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo tatizo kubwa la ajira linalowakabili vijana na kuelezea mipango ya serikali katika kuwajengea uwezo na kuwawezesha kiuchumi.
Alisema serikali imeweka mkazo zaidi katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula na kupanda kwa bei za bidhaa hususan mchele, kwa kutumia ardhi ndogo iliopo kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo kiasi cha hekta 8,000 zimetengwa na pale lengo hilo litakapofikiwa tatizo hilo litakuwa limetatuka kwa asilimia 60.
Alisema serikali imeandaa mipango madhubuti ya kuwafunza wakulima juu ya matumizi bora ya ardhi, ili kupata kipato kikubwa na kuinua maisha yao.
Maalim Seif aliiomba Norway kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wavuvi wa Zanzibar, ambao wamekuwa wakiendelea kuvua kwa kutumia mbinu za kizamani na vifaa duni.
Aidha aligusia tatizo la magendo ya uvuvi wa bahari kuu, ambapo makampuni mbali mbali kutoka nchi za nje, ikiwemo Japan yanahusika na uhalifu huo.
Nae Balozi Klepsivik alisema Norway itaendeleza ushirikiano wake na Zanzibar kwa faida ya nchi hizo na wananchi wake.
Akizungumzia suala la uharamia unaofanywa na jamii ya Kisomali, alisema hili ni tatizo linaloikabili dunia, ikiwemo nchi za ukanda wa Mashariki na Kati ya Afrika.

MATEMWE IKO SALAMA KIMAADILI

Matemwe iko salama kimaadili

Na Mwanajuma Abdi
SHEHA wa Matemwe Haji Sheha amesema hakuna uvunjifu wa maadili katika kijiji hicho, kwani wameweka mipaka ili mambo yanayofanyika katika fukwe yaishie huko huko.
Akizungumza na gazeti hili, huko Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja, sheha huyo alisema kijiji chake kimeweka mipaka ya mambo kwani yanayofanyika ufukweni ni marufuku kuonekana juu ambako wananchi wanaishi.
Alisema kutokana na mipaka hiyo, kijiji hicho hakina tatizo kubwa la uvunjifu wa maadili kama vilivyo vijiji vyengine, ambako hufikia hadi kutokea uvunjifu wa amani.
Sheha huyo alifahamisha kuwa wanyeji wa kijiji hicho wameelezwa wazi kutokwenda ufukweni kuiga tamaduni za kigeni ambazo hazipendezi kwa jamii.
“Matemwe kuna tamaduni za wageni, ambazo sio mila za kizanzibari, lakini tumeweza kuwaeleza wananchi wanapokwenda huko desturi na tabia za huko wasizilete mitaani ili kuhofia uharibifu wa maadili kwa vijana”, alisema.
Alieleza baadhi ya viongozi wa dini walifika ofisini kwake na kumueleza kwamba watu wanatembea utupu kwenye pwani ya kijiji hicho, ambapo alikuwa mkali kwa kuwaambia wanafuata nini huko wakati hakuna msikiti wa kusalia?.
Akizungumzia upande wa wawekezaji, alifahamisha kuwa, wana maelewano mazuri na baadhi ya vijana wa kijiji hicho na wamekuwa wakinufaika na ajira kutokana na kukua kwa sekta ya utalii.
“Kasoro ndogo ndogo zipo, lakini sio kubwa za kuweza kutugawa”. Alieleza.
Alizishauri jamii zinazoishi katika maeneo ya wawekezaji hususani katika ukanda wa utalii wabakie na tamaduni zao kwani kujiingiza huko kunasababisha migogoro isiyo ya lazima.
Alisema watu wanapokwenda katika maeneo ya utalii watakutana na mengi kutokana na wageni kuingia nchini wakiwa na tamaduni zao, hivyo sio rahisi kuzifuata zile za Kizanzibari, na kuwataka wananchi kutojiingiza katika mazingira hayo kwa vile hakuna shughuli zinazowahusu kwenda huko.
WAFANYABIASHARA na wadau wa Forodha kisiwani Pemba, wakifuatilia kwa makini mafunzo ya kuhamasishwa kulitumua vyema soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mafunzo hayo yameandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Picha na (Bakari Mussa).

WANAFUNZI 500 WASHIRIKI ZOEZI LA UPANDAJI MITI

Wanafunzi 500 washiriki zoezi la upandaji miti

Na Suleiman Rashid, Pemba
ZAIDI ya wanafunzi 500 wa skuli mbali mbali kisiwani Pemba wameshiriki katika zoezi la upandaji wamiti kwenye eneo la vilima vitatu Michweni ambayo imeathirika na mazingira.
Mazingira katika eneo hilo yameharibika vibaya kutokana na uchimbwaji wa kifusi na uchongaji wa matufali ya mawe kwa ajili ya ujenzi.
Zoezi hilo la upandaji miti lina lengo la kuadhimisha mwaka wa kujitolea kwa nchi za Umoja wa Ulaya limetayarishwa na Jumuiya ya Global Network of Religion for Children (GNRC).
kwa ajili ya kuyarejesha maeneo hayo yalio athiriwa na uchfuzi wa mazingira kwa kushirikian na jamii kulipanda miti.
Akizungumza wakati wa kulizindua zoezi hilo ofisa wa utumishi wa wilaya Michewni, Hamadi Mbwana Shaame aliiomba Jumuiya ya Ulaya kuendelea kusaidia ili kuyaokoa maeneo mengi ya Micheweni ambayo mazingira yake yameathirika.
Alisema wakati harakati za binaadamu za kujitafutia maisha zikiendelea zimekuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira na kusababisha nchi kupata hasara ya kutumia fedha ili kuyarejesha maeneo hayo katika hali ya kawaida.
“Maeneo mengi ya kisiwa chetu yameharibiwa hasa hapa kwetu Michewni ukataji wa kokoto na mawe umeacha mashimo makubwa”, alisema Shaame.
Kwa upnade wake Haji Vuai Haji kutoka taasisi ya kujitolea, aliwataka wananchi wa Michewni kuitunza miti hiyo ili lengo la kutunza eneo hilo liweze kufikiwa kwa kutoikata ovyo.
Alisema wananchi wa Micheweni wanafaa kuiga mfano wa marehemu Dk. Omar Ali Juma, Makamu wa Rais wa zamani wa Tanzania, ambaye alijishughulisha kikamilifu kuwashajiisha wananchi wa Micheweni kupanda miti.
Kwa upande wake Mwalimu Asha Msabaha akiwakilisha wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali alisema kutoka na mkakati wa utunzaji wa mazingira duniani wananchi wa Micheweni kupunguza ama kuacha kuyachafua mazingiara.

WAKULIMA WATAKIWA KUACHA KUUZA MAZOA MASHAMBANI.

Wakulima watakiwa kuacha kuuza mazao shambani

Na Jumbe Ismailly, Manyoni
KATIBU wa uchumi na fedha CCM Taifa, Lameck Nchemba Mwigulu amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wakulima wilayani Manyoni, kuuza mazao yakiwa bado shambani.
Mwigulu alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mji mdogo wa Itigi, wilayani Manyoni wakati akizungumza na wanachama wa CCM wa kata za Itigi na Majengo kwenye sherehe za ushindi wa kesi ya uchaguzi iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa jimbo la Manyoni Magharibi, John Paulo Lwanji.
Alisema tabia ya kuuza chakula kikiwa shambani ni hatari na inaweza kuwaweka wananchi kwenye hali ya njaa, badala yake aliwataka wayatunze ili yaweze kuwasaidia wakati wa matatizo.
“Wana Manyoni magharibi mna bahati sana hata wakati wa hali ya hewa ilipokuwa mbaya, niliwakuta mna ufadhali kuliko sehemu zingine, kwa hiyo chakula matakachovuna nawaombeni mkitunze na msiuze kikiwa shambani”, alisema.
Akizungumzia kuhusu chama, Mbunge huyo alisema mshikamano unahitajika na kuwakumbusha wanachama wa chama hicho juu ya wajibu na umuhimu wa mshikamano ndio siri ya katika upatikanaji wa maendeleo.
Katibu huyo wa uchumi na fedha hakusita kuwashauri baadhi ya wanachama wa chama hicho walioanza kupotoshwa warejeshe akili zao kwenye mshikamano ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

TANGA FRESH YAOMBA MSAMAHA WA KODI.

Tanga Fresh yaomba msamaha wa kodi

Na Tumaini Kawogo, Dar
KAMPUNI inayojishughulisha na usindikaji pamoja na uuzaji wa maziwa ya Tanga Fresh Limited, imeitaka serikali iwasaidie kuwafutia kodi ili kukuza uzalishaji wa maziwa hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam ofisa masoko wa kampuni hiyo Chares Benjamin, alisema wamekuwa wakipata faida kidogo kutokana na kodi inayotozwa kuwa kubwa.
Alisema kampuni yao imekuwa ikizalisha bidhaa nyingine kutokana na maziwa fresh ambazo ni yoghurt, samli, jubin, na maziwa ya mtindi lakini pamoja na hilo bado imekuwa ni tatizo katika ukusanyaji mapato.
Aidha alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ambapo moja ya changamoto hizo ni kukwama kwa magari yanayosafirisha bidhaa hizo hasa katika mikoa ya Dodoma, Tanga, na Morogoro ambapo barabara zimekuwa zikiharibika kutokana na mvua nyingi zinazonyesha.
Hata hivyo alisema kuwa wanatarajia kufanya maonyesho ya usindikaji maziwa kwa makampuni 20 ya ndani na nje ya nchi ambapo yatafanyika Mei 25 hadi 27 mwaka huu katika hoteli ya Movenpick.
Aidha aliwataka wananchi kujijengea mazoea ya kunywa maziwa ili kuweza kujenga afya zao hasa kwa watoto wadogo.

GLOBAL FUND YAISAIDIA BODI YA CHAKULA

Global Fund yaisaidia Bodi ya Chakula

Na Fatma Kassim, Maelezo
BODI ya Chakula, Dawa na Vipodozi imepata msaada wa vifaa mbali mbali vya uchunguzi kutoka shirika la mfuko wa Fedha wa Dunia Global Fund vyenye thamani ya shilingi 21,852,000.
Vifaa hivyo ni pamoja na mashine ya HPLC ambayo itatumika kwa ajili ya uchunguzi na ubora wa usalama wa Chakula Dawa na Vipodozi pamoja na ‘mini lab kits’ za kuchunguzia ubora wa dawa za binadamu, mifugo na kemikali mbali mbali za kimaabara.
Mrajis wa Bodi hiyo Dk. Burhan Othman Simai alisema kupatikana kwa vifaa hivyo kutaisaidia Bodi hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na utaalamu.
Aidha alifahamisha kuwa vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka ambapo Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar itashiriki katika uwiano wa usajili wa dawa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema katika uwiano wa usajili wa dawa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutasaidia katika kupunguza tatizo la dawa zisizosajiliwa pamoja zisizofaa kwa matumizi ya mwanadamu kwa nchi za Afrika Mashariki.
Dk. Burhan alisema Bodi yake itazidi kuhakikisha kuwa dawa bandia na duni haziingii nchini kwani zinaweza kuleta athari kwa mtumiaji, na shirika la Afya Ulimwenguni linapambana na dawa hizo hususan za kutibu maleria.
Katika hatua nyengine Bodi hiyo inatarajia kufanya uchunguzi wa kina juu ya kuwekwa madini joto kwenye chumvi inayotumiwa na wananchi.
Alisema uchunguzi huo utasaidia kutambua uwekwaji wa madini joto katika chumvi na kuepusha athari mbali mbali kwa chumvi ambayo haina madini joto ambayo ni pamoja na kuwa na watoto wasio na afya ya kutosha.

AMEIR AMPANIA RAZA KATIKA KONGAMANO

Ameir ampania Raza katika kongamano

Asema halitakuwa la watu wasiojua soka
Na Donisya Thomas
LICHA ya wadau wataotaka kushiriki kongamano la soka linaloandaliwa na Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Haji Ameir kutakiwa kujaza fomu za ushiriki, mfanyabiashara Mohammed Raza atapewa mwaliko maalumu ili afahamishwe kuwa ZFA ni chama cha soka na sio cha siasa.
Makamu huyo wa Rais, amesema kongamano la wadau wa soka Zanzibar litafanyika mwishoni mwa mwezi ujao, ambapo ameonesha kukerwa na kauli ya Raza aliyoitoa hivi karibuni, kuwataka wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kuzingatia maslahi ya umma na sio ya wagombea au utashi binafsi.
Ameir amemwambia mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Bwawani, kuwa kongamano hilo linaloandaliwa kujadili changamoto mbalimbali zihusuzo soka la Zanzibar na namna ya kuzipatia ufumbuzi, linapangwa kufanyika katika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani.
Alisema kongamano hilo litawashirikisha wadau wa mchezo huo nchini kutoka makundi tafauti ikiwa pamoja na wachezaji wa zamani wakiwemo waliochezea timu za taifa za Zanzibar na Tanzania, sambamba na waandishi wa habari za michezo.
Mbali na hao, Makamu huyo alisema pia wanasheria, watu waliowahi kuiongoza ZFA kwa vipindi tafauti, makocha, waamuzi wa ligi madaraja mbali mbali, wajumbe wa mkutano mkuu wa ZFA na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watashirikishwa katika kongamano hilo.
Alisema mipango iko mbioni kununua muda katika kituo cha Televisheni Zanzibar, Sauti ya Tanzania Zanzibar, Zenj FM pamoja na Bomba FM, kwa ajili ya kutangaza moja kwa moja kongamano hilo, pamoja na kumualika mmoja wa viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa mgeni rasmi.
Hata hivyo, Haji Ameir alisema sio kila mtu ataruhusiwa kushiriki kongamano hilo, bali itatolewa fursa kwa watu maalumu hasa wale watakaowahi kuchukua fomu za kushiriki ambao wana uelewa wa mchezo wa mpira wa miguu.
Alisema siku zitakapokaribia fomu za kuomba ushiriki zitatolewa bure kwa muda maalumu, na kwamba ni washiriki waziozidi 200 ndio watakaoruhusiwa kutia mguu katika ukumbi wa Salama ambako kongamano hilo litafanyika, huku gharama zote zikitoka mfukoni mwa Makamu huyo na sio ZFA.
"Sio kila mtu atashiriki kongamano hilo, tutatoa fomu maalumu ili kupata idadi ya washiriki, na tutaanza asubuhi hadi jioni, watakaobakia nyumbani watasikiliza kupitia vyombo vya habari nilivyovitaja, hata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wataalikwa kwa idadi maalumu kwa kuangalia wale wenye uelewa wa soka miongoni mwao", alifafanua.
Kongamano hilo linaandaliwa kufuatia hali ya hewa ya soka Zanzibar kutawaliwa na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali dhidi ya uongozi wa ZFA unaodaiwa kuchangia kuporomosha kiwango cha mchezo huo nchini, na kutakiwa kuachie ngazi

WAPONGEZA MPANGO WA KUKOMESHA MAJI MNAZIMMOJA

Wapongeza mpango wa kukomesha maji Mnazimmoja

Washauri agizo la Rais lipewe kipaumbele
Na Salum Vuai, Maelezo
WAPENDA michezo mbalimbali wa Zanzibar, wamepongeza hatua ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kutaka jitihada zifanywe kurekebisha miundombinu ya uwanja wa Mnazimmoja ili kumaliza tatizo la kutuwama maji.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti, baadhi ya wananchi wamesema iwapo kauli ya Rais itafanyiwa kazi na kuurejesha uwanja huo katika hali ya kuweza kutumika kwa vipindi vyote, itakuwa faraja kubwa kwa wanamichezo wanaotumia uwanja huo kwa mazoezi.
Mkurugenzi wa klabu ya Miembeni Haji Sultan 'Kaka', amesema miundombinu mibovu inayoufanya uwanja huo kutuwama maji kila msimu wa mvua unapofika, inawanyima vijana fursa ya kuendeleza programu za mazoezi wanazojipangia, na hivyo kushusha viwango vyao vya soka.
"Kwa mfano sasa ni wakati wa masika, maji ambayo hayawezi kutolewa yamejaa, inatubidi tutafute viwanja mbadala vya mazoezi ambavyo havipo huku tukikabiliwa na mechi za ligi", alisema Sultan ambaye klabu yake inayoshiriki ligi kuu inatumia sehemu ya uwanja huo kwa mazoezi.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ZFA Wilaya ya Mjini Nassor Salim Ali 'Jazeera' ambaye pia ni Mwakilishi wa jimbo la Rahaleo, amepongeza hatua ya Rais kuzipigia upatu mamlaka zinazohusika kuufanyia matengenezo uwanja huo, akisema hatua hiyo itawaondoshea usumbufu wanasoka wanaoutumia.
"Masika yanapokuja huchukua muda mrefu, kipindi chote hicho kinawafanya wanasoka wavunde kwa kukosa mazoezi, kauli ya Mheshimwa Rais ni ya kupongezwa na tunaamini wahusika wataifanyia kazi haraka kwa sababu tunafahamu uwezo wa kurekebisha uwanja huu upo", alisema Jazeera aliyekutwa karibu na uwanja huo kwa shughuli maalumu.
Naye Abdul Mshangama ambaye ni mchezaji mwandamizi wa timu ya Wazee Sports, amesema Dk. Shein ameonesha kuguswa na maendeleo ya soka nchini, na kwamba agizo lake linaonesha namna anavyopenda vijana waendelezwe kimichezo.
Kwa miaka mingi, uwanja wa Mnazimmoja unashinda kutumika kila yanapofika majira ya mvua, kutokana na kujaa maji na kutuwama kwa muda mrefu huku wachezaji wengi wakijipa likizo za muda, ambapo Dk. Shein aliutembelea katika ziara yake ya Mkoa wa Mjini Magharibi hivi karibuni.

MBUNGE LAWAMANI KUKIMBIA MWALIKO WA WASANII.

Mbunge lawamani kukimbia mwaliko wa wasanii

Na Aboud Mahmoud
IMEELEZWA kuwa, sanaa ya filamu nchini Zanzibar, inashindwa kuendelea kwa kuwa viongozi wengi wa majimbo hawaoni umuhimu wa kuwasaidia wasanii hao wa filamu na maigizo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Sanaa ya Maigizo Zanzibar Haidhuru Filbert Haidhuru, amesema hayo wakati wa sherehe za uzinduzi wa filamu ya 'Nyakunguju' ziliyofanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa skuli ya Haile Selassie.
Haidhuru alitoa mfano wa sherehe hizo ambapo aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa jimbo moja lililoko Wilaya ya Mjini (jina tunalo), aliwaweka watu kwa muda mrefu wakisubiri ujio wake lakini akashindwa kutokea.
Hata hivyo, kwa kuwa alikuwa amealikwa rasmi kwa mwaliko wa mapema, uongozi wa jumuiya hiyo uliamua kumzindua kwa kumpigia simu majira ya saa 2:15 usiku, lakini kwa mshangao wa wengi, alijibu asingeweza kufika kwa vile alikuwa jijini Dar es Salaam.
"Kwa kweli sanaa ya maigizo visiwani kwetu haiwezi kwenda mbele kwani viongozi wetu majimboni wanaturudisha nyuma, wanatujua wakati wanapotaka kura tu lakini baada ya hapo hawana tena usuhuba nasi", alisema Mwenyekiti huyo.
Haidhuru alieleza kuwa, mbali na Mbunge huyo ambaye ni mfanyabiashara maarufu hapa nchini, pia waliwaalika viongozi mbalimbali wakiwemo Mbunge na Mwakilishi wa jimbo lao na lile jirani la Jang'ombe, lakini wote hawakufika.
Hata hivyo, sherehe za uzinduzi huo zilizojaza ukumbi, ziliokolewa na mwanahabari mwandamizi wa kituo cha ITV Maulid Hamad Maulid, aliyejikuta akivalishwa joho la kuwa mgeni rasmi mbadala.
Akizungumza katika hafla hiyo, Maulid alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na hazina kubwa ya wasanii wa fani mbalimbali, lakini wanashindwa kupiga hatua kutokana na kutopewa umuhimu na mamlaka zinazohusika ikiwa ni pamoja na viongozi wa majimbo kuwakimbia wasanii.
Aliwataka wasanii hao kutumia fursa ya kushiriki katika matamasha na kuingia mikataba na mahoteli ili kujitangaza, hali aliyosema itasaidia kuwainua kimaisha

MIEMBEZI DUMA HAKUNA MBABE.

Miembeni, Duma hakuna mbabe

Na Mwajuma Juma
TIMU za Miembeni na Duma, zimelazimika kumaliza dakika 90 kwa sare ya 0-0 katika pambano la ligi ndogo lililochezwa kwenye uwanja wa Mao Dzedong ,mwishoni mwa wiki.
Kwa matokeo hayo, Miemveni imepanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12, ikitanguliwa na Mafunzo inayoongoza lig hiyo kwa pointi 14 sawa na Jamhuri ikishika nafasi ya pili kwa tafauti ya magoli ya kufunga na kufungwa kati yake na askari hao wa wafungwa.
NAYE SULEIMAN BANGAYA, anaripoti kuwa timu kongwe ya soka Zanzibar, Kikwajuni, imeikong'ota Mlandege bila huruma kwa kuibugiza magoli 4-1 katika mchezo wa ligi daraja la kwanza Taifa.
Na katika mchezo mwengine wa ligi hiyo, timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Chwaka, zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka uwanjani kwa sare ya bao 1-1 kwenye uwanja wa Fuoni.
Nayo ligi daraja la pili Wilaya ya Mjini, mchezo uliochezwa uwanja wa Dimani, ulishuhudia watoa pasipoti Uhamiaji wakila sahani moja na Coast Stars kwa sare isiyokuwa na magoli, huku Mwembeshauri ikiichakachua Mwembeladu kwa kipigo cha 4-1.
Matokeo ya Central katika viwanja tafauti yanaonesha Amani Kids 3, Valencia 1, Arizona 8, Darajabovu 1, na Kwahani 4, Beach Boys 1.

Friday, 20 May 2011

WAWILI WASHIKILIWA KWA MAUAJI SINGIDA

Wawili washikiliwa kwa mauaji Singida

Na Jumbe Ismailly, Singida
JESHI la Polisi mkoani Singida linawashikilia watu wawili wa mji Mdogo wa Itigi, kwa tuhuma za kuharibu mali ya Benki ya NMB Tawi la Itigi na kumuua Juma Rashidi (32) mkazi wa Kijiji cha Tura, mkoani Tabora, aliyekuwa akituhumiwa kumuua dereva wa pikipiki (Bodaboda).
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Celina Kaluba aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo kuwa ni pamoja na Mohamed Masudi (24) na David Nicodemu (25), ambapo tukio hilo lilitokea Mei 15 mwaka huu huko Itigi.
Kaluba alisema dereva huyo wa pikipiki alikatwa na kitu chenye ncha kali kisogoni na abiria huyo Geu Njongaji na kisha kudondoka chini na hatimaye kuchinjwa shingo kama kuku.
Kamanda huyo alibainisha kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kufanikisha mauaji hayo, aliamua kupora pikipiki hiyo yenye namba za usajili T.962 BNF aina ya Sanlag na kuiendesha kwenda hadi kwao katika Kijiji cha Tura.
"Inaelekea wazi kwamba baada ya kuipora pikipiki hiyo ndipo Geu aliiendesha kwa mwendo wa kasi na hata hivyo hakuweza kufika mbali, akaligonga shina la mti mkubwa na hivyo kuumia vibaya sana",alifafanua Kaluba.
Kamanda Kaluba alisema kutokana na majeraha aliyopata, ndipo Geu alipoamua kurudi tena Itigi kwa ajili ya kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Gasper na ndipo wananchi waliokuwa wamepata taarifa ya kuuawa kwa dereva huyo wa bodaboda walimvamia na kuanza kumpa kipigo.
Alisema kamanda huyo kuwa hata hivyo licha ya uvamizi huo wa wananchi lakini inasemekana kwamba Geu aliweza kukimbilia katika Benki ya NMB Tawi la Itigi kwa lengo la kujisalimisha maisha yake, lakini kundi kubwa la wananchi wenye hasira
Kilimfuatilia nakufanikiwa kumtoa nje na kasha kumpiga kwa silaha mbalimbali na hivyo kusababisha kifo chake.
"Hata hivyo baada ya wananchi hao wenye hasira kukatazwa kuingia ndani ya majengo ya Benki na askari polisi waliokuwa lindo, ndipo waliamua kufanya fujo kubwa hadi kuharibu milango, madirisha, pamoja na vioo vya magari, hivyo
tunawashikilia Mohammed Masoud (24) na David Nicodemo (25) kuhusiana na mauaji na uhuribifu wa mali za Benki hiyo”, alisisitiza kamanda Kaluba.
Katika tukio jingine mkazi mmoja wa kijiji cha Ngimu, tarafa ya Mgori, katika halmashauri ya wilaya ya Singida, Raymond Erasto (26) aliwaua wazazi wake Erasto Kilakuno (78) na mama yake Frida Dule (57) kwa kuwakata kata kwa panga.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi wa Mkoa wa Singida, alisema mauaji hayo yamefanyika Mei 15 mwaka huu majira ya 1:45 jioni katika Kijiji cha Ngimu, tarafa ya Mgori na kwamba chanzo cha mauaji hayo inasadikiwa kwamba muuaji huyo alikuwa amerukwa na akili.
Aidha msemaji huyo wa jeshi la polisi alisema kuwa muda mfupi kabla kijana huyo kuwaua wazazi wake hao, alimjeruhi Ester Elihuruma (3) kwa kumkakata kwa panga sehemu mbali mbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali.
"Tayari tumeshamkamata mtuhumiwa huyo na bado tunakamilishe mambo machache yaliyobakia ili tuweze kumpeleka kwenye hospitali ya Mirembe, iliyoko Mkoani
Dodoma ili kwenda kuhakikiwa akili yake",alisisitiza kamanda Kaluba.

MACHAFUKO UARABUNI YAONGEZA MFUMKO WA BEI.

Machafuko Uarabuni yaongeza mfumko wa bei

Na Jumbe Ismailly, Iramba
KATIBU wa Uchumi na Fedha Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Lameck Nchemba Mwigulu amesema machafuko katika nchi za kiarabu yamechangia kupanda kwa gharama za maisha.
Mwigulu alisema hayo kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara aliyohutubia katika vijiji vya Makunda na Nkinto, wilayani hapa wakati wa ziara ya siku tano ya kuitambulisha sekretarieti mpya wa chama hicho.
Alisema machafuko yanayoambatana na maandamano katika baadhi ya nchi za kiarabu yamepandisha gharama za maisha huku kupanda kwa bei ya mafuta kukichangia mfumko wa bei na kupanda kwa gharama hizo.
Mwigulu ambaye ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi (CCM), alisema duniani kote maandamano huwa hayana faida zaidi ya kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.
Alisema maandamano yanayoongozwa kila kukicha na viongozi wakuu wa Chama cha CHADEMA, nayo yamekuwa yakichangia kwa namna moja au nyingine gharama za maisha kutokana na watu kutumia muda wao mwingi kwenye maandamano badala ya kujikita kwenye uzalishaji.
“Kiongozi wao anayewaongoza nilimuhurumia sikujua kwa nini anafanya hivyo, lakini nikagundua ni dokta, hata nyie mtadhani ni dokta wa kweli, kumbe ni dokta wa sheria za kanisa, hajui yanayoendelea hapa”, alisema Mweka hazina huyo.
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Oganaizesheni Asha Juma Juma, alisema sasa chama kimefuta utaratibu wa kuingiza wanachama wapya wa papo kwa papo kwa kuhofia vurugu zinazokuja kujitokeza mara tu baada ya kuwaingiza ndani ya chama.

WAHUDUMU WA AFYA WAKOSA MAKAAZI CHAKECHAKE

Wahudumu wa afya wakosa makaazi Chake Chake

Na Lulua Salum, Pemba
WAFANYAKAZI 21 walipelekwa katika hospitali ya Chake Chake wakitokea Unguja wamekosa makazi ya kudumu baada ya kuwasili kisiwani Pemba.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema tangu kuwasili kisiwani humo wamekuwa na tatizo la makaazi jambo ambalo ni kinyume na walivyoahidiwa.
Walifahamisha kabla ya kuwasili katika kituo hicho cha kazi waliahidiwa kupatiwa makaazi pamoja na huduma muhimu wanazopaswa kupewa.
Kutokana na hali hiyo wanalazimika kukaa chumba kimoja watu watano, ikizingatia hali ya mazingira si salama pamoja na nyumba hiyo kukosa huduma muhimu kama maji, umeme na choo jambo linalohatarisha afya zao.
“Tumeshanga kukuta haya tuliyoyakuta, baadhi ya hospitali za Pemba hazina nyumba za madaktari na sio kama hawalifahamu hili bali ni kuonesha kutowajali watendaji wake’’, walisema madaktari hao.
Walieleza kuwa imefikia hatua ya kuishi kwa wasamaria wema ambao wameguswa na tatizo la ukosefu wa nyumba za makaazi.
Walisema tangu wafike Pemba wameshahama mara nne ndani ya wiki moja hali inayowasababishia kupoteza mizigo yao sambamba na kuongezeka kwa gharama za matumizi hususan katika usafiri na chakula.
Walifahamisha kuwa licha ya kadhia hio na kukosa mapokezi mazuri kutoka wa wenyeji wao jambo linalowawia vigumu kufanya kazi zao, lakini bado wao wako tayari kufanya kazi na wamefurahi sana kupangiwa kazi Pemba.
Kwa upande wake Daktari dhamana wa hospitali ya Chake Chake, Sauda Kassim alikiri kupokea wahudumu hao wa afya na kusema hio ni faraja kwao kwani kilio cha muda mrefu cha kuwepo kwa uhaba kimepatiwa ufumbuzi.
Kuhusiana na suala kutopatiwa makaazi salama na ya kudumu kwa madaktari hao, alisema suala hilo wanalifanyia kazi na tayari wameshakaa na kamati ya wilaya kwa ajili ya utatuzi wa tatizo hilo.
Akizungumzia lawama waliyotupiwa ya kutowapokea vizuri na kutotoa mashirikiano ya karibu alisema wao wamewapa baraka zote na wapo nao bega kwa bega kuona kwamba hakuna tatizo wanalolipata wakiwa kazini na hata nje ya kazi.
Aliwataka wafanyakazi hao pamoja na matatizo waliyonayo wawe na subira kwani viongozi wao wako mbioni kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.

C-WEED YAIOMBA SERIKALI ILIPE UMUHIMU ZAO LA MWANI

C-weed yaiomba serikali ilipe umuhimu zao la mwani

Na Kauthar Abdalla
KAMPUNI ya ununuzi wa mwani ya C-weed Corporation imeiomba serikali kufahamu umuhimu wa zao hilo nchini pamoja gharama wanazozitumia wakati wa usafirishaji.
Akizungumza na mwandishi wa habari meneja wa mahusiano ya jamii wa kampuni hiyo Makame Salum Nassor alisema kampuni ili kuweza kusafirisha bidhaa hiyo haina budi kutumia gharama kubwa kiasi ambacho kinarejesha nyuma maendeleo ya kampuni hiyo .
Alisema meneja huyo kuwa kampuni imefikiria kuanzisha viwanda vingi vya kuusanifu mwani huo kwa kutengenezea vitu mbali mbali lakini hatua hiyo imekuwa ngumu kutokana na kutokuwa eneo la kutosha la kujenga kiwanda hicho pamoja na uhaba wa mali ghafi za kutengenezea vitu hivyo.
Alisema kwamba kiwango cha uzalishaji wa mwani huo kwa Unguja hakitoshelezi kuanzisha kiwanda inahitajika zaidi ya tani 10,000 kwa mwaka ili kuweza kumudu mahitaji hayo lakini kwa sasa ni tani elfu saba kwa mwaka ambazo wanazipata kutoka kwa wakulima wa zao hilo.
Hata hivyo meneja huyo alielezea juu ya malalamiko ya muda mrefu ya wakulima wa mwani kuwa bei ndogo wanayouzia lakini alisema kwa kuwa biashara ni huru basi kila mfanyabiashara anaangalia uwezo wa biashara yake ndipo aweze kutoa bei ya kununulia kwa wakulima hao.
Aidha alifahamisha kuwa bei ndogo inategemea na mnunuzi anaenunua kutoka katika kampuni hiyo ambapo zaidi ni kutoka katika nchi za nje ikiwemo Marekani, China na Ulaya.
Hivyo aliwaomba wananchi pamoja na wakulima kuondoa dhana ya kusema kwamba wanadhulumiwa katika biashara hiyo ila ni hali ngumu ya biashara wanayokumbana nayo kwa makampuni ya nje wanayoyauzia.
Pia meneja huyo ameitaka serikali kukaa vikao vya mara kwa mara na wamiliki wa makampuni yaliopo nchini ili kujadili mambo mbali mbali yanayohusu zao hili ikizingatiwa kuwa ni zao linaloingiza pato kubwa nchini kwa lengo la kuwaboresha wakulima wote na taifa kwa ujumla.

WAFANYAKAZI USTAWI WA JAMII WASISITIZA KUONGEZA TAALUMA

Wafanyakazi ustawi wa jamii wasisitiza kuongeza taaluma

Na Sharifa Maulid
MKURUGENZI Idara ya Mipango, Sera na Utafiti wa wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto Mhaza Gharib Juma, amewataka wafanyakazi wa Ustawi wa Jamii kufanyakazi kwa umakini na kwa kutumia taaluma zinazohusu kazi zao.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku nane kwa wafanyakazi 44 wa Idara ya Ustawi wa jamii wa Unguja na Pemba, yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar-e-salaam na chuo cha jamii cha Jane Addams cha Illinois Chicago nchini Marekani.
Alisema wakati umefika wa kuwepo mabadiliko katika utendaji wao na mabadiliko hayo yatafanyika endapo wafanyakazi hao watatumia taaluma zao katika kuihudumia jamii.
Mhaza alisema ipo tofauti ya wafanyakazi wenye elimu na wale wanaofanyakazi kwa kutumia uzoefu huku akisisitiza wenye elimu watumie taaluma zao katika utoaji wa huduma.
Alisema ni muhimu kwa wafanyakazi hao kujitahidi kuiboresha jamii kwa kufuata mila na desturi za Zanzibar ili kuweza kuwatunza watoto na wazee. “Napenda kuwahakikishieni wawezeshaji kuwa Elimu mtayoitoa itatumika kwa maslahi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar”, alisema.
Mkurugenzi huyo alilishukuru shirika la misaada la Marekani (USAID) kupitia asasi ya kimataifa American International Health Alliance (AIHA) kwa mchango wake ambao umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo waliwashukuru wawezeshaji kwa njia walizotumia ambazo zimeweza kufahamika kwa wote na kuwaomba kutembelea katika sehemu za kazi baadae ili kuona utendaji wao.
Wamesema taaluma waliyoipata ya kushughulikia masuala ya kesi za watoto na namna ya kutatua kesi za kiustawi itawafanya kutekeleza majukumu yao vyema.

Tuesday, 17 May 2011

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kuhusiana naMtambo wa kisasa wa kuzalisha madume bora  ya ngombe uliopo Maruhubi alipotembelea kituo hicho jana.Anaeeleza maelezo ni Mkuu wea Kituo hicho Dk. Khamis Ibrahim (Picha na Ramadhani Othman )    

DK. SHEIN:SERIKALI IMEANZA KUTEKELEZA AHADI ZAKE

Dk.Shein: Serikali imeanza kutekeleza ahadi zake

• Afungua kituo cha afya daraja la pili
Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali imeanza kutekeleza ahadi ya kuleta mabadiliko katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya vya daraja la pili, hatua itayoipunguzia mzigo hospitali ya Mnazimmoja.
Dk. Shein, alisema hayo jana baada ya kukifungua rasmi kituo cha Afya daraja la pili cha Mpendae, ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi, michango ya wahisani na viongozi wa Jimbo hilo.
Dk. Shein, alisema kufunguliwa kwa kituo ni ahadi ya serikali iliyoitoa wakati wa kampeni za kuleta mabadiliko katika sekta ya afya pamoja na kuipunguzia mzigo hosptali ya Mnazimmoja kwani iko katika hatua za kuwa ni hospitali ya Rufaa.
Alisema serikali itahakikisha inazitekeleza ahadi zake zote ilizozitoa na kuhakikisha mikoa yote Unguja na Pemba inakuwa na hospitali za daraja la pili ambapo tayari kwa mjini hospitali hizo katika Jimbo la Kwamtipura na Mpendae.
"Mtakumbuka katika kiwanja cha Garagara nilisema nitaviendeleza vituo vya afya vya Mpendae na Kwamtipura ambapo tutavijenga kwa kuvifanya kuwa ni vya daraja la pili, lengo ni kupunguza msongamano katika hospitali kuu ya Mnazimmoja”, alisema Dk. Shein.
Dk. Shein, aliwataka viongozi wa wizara pamoja na Jimbo hilo kuona wanatafuta njia zaidi zitazowawezesha kufanikisha ujenzi wa hospitali hiyo kwa awamu ya pili, huku pia akitoa wito kwa watendaji wa sekta hiyo kubadilika.
Mapema baadhi ya viongozi wa Jimbo hilo wakitoa maoni yao katika risala, walisema wanakusudia kuendeleza ujenzi huo kwa awamu ya pili baada ya ile ya kwanza kukamilika ambapo tayari huduma zimeanza kupatikana kituoni hapo.
Alisema ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuwa wa ghorofa mbili ambapo utagharimu shilingi milioni 400, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi 152 zimetumika.
Wananchi hao waliiomba serikali kuwafikiria kuwapatia ajira walinzi wanaolinda kituo hicho na kuwaimarishia mfumo wa maji safi na pia kuishinikiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kumalizia ujenzi wa Skuli ya Sekondari katika Jimbo hilo.
Katika hatua nyengine Dk. Shein alitembelea kituo cha mtambo wa kuzalishia mbegu bora za madume ya Ng’ombe huko Maruhubi, na kuutaka uongozi wa wizara ya Mifugo na Uvuvi walidhibiti eneo la kituo hicho ili kuepuka uvamizi.
Dk. Shein, alisema nia ya serikali hivi sasa ni kuona sekta ya ufugaji inaimarika baada ya kuonekana huduma nyingi kufifia na kwamba serikali itaimarisha sekta hiyo.
Alisema maendeleo ya ufugaji ni moja ya mambo ya msingi ambayo serikali imedhamiria kuyakuza na kuwapo kwa mtambo unaotumika kuzalishia mbegu za ufugaji ni hatua itayokuza maendeleo kwa sekta hiyo.
Naye Mkuu wa kitengo hicho, Dk. Khamis Ibrahim, akitoa maelezo juu ya mtambo huo alisema tayari hivi sasa imeweza kuwapandishia ng’ombe 1,776 ambapo kwa upande wa Pemba ni 1,046 na Unguja ni 721 kwa mwaka.
Aidha, mtaalamu mwengine wa wizara hiyo Hafidh Said, alisema nia ya wizara hiyo kuona hivi sasa wanapunguza uagizaji wa ng’ombe wa kupandishia kutoka Arusha, kutokana na hivi sasa kuwepo kwa ng’ombe wawili wanaofanya kazi ya kutoa mbegu.
Akifanya uzinduzi wa kituo cha skuli cha Meya Dk. Shein, aliwataka wananchi kuona wanaendeleza kutoa michango yao katika kukuza sekta hiyo ya elimu kwani nia ya serikali kuona maendeleo ya elimu yanakuwa.
Alisema serikali ya awamu ya saba italiendeleza hilo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo uamuzi wa Rais wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, aliyeahidi kutoa elimu bila ya malipo kwa Wazanzibari wote.
Dk. Shein kwa kufanikisha maendeleo ya mradi huo ameahidi kutoa shilingi milioni 7,000,000 ikiwa ni mchango wake kwa ajili ya ujenzi huo ambapo hapo awali mratibu wa skuli hiyo Sichana Talib alisema bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za kukamilisha mradi huo ikiwemo ujenzi wa kiwanja ambapo hadi sasa tayari wameshatumia milioni 30.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za Mkoa wa Mjini Magharib ambapo ilieleza kuwa serikali ya mkoa imeweza kufanikisha miradi mbali mbali ya maendeleo huku kukiwa na changamoto mbali mbali za kuimarisha Mkoa ambapo aliwataka viongozi wa Mkoa kuendeleza jitihada hizo.
Aidha, Dk. Shein, alifanya ukaguzi katika kiwanja cha Mnazimmoja na kuutaka uongozi wa Baraza la Manispaa, kuliangalia suala la michirizi katika kiwanja hicho ikiwa ni hatua ya kukabiliana na tatizo la kujaa maji kwa wakati wote.
Kaimu Mkurugenzi wa Baraza hilo Mzee Khamis, alisema maji yanayokaa katika eneo hilo hivi sasa tayari baraza lake inalifikiria kulifanyia kazi baada ya kuonekana athari zake kuongezeka ikiwa ni hatua watayoifikiria kwenda sambamba na mradi wa mitaro wa maeneo ya Ng’ambu ambao utaanza karibuni.
Dk. Shein, ataendelea tena leo kufanya ziara yake hiyo, kwa kutembelea wilaya ya Magharibi, kwenye kituo cha utafiti wa kilimo Kizimbani, Ufunguzi wa nyumba ya daktari Kizimbani, Uwekaji wa Jiwe la Msingi la kituo cha Afya Mtoni na kukagua Kilimo cha Mpunga wa Kumwagilia maji.
Sehemu nyengine ambazo atarajiwa kuzitembelea ni ya Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya magharibi, Ufunguzi wa nyumba ya daktari Kombeni, kukagua uwanja wa timu ya Bweleo na uwekaji wa jiwe la msingi Skuli ya Maandalizi ya Bweleo.
Mikutano ya hadhara ambayo ilipangwa kufanyika katika ziara hizo Idara ya Habari Maelezo, imeeleza kuwa imefutwa.

OMANAIR YAAZA SAFARI MOJA KWA MOJA ZANZIBAR

‘Oman Air’ yaanza safari za moja kwa moja Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi
SAFARI za anga kutoka Oman hadi Zanzibar zimeanza ramsi jana baada ya ndege ya shirika la Oman ‘Oman Air’ kutua katika uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wa Zanzibar.
Hayo yamebainika katika hafla ya uzinduzi wa ndege ya ‘Oman Air’, iliyofanyika katika hoteli ya Serena Inn iliyopo Shangani mjini hapa.
Ndege ya kwanza iliwasili Zanzibar jana asubuhi, ambapo iliteremsha abiria 65 na kupakia abiria 40, ikielekea na safari yake ya Oman kwa kupitia Dar es Salaam.
Sherehe maalum ilifanyika kiwanjani hapo kwa ngoma za asili na viongozi mbali mbali kuhudhuria akiwemo Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud.
Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar, Majid Alabadi alisema Oman imeamua kurejesha ndege hiyo kutokana na hali ya uwanja wa ndege wa Zanzibar kuimarishwa vizuri pamoja na kuwepo kwa usalama wa uhakika.
Alieleza uwanja wa Abeid Amani Karume umefanyiwa matengenezo makubwa na umeimarishwa kwenye utoaji wa huduma pamoja na suala zima la usalama.
Balozi Alabadi alifahamisha kuwa nchi ya Oman inajivunia mahusiano ya kidugu na kimawasiliano ya muda mrefu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Wazanzibari.
Alisema shirika hilo kurejesha huduma zake moja kwa moja hapa Zanzibar litasaidia kukuza biashara ya utalii.
Nae Katibu Mkuu wa Miundombinu na Mawasiliano, Dk. Vuai Lila alisema uwanja huo umeimarishwa kwa kufanyiwa matengenezo na kuzidishwa njia ya kurukia ndege, ili ndege kubwa na ndogo zituwe bila ya wasiwasi.
Aliongeza kusema kwamba, ujenzi wa ukuta (uzio), unaendelea ili kuweka usalama na ulinzi wakati wa ndege zinapotua na kuruka, sambamba na ujenzi wa jengo la abiria la kisasa, ambapo litakamilika baada ya mwaka mmoja na nusu.
Shirika la ‘Oman Air’ litafanya usafiri wa moja kwa moja kutoka Oman hadi Zanzibar mara tatu kwa kwa siku za Jumatatu, Jumanne na Jumamosi, ambapo ndege itakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 156.

MKUTANO WA KIMATAIFA UJASIRIAMALI KUKUZA MAENDELEO

Mkutano kimataifa ujasiriamali kukuza maendeleo

Na Mwanajuma Abdi
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mwanamwema Shein amesema mkutano wa kimataifa wa kujadili harakati na shughuli za wanawake utasaidia kukuza maendeleo ya akinamama na uchumi wa nchi.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa siku moja wa kimataifa wanawake ulioandaliwa na Jumuiya ya ZAYEDESA, chini ya Mwenyekiti wake, Mama Shadya Karume ambao umewakutanisha wanawake wa Zanzibar, Jamhuri ya Czech na Jamhuri ya Slovak.
Mkutano huo wa siku moja wa wafanyabishara wadogo wadogo, wanawake, NGOs na utalii ulifanyika katika hoteli ya Waridi Beach Resort, Pwani Mchangani.
Alisema majadiliano yatakayofanyika katika mkutano huo yatasaidia kuleta maendeleo kwa wanawake kwa kupata taaluma, huku pia akitumia fursa hiyo kuelezea wanawake wa Zanzibar jinsi wanavyojiimarisha katika kuondokana na umasikini.
Mama Shein alisema maendeleo na hatua walizopiga wanawake wa Zanzibar yanatokana na kuimarika kwa amani na utulivu, huku akiwashajiisha wageni hao kutembelea sehemu mbali mbali za kihistoria ikiwemo Mji Mkongwe, ambako watajionea kazi zinazofanywa na akinamama.
Alizipongeza juhudi za ZAYEDESA kwa kuwezesha mkutano huo kufanyika Zanzibar, ambapo utasaidia kuwanyanyua kielimu wafabiashara wadogo na kuwaongezea ufanisi katika shughuli za kijasiriamali.
Nae Mwenyekiti wa ZAYEDESA, Mama Shadya Karume akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, alisema wanawake wajasiriamali wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto mbali mbali zinazokwamisha juhudi zao za kimaendeleo ikiwemo ukosefu wa elimu ya biashara, hali inayosababisha kutokuwa wabunifu.
Alisema changamoto nyengine ni suala zima la kutokuwa na soko la uhakika la kuuza bidhaa zao wanazozalisha, huku pia kukiwa tabia potofu kuwa suala la ujasiriamali ni la wanaume na si la wanawake.
Shadya alisema pia wajasiriamali wa Zanzibar wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la mitaji midogo pamoja na uwezo wa kutimia teknolojia za kisasa katika kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Alieleza wanawake wengi wamejiajiri katika shughuli mbali mbali kwa ajili ya kujiletea maendeleo ya na nchi kwa ujumla licha kuzongwa na majukumu ya kuhudumia familia zao.
Shadya Karume alisema baadhi ya shughuli wanazojishughulisha ni pamoja na uuzaji wa bidhaa mbali mbali za kazi za mikono, ukulima, uuzaji wa vyakula na kufanya kazi za elimu na afya.
Hata hivyo aliwashukuru Jamhuri za Czech na Slovak kwa kukubali kuja kuungana na wananchi wa Zanzibar kwa kuikubalia Jumuiya ya ZAYEDESA kwa kuzidisha mashirikiano yao katika kuhudhuria mkutano huo.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Czech, Alena Gajduskova alisema wanawake wa huko wamepiga hatua kubwa kutokana kupatiwa taaluma za shughuli za kibiashara pamoja na kuwepo progamu maalum za wanawake katika kuwanyanyua kiuchumi.
Naye Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman alisema wanawake wa Zanzibar wamepata muamko katika shughuli za kujiletea maendeleo yao na kuondokana na umasikini.
Alisema juhudi za serikali ni kuwajenga kitaalum ili waweze kuifanya miradi yao na vikundi iwe endelevu.

TAFITI ZITUMIKE SIO KUBAKI MAKABATINI

Tafiti zitumike sio kubakia makabatini
Na Ramadhan Makame
MKUU wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) kilichopo Chwaka, Kamal Kombo Bakari, amesema Zanzibar itapiga hatua kubwa za kimaendeleo endapo tafiti zitatumika kikamilifu badala ya kuishia katika makabati ya ofisini.
Kamal alieleza hayo hoteli ya Visitors Inn, iliyopo Jambiani baada ya ufunguzi wa semina kuwafundisha njia za kisasa za ufanyaji utafiti walimu wa Vyuo vya Elimu ya Juu vya Zanzibar.
Alisema utafiti wowote unaofanywa, ni lazima ulenge kusaidia matatizo ya wananchi na hakutakuwa na maana ya kuendeleza kufanywa kwa tafiti kama zitaendelea kuishia kwenye makabati ya ofisini.
“Tafiti zinazofanywa zisaidie maendeleo ya nchi na uondoke utamaduni wa kuishia katika makabati ya maofisini”, alisema Mkuu huyo.
Mkuu huyo alisema kufanyika kwa mafunzo hayo kutasaidia kuamsha ari ya ufanyaji tafiti katika vyuo vya Zanzibar ambayo vimekuwa vikijikita zaidi kutoa taaluma kuliko ufanyaji wa utafiti.
Bakari alisema mataifa ya nje hasa Ulaya yamepiga hatua za kimaendeleo kutokana na matumizi ya tafiti za vyuo vikuu.
Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Karna Soro, alisema tafiti ni nyenzo na muhimili muhimu katika kuharakisha maendeleo ya nchi.
Mratibu huyo alisema utafiti husaidia kutoa maamuzi sahihi ya kimaendeleo na kisiasa sambamba na kuonesha hali halisi ya tatizo lililopo katika muda uliopo na njia bora za kukabiliana na matatizo hayo.
“Matatizo ya kimaendeleo yanayoikabili nchi kwenye uchumi na siasa yataondoka endapo watoa maamuzi watajikita katika kuyafumbua matatizo hayo wakitumia tafiti zilizofanywa”, alisema Soro.
Alifahamisha kuwa mara nyingi wanasiasa wamekuwa wakikwepa kuzitumia tafiti kama njia ya kujikinga kutokana na dhana kuwa zimekuwa zikiwakosoa, jambo ambalo alisema limepitwa na wakati.
Mafunzo hayo ya siku tano yanayoendeshwa na Chuo cha Usimamizi wa Fedha Zanzibar (ZIFA), yanawashirikisha wahadhiri kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vya Zanzibar.

POLISI WATATU MAHAKAMANI KWA KUOMBA RUSHWA

Polisi watatu mahakamani kwa kuomba rushwa

Na Jumbe Ismailly,Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Singida, imewapandisha kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Manyoni askari polisi watatu wa kituo mji mdogo wa Itigi, wilayani kwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni mbili.
Waliofikishwa katika mahakama hiyo ni pamoja na Joseph Raphael Nkurlah, Nasibu Thabiti Njovu na Noeli Madimo Philimon ambao hata hivyo nyadhifa pamoja na umri wa kila mmoja wao hazikuweza kupatikana mara moja.
Kwa mujibu wa mwanasheria wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Singida, Antidius Rutayuga, askari polisi hao wamefunguliwa kesi namba 81/2011 Machi 29, mwaka huu katika mahakama hiyo.
Aidha Mwanasheria huyo alisema mashitaka ya askari hao yapo chini ya vitendo vya rushwa k/f cha 15 (1)(a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa nambari 11/2007.
Rutayuga alisema kwamba, Januari 23 mwaka huu washitakiwa kwa pamoja wakiwa katika kijiji cha Kazikazi, tarafa ya Itigi wilayani humo waliomba na kushawishi wapewa rushwa na mzee Samson Ntungwa (68) shilingi milioni mbili ili wasimfungulie kesi ya kumficha muhalifu wa kesi ya mauaji aliyetambulika kwa jina la Mussa Bakari.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwanasheria huyo siku ya tukio Januari 25, mwaka huu katika muda usiofahamika wakiwa kwenye kituo chao cha kazi washitakiwa hao kwa pamoja
walipokea rushwa ya shilingi milioni mbili tasilimu kutoka kwa mzee Samsoni.
Rutayuga kwamba washtakiwa hao kila mmoja kwa wakati wake walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana hadi Mei 19,mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

WAUMINI WAGHADHIBISHWA NA PADRI KUMCHAPA MAKOFI MUUMINII

Waumini waghadhibishwa Padri kumchapa makofi muumini

Na Kunze Mswanyama, Kigoma
WAUMINI wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Gungu Mkoani Kigoma, wamekilaani kitendo cha aibu cha Padri Sabasi kumtandika makofi kanisani muumini wake.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, waumini hao walisema kitendo kilichofanywa na Padri huyo ni cha aibu na kinapaswa kulaaniwa.
“Kutokana na uzee wake mama yetu aliyepigwa makofi kweli kitendo hicho kimetushusha mori kwenda kuabudu kanisani hapo, viongozi wa dini wanaongozwa na roho wa upole sijui huyu anaongozwa na roho gani hiyo", alisema mmoja wa waumini hao, John Xveri.
Mama aliyepigwa makofi na Padri inasemakana ana umri wa miaka 76 na alipigwa baada ya kupokea mkate wa sakramenti na kisha kukaa kwenye kiti badala ya kusimama ili kusubiri kuutumia pamoja na wenzake,jambo lililomkera padri huyo hivyo kumchapa vibao ajuza huyo.
Kwa ukali kabisa kabla ya kushusha kipigo, alisema “Kwa nini unakula sakramenti hali umekaa chini, hujui kama ni dhambi?” alisema Padri huyo.
Xveri alisema wakati Pdri huyo kutoa ukali huo walidhani ni sehemu ya kupata upole wa Yesu na pia huruma zake, lakini wanakutana na yale yale ya duniani ambayo kamwe hayaelezeki.
Alipoulizwa juu ya kitendo hicho cha kumpiga kondoo wake, Padri Sabasi alisema kuwa kwa taratibu za kanisa lao hutakiwa kusimama kwenye foleni ukiwa na mkate huo hadi pale utakapoamriwa kuitumia.
Alisema mama huyo alichukua mkate huo mtakatifu na kuuweka kwenye maziwa yake kisha kukaa mimi nikajua anataka kuufanyia mambo ya kishirikina.
Kutokana na hali hiyo waumini wapatao 2,000 wamedhamiria kutokwenda kusali kanisani hapo wanatakiwa wauone upendo wa Mungu na badala yake wanakutana na kadhia za ajabu kama hiyo ambayo hadi sasa Baraza la wazee wa Kanisa hilo wanakutana ili kuchukua hatua dhidi ya Padri huyo.

SEKTA BINAFSI ITEKELEZE MKAKATI WA UKIMWI

Sekta binafsi itekeleze mkakati wa UKIMWI

Na Nafisa Madai, Maelezo
SEKTA binafsi zimetakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kupambana na UKIMWI kwa kuanzisha mipango maalum ya kukabiliana na gonjwa hilo katika sehemu za kazi.
Akifungua semina ya siku moja Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Islam Seif aliwataka viongozi wa sekta binafsi kutimiza wajibu wao kwa kuwasaidia wenye kuishi na VVU na watoto wenye kuishi kwenye mazingira magumu.
Islam aliyefungua semina hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais alizitaka asasi hizo kuacha kunyanyapaa na ubaguzi kwa watu wenye UKIMWI kwani kufanya hivyo ni kinyume na katiba ya Zanzibar ambayo inakataza ubaguzi.
Alisema mkakati wa taifa uliopo ukifuatwa utasaidia kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya UKIMWI katika sehemu za kazi jambo ambalo litaiweka salama nguvu kazi ya taifa hili.
Alisema vijana ndio waathirika wakubwa wa gonjwa hili hali inayohatarisha kuzorota uchumi nchi kutokana na kupoteza nguvu kazi tegemezi ya taifa na kupoteza vipato vya watu kwa kugharamia huduma za tiba.
Islam alisema licha kuwa Zanzibar takwimu za UKIMWI ni 0.6 ikilinganishwa na nchi nyengine lakini ipo haja kupunguza idadi hiyo kutokana na idadi hiyo iliyopo kutokana udogo wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Naibu huyo alifahamisha kuwa ipo haja ya kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa maeneo ya sekta binafsi kwa kushirikiana na jumuia ya wafanyabiashara ya ABCZ.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC), alisema jamii iyashughulikie makundi maalum ambayo yako kwenye uwezekano wa kuambikizwa ikiwemo watumiaji wa dawa za kulevya, madada poa pamoja na wanaume wanaojishughulisha na vitendo vya ushoga.
Wakichangia katika semina hiyo washirikia hao walipendekeza yapo mabadiliko ya mila na desturi ndiko kunakochangia kasi ya maambikizi na kutaka sheria za uwekezaji zifuatwe.
Mkutano huo ambao una azma ya kuweka muelekeo mpya wa kimtizamo na kifikra na na misingi ya kuimarisha muitikio wa sekta binafsi katika mapambano ya UKIMWI Zanzibar imewahusisha wadau mbali mbali wa sekta binafsi wa Unguja na Pemba.

KOROSHO YAPELEKA NEEMA MKURANGA

Korosho yapeleka neema Mkuranga

Na Shan Hussein, Mkuranga
HALMASHAURI ya wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani, imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 11 katika msimu wa mwaka jana wa zao la korosho.
Mkuu wa wilaya hiyo, Henry Clence, alitoa taarifa hiyo katika Kikao cha Madiwani, kilichokuwa kikijadili maendeleo ya halmashauri hiyo, na kutoa taarifa juu ya fedha zilizopatikana katika zao hilo.
"Miaka ya nyuma tulikuwa tukipata mapato kidogo katika zao hili, baada ya serikali kuweka mfumo wa sitakabadhi ghalani, zoezi hili linakwenda vizuri na kusababisha wilaya kupata fedha nyingi na wakulima kunufaika na zao hilo,''alisema.
Mkuu huyo alisema miaka ya nyuma kilo moja ya korosho, ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi 150, lakini baada ya mfumo kuanza wa stakabadhi ghalani kilo moja ya korosho imeuzwa mpaka shilingi 1,800.
Alisema kupatikana kwa fedha nyingi kumesaidia kupatiwa pembejeo ya ruzuku nyingi ambayo thamani yake ni shilingi milioni 43, hivyo itawasaidia wakulima katika kuongeza uzalishaji wa korosho, ikiwamo na kupulizia mashamba yao kwa wakati.
Clemence aliwataka madiwani kuwahamasisha wakulima kupalilia mikorosho yao kutokana na hivi sasa kuwa na korosho nyingi, pamoja na kupulizia dawa.
"Mpande na miembe ya miaka michache ipo mingi tu, pale mnapo vuna korosho zenu msikae bure na baadaye anaanza tena kunufaika na zao la miembe,''alisema, mkuu huyo.
Aliongeza kuwa, mikorosho sasa hivi imekuwa na soko kubwa Kutokana na kusimamiwa kikamilifu, pia alisema taarifa kutoka soko la juu inasema kuwa korosho za Mkuranga ni tamu kuliko korosho za maeneo mengine.

Saturday, 14 May 2011

ATAEPATA UONGOZI CCM KWA RUSHWA KUEGULIWA - BALOZI SEIF

Ataepata uongozi CCM kwa rushwa kuenguliwa – Balozi Seif

• Asema uvuaji gamba umeletwa na tuhuma za ufisadi
Na Abdulla Ali, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi amesema nia ya Chama hicho ya kujisafisha ilitokana na tuhuma mbali mbali za wananchi juu ya ufisadi wa baadhi ya viongozi wake na kupelekea kupata ushindi mdogo katika uchaguzi uliopita.
Balozi Seif alieleza hayo alipozungumza na viongozi wa CCM kisiwani Pemba, akiwa katika ziara ya siku mbili ya kikazi.
Kwa hivyo alisema CCM imejivua gamba kwa kupanga safu mpya ya uongozi na watendaji wake pamoja na kuachana na njia zote zinazopelekea kushawishi rushwa wakati wa kutafuta viongozi.
Hivyo aliwataka viongozi kuwa makini katika chaguzi mbali mbali na kuwachaguwa viongozi kutokana na uwezo wao, sifa za utendaji na za kielimu ukiwemo uadilifu na kuwaepuka wanaotumia fedha au pochi kujipatia madaraka.
“Kamati ya maadili kamwe haitaridhia mtu yeyote kujipatia uongozi kwa rushwa na ata bainika watamuenguwa pasi na muhali,” alisema Balozi Iddi.
Wakati huo huo Balozi Seif amewataka wafanyakazi wa ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kufanya kazi kwa bidii kufanikisha kazi za Mtendaji Mkuu wa Serikali.
Hayo yalieleza katika mkutano wake na wafanyakazi wa Ofisi yake ya Pemba uliofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba.
Alisema akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar anataka wafanyakazi wa Wizara yake wawe ni mfano wa utendaji bora.
Aliwataka wajitahidi kuimarisha umoja, upendo miongoni mwao na kuachana na majungu na fitina kwa lengo la kurahisisha utendaji wao.
Balozi Iddi alieleza kuridhishwa kwake na utendaji mzuri wa Ofisa Mdhamini wa Wizara hiyo, Amrani Massoud kwa usimamizi wake mzuri uliopelekea kuwa na ufanisi bora katika ofisi ya Pemba bila ya matatizo.
Aidha, aliahidi kuwapatia mafunzo kwa awamu wafanyakazi wa Ofisi hiyo na kurekebisha masuala mengine kadri bajeti itakavyoruhusu.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Meja mstaafu, Juma Kassim Tindwa aliupongeza utendaji wa Ofisi hiyo na kusema umekuwa wa mfano na kuzitaka ofisi nyengine kisiwani humo kuiga.
Kabla ya hapo Balozi Seif, alikutana na wafanyakazi wapya wa Wizara ya Afya waliopelekwa Pemba kuanza kazi, ambapo aliwapongeza kwa kuonesha uzalendo wao na kukubali kutimiza wajibu wao kufanya kazi popote nchini.
Alisema Zanzibar ni Pemba na Unguja, hivyo waajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya kazi Pemba ni wajibu na sio adhabu kama inavyotafsiriwa na baadhi yao.
Nae Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya alionya juu ya wafanyakazi wataorejea Unguja bila ya ruhusa kuwa hawatopata fursa ya kuajiriwa tena.
Halikadhalika, alieleza umuhimu wa ajira kwao kwani alisema hata hiyo ajira yao imetokana na jitihada kubwa za Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Iddi ya kuomba wapatiwe fursa hiyo mbali ya kuwepo hali ngumu ya kifedha.

VUAI AHIMIZA UWAJIBIKAJI CCM ZANZIBAR

Vuai ahimiza uwajibikaji CCM Zanzibar

Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai amewataka watendaji wa Chama hicho kutekeleza kwa vitendo maagizo ya halmashauri kuu ya taifa.
Vuai alieleza hayo jana ofisi kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa alipokutana na makatibu wa CCM wa mikoa, wilaya pamoja na maofisa wa chama wa ofisi kuu ya CCM Zanzibar.
Alisema ili chama kiimarike ni lazima washuke kwenye ngazi za chini katika ngazi ya shina, maskani na matawi ambako ndiko kwenye wanachama wengi wa chama hicho.
Alisema ili chama kisonge mbele katika kutekeleza majukumu yake ni lazima watendaji wa chama hicho wahakikishe wanafanya vikao kwa mujibu wa katiba.
Aidha Naibu huyo alisisitiza haja kwa viongozi hao kuhakikisha wanaandaa mikakati itakayosaidia kuanzisha miradi itakayokiwezesha chama kuongeza mapato ili kukimu gharama za uendeshaji.
Naibu huyo alitumia fursa ya mkutano huo kuwakumbusha viongozi hao kuwahimiza wanachama kulipa ada za uanachama na kuwa na moyo wa kutoa michango ya hiyari.
Alisema suala la maelewano na ushirikiano katika miongoni mwa watendaji nalo lina umuhimu wake na kusisitiza suala hilo kuendelezwa na kuepuka mifarakano.
Vuai alitoa wito kwa watendaji wa CCM wahakikishe wanafikia malengo ya kazi za kisiasa na kiuchumi mbele ya kamati za siasa.

WAWEKEZA WA KIGENI WANYANYASA WABIA WAZALENDO

Wawekezaji wa kigeni wanyanyasa wabia wazalendo

Na Mwantanga Ame
BAADHI ya watendaji serikalini wamedaiwa kuchukua mabilioni ya fedha, kwa kushirikiana na wawekezaji wasio waaminifu na kuwakandamiza wawekezaji wazalendo kuuwa sekta ya utalii.
Hayo yamejitokeza mbele ya Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi, ilipofanya mazungumzo na baadhi ya wamiliki wa mahoteli ya kitalii huko Marumbi wilaya ya kati Unguja.
Watendaji wa ngazi za juu serikalini hasa sehemu ya mapato wamelalamikiwa na wawekezaji wazalendo wamekuwa wakishirikiana na wawekezaji wa nje na huchukua mabilioni ya fedha kupitia sekta hiyo ya utalii na kuwakandamiza kwa vitisho wazalendo.
Mmoja wa wamiliki hoteli ya kitalii, Ali Mgeni, alisema hali hiyo imejitokeza baada ya kufuatwa na watendaji hao kutakiwa kutohoji juu ya mmoja wa wamiliki aliyeingia naye mkataba kumbaini kwenda kinyume na makubaliano waliyofungiana mkataba wake.
Alisema Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi (ZIPA), imemruhusu Mwekezaji huyo kuzimiliki hoteli tisa zilizomo katika ukanda wa kati na Kaskazini, na huku akiwa hana faida yoyote anayoingiza katika serikali kutokana na kuendeleza utalii kwa njia ya pekeji ambapo watalii hulipia kila kitu nchini kwao.
Alisema alichokibaini Mwekezaji huyo amekuwa akipata nguvu ya kufanya hivyo kutokana na kushirikiana na baadhi ya maafisa wa kodi hapa nchini kwani baadhi yao kumfuata na kumtaka asiliingilie suala hilo.
Alisema kinachomuuma kuona Muwekezaji huyo bado serikali inamfungisha mikataba ya kumiliki hoteli nyengine, wakati wakijua kuwa mikataba yake haina faida na serikali kutokana na watalii anaoleta sio wanakuja kutumia kwa vile tayari wameshalipia kila kitu nchini Italia.
Alisema hali hiyo humfanya alieingia nae ubia kutofaidika kwani hutegemea zaidi kupata fedha za wageni ambao hutumia ziada ya kile walicholipia nchini kwao ambapo kwa mwezi huweza kupata shilingi 200,000.
“Ingawa wageni hao wanakuja katika hoteli na hujazana kwa msimu lakini huwa hawatumii na kama watatumia hawazidi zaidi ya shilingi 200,000 kwa mwezi kwani ile chai yao basi imeshalipiwa nchini Italia sie kazi yetu kumuwekea mgeni anywe” alisema Muwekezaji huyo.
Alisema hapo awali yeye aliingia ubia na Muwekezaji huyo kwa kutomudu gharama za ujenzi kwa kutumia kiwanja chake kwa kushirikiana na kaka yake, lakini kaka yake huyo anaeishi Italia hivi sasa anashindwa kumfahamu kwa vile hapati shauri jema kutokana yeye ndie aliehusika kumleta mwekezaji huo.
Alisema cha kushangaza mmiliki huyo, hivi sasa amebadilisha hata makubaliano ya mwanzo ambapo alitakiwa kuilipa familia hiyo asilimia 25 lakini amebadili mkataba wake na kumueleza hivi sasa asilimia anayotakiwa kuipata ni 15 lakini hata hivyo hivi sasa hawaipati na anapojaribu kumuuliza kaka yake humwambia atalipiwa na Mungu.
Mmiliki huyo alisema Hoteli ambazo Mwekezaji huyo amezichukua ni zile ambazo zilianzishwa kwa mfumo wa Uwekezaji wa pakeji na wawekezaji wake kushindwa kuziendesha ambapo yeye huzinunua kwa Wawekezaji wenzake nchini kwao na kukubaliwa kuwekeza kama mmiliki halali kutoka kwa wenzake hao.
Akiendelea alisema hali hiyo imekuwa ikimfanya kukabiliwa na madeni mengi ya wasambazaji wa huduma katika hoteli hiyo ambapo zimefikia zaidi ya shilingi milioni 41 na baada ya kumtumia taarifa za madeni Mbia mwenzake amemleta shilingi milioni 23 huku kukiwa na bakaa ya madeni.
Kuhusu malipo ya wafanyakazi nayo alisema hivi sasa kutokana na msimu kuwa mdogo amekubaliana na baadhi ya wafanyakazi kupumzika hadi msimu utapoanza, lakini kwa waliobakia bado ameshindwa kuwalipa mshahara wao wa mwezi uliopita.
Kuhusu malipo ya kodi za serikali alisema hizo hazina mashaka kutokana na Muwekezaji huyo amekuwa akijitahidi kulipia kodi zote anazotakiwa kuzilipa serikalini.
Mwekezaji huyo alisema hivi sasa anajitayarisha kutafuta mwanasheria ikiwa ni hatua ya kuanza maandalizi ya kumfikisha mbia mwezake Mahakamani kwa kushindwa kumpatia sehemu ya asilimia aliyotakiwa kuipata kulingana na mkataba waliokubaliana.
Hapo awali alisema katika makubaliano yao walikubaliana fedha za majengo wajilipe ndani ya kipindi cha miaka minne lakini cha kushangaza imefikia miaka sita hawajaanza kupata asilimia yao ya miaka miwili na badala yake ameletewa mkataba mwengine unaopunguza asilimia zake.
Mkurugezi Mipango katika Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ashura Haji Mrisho, alisema matatizo ya aina hiyo yapo mengi kutokana na baadhi ya wananchi kuamua kushirikiana na wawekezaji kwa kuwapa ardhi ili wajenge bila ya kupitisha miradi yao ZIPA.
Alisema Wananchi wa maeneo ya ukanda wa bahari huingia mikataba kwa kushea ili wajengewe kwa njia ya kuendesha hoteli hizo jambo ambalo huwasababishia matatizo baadae kutokana na baadhi ya wanaoshirikiana kutokuwa waaminifu na hukatisha mikataba ya Wazalendo ama huwafikisha mahakamani pale wanapoonesha nia ya kutaka kujitoa katika miradi walioanzisha.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Asha Bakari Makame, alisema ipo haja kwa watendaji wa Wizara hiyo kuyaona matatizo ya aina hiyo kwani serikali imekuwa inakosa mapato mengi huku watu wachache wakifaidika na miradi ya aina hiyo.
Alisema, utalii wa aina hiyo, hivi sasa unaonekana haufai na haelewi kwanini ZIPA na Idara nyengine zinazosimamia sekta hiyo kuendelea kuwafungisha mikataba wawekezaji wanaotaka kuendesha utalii kwa mbinu ya pakeji.
Mwenyekiti huyo aliwataka viongozi wa Wizara hiyo kukaa pamoja na ZIPA, ZRB, na wadau wengine kulizungumzia suala hilo na kuliandalia mkakakati maalum huku wakitaka kufanyika uchunguzi kuona wadau hao kama hawana mkono wao wa kuifilisi serikali kwa kushirikiana na wawekezaji hao.
Alisema hilo ni vyema wakalishughulikia kwani linaweza kuwafanya wazanzibari wakajikuta ardhi yote imechukuliwa na wageni kutoka na kuingia nao ubia watapojaribu kufuta mikataba watapandishwa mahakamani na kushindwa kulipa fedha watazokuwa wanadai.
Akitoa maelezo yake Katibu Mkuu wa Wizara ya habari Utamaduni, Utalii na Michezo, Dk.Ali Mwinyikai, alisema atahakikisha wanalifanyia kazi suala hilo ikiwa pamoja na kuwapatia zaidi elimu wawekezaji wazalendo kufahamu haki zao na namna ya kuingia mikataba kwa kutumia njia ya kodi badala ya kukubali ubia nao.
Ni hivi karibuni tu Baraza la Wawakilishi lilipokea ripoti ya

MIAKA 30 JELA KWA KUBAKA MWANAFUNZI

Miaka 30 jela kwa kubaka mwanafunzi

Na Nalengo Daniel, Morogoro
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi mkoa wa Morogoro imemuhukumu Hashimu Nunda (50) mkazi wa Kichangani Manispaa ya Morogoro kwenda jela miaka 30, viboko 12 na kulipa fidia ya Sh. 1milioni baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza.
Hukumu hiyo ilitolewa na hakimu wa Mahakama hiyo Maua Yusuph baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao haukuacha shaka yoyote katika kuthibitisha shitaka hilo.
Akisoma hukumu hiyo hakimu Yusuph alisema kuwa ametoa adhabu hiyo kali dhidi ya mshitakiwa ili iwe fundisho na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo ambayo aliiita kuwa ni ya kinyama ya udharirishaji.
Akijitetea ili mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa huyo alidai kuwa anafamilia inayomtegemea wakiwemo wake zake wawili pamoja na wototo, ameshakuwa mtu mzima na pia ni mkosaji wa mara ya kwanza.
Hata hivyo hakimu huyo alitupilia mbali utetezi huo baada ya upande wa mashitaka kuiomba mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa kwa madai kuwa vitendo vya ubakaji vinaongezeka kwa kasi na vimekuwa vikiwadharirisha hasa watoto na kuwaathiri kisaikolojia.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka Mrakibu msaidizi wa polisi Agostino George kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 20 mwaka huu saa 12: 55 jioni katika eneo la Kichangani Manispaa ya Morogoro.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mshitakiwa akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa alimbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka nane ambaye ni mwanafunzi anayesoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mtawala baada ya kumlaghai na kumpeleka kwenye mashamba ya miwa ya Kichangani na kumbaka kisha kumsababishia maumivu makali.
Alipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alikana shitaka na hivyo upande wa mashitaka ulilazimika kupeleka mashahidi ambao waliithibitishia mahakama pasipokuwa shaka yoyote kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kama alivyoshitakiwa mahakamani hapo.

WAZIRI SHAMUHUNA NA BALOZI WA CHINA.

WAZIRI wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna, akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Qiman huko ofisini kwake Shangani mjini Zanzibar.(Picha na Zahor Suleiman).

UMEME WA JUA KUENDESHWA NA MAJI

Umeme wa jua kuendeshwa na maji

Na Zahor Suleiman
CHINA imekubali kuisaidia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutumia teknolojia ya umeme wa jua ambayo itaendesha pampu za kusukumia, kuchimba visima na ulazaji wa mabomba ya maji safi na salama kwa vijiji vya Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Qiman alipokuwa akizungumza na waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna huko ofisini kwake Shangani mjini Zanzibar.
Balozi huyo sambamba na msaada huo aliahidi Nchi yake pia kuisaidia Zanzibar katika kuipatia umeme wa teknogia hiyo kwa matumizi ya taa za barabarani kwa mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Balozi huyo alimueleza waziri Shamuhuna kwamba China itaisaidia Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na teknolojia ya habari kwa kuunganisha TVZ na matumizi ya mitambo hiyo ya umeme wa jua ili kuimarisha matangazo yake.
''Tunakusudia kuleta wataalamu wetu wa umeme huo wa jua kuendesha mitambo sambamba na wataalamu wa Zanzibar kupatiwa mafunzo ya muda mfupi nchini China kwa ajili ya kuendesha mitambo hiyo'', alisema Balozi huyo.
Nae waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ali Juma Shamuhuna, aliishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada yake mingi ya kimaendeleo kwa Zanzibar na kumuahidi Balozi huyo kutoa kila aina ya mashirikiano ili kuhakikisha mipango hiyo inafanikiwa na hatimae kuimarisha sekta hizo muhimu za maendeleo.
Mamlaka ya Maji Zanzibar inakabiliwa na changamoto mbali mbali za kuimarisha huduma za maji ikiwemo uchakavu wa mabomba na matumizi makubwa ya umeme wa kuendeshea pampu za kusukumia maji.
Zaidi ya visima vya maji safi na salama 49 vinavyohudumia Mkoa wa Mjini Magharibi pekee lakini bado upatikanaji wa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo ni kwa mgao.
Hali hiyo inasababishwa na kuharibika mara kwa mara kwa pampu za kusukuma maji kwa sababu mbali mbali za kiufundi pamoja na maji mengi kuvuja kutokana baadhi ya maeneo miundo mbinu ya kusambazia ni chakavu.

WAFARASA WAITEMBELEA IDARA YA UCHAPAJI

Wafaransa waitembelea Idara Uchapaji

Na Mohamed Mzee
UJUMBE wa watu 25 kutoka Ufaransa ukiongozwa na Marc Costantini, jana ulitembelea Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Saateni kujionea hali halisi ya mitambo na namna kampuni za Ufaransa zitakavyotoa michango yao katika sekta ya uchapishaji Zanzibar.
Ukiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni , Utalii na Michezo, Abdillahi Jihad Hassan, ambaye alikuwa ndiye Mkalimani wa lugha ya Kifaransa , Constatini alieleza kufurahiswa kwake na ziara hiyo na kusema kuwa itajenga urafiki na watu wa Zanzibar.
Alisema watakuwa mabalozi wazuri wakiwakilisha kampuni zipatazo 20 za uchapishaji nchini Ufaransa na kwamba ripoti yao itasaidia kimaeneeleo.
Aidha alimshukuru Mkurugenzi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Iddi Suleiman Suwedi na wafanyakazi wote na kusema kuwa amefarajika sana na mapokezi aliyoyapata yenye kuonesha upendo na urafiki.
Costantini na ujumbe wake waliipatia Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali shilingi 2,000,000.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali , Iddi Suleiman Suwedi, aliushukuru ujumbe huo kwa ziara hiyo na msaada walioutoa na kuwataka kujenga ushirikiano zaidi hapa Zanzibar katika sekta hiyo ya uchapishaji.
Aidha aliwaomba kuwa mabalozi wazuri nchini mwao katika kuifikiria Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kupata uwezo wa kimitambo.
Ujumbe huo umefika hapa nchini kwa ushirikiano na kampuni ya Grand Travel International(GTI) iliyopo Shangani , mjini Zanzibar.

WALIOACHA DAWA ZA KULEVYA WAPEWE TAALUMA

Walioacha dawa za kulevya wapewa taaluma

Na Zainab Jecha, MCC
ZAIDI ya shilingi milioni 12 zimetumika kwa ajili ya mafunzo maalum kwa vijana wa jumuiya inayopambana dhidi ya UKIMWI na dawa za kulevya ya ZAIDA kwa lengo la kutoa elimu ili kupunguza ya maradhi hayo.
Ofisa miradi takwimu na ufuatiliaji wa mradi wa F.H.I family health international, Mbarouk Said Ali alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema elimu iliyotolewa iliwalenga vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya, ili kuwawezesha kutambua athari zinazopatikana dhidi ya utumiaji wa dawa hizo.
Ofisa huyo alisema elimu waliyopatiwa vijana hao pia ililenga kuwapa changamoto vijana hao katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Akizungumzia changamoto inayoikabili jumuia hiyo, alisema ni pamoja na wafadhili kuchelewesha misaada na kusababisha kuzorota kwa miradi mbali mbali ya jumuiya hiyo.
Ofisa huyo alitoa wito kwa wafadhili mbali mbali kusaisaidia jumuia hiyo kwani imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tatizo la dawa za kulevya na UKIMWI linamalizika hapa nchini.
Aidha aliwataka vijana kuacha matumizi ya dawa za kulevya na kujishughulisha kazi mbali mbali za ujasiriamali ambazo zitawawezesha kujitegemea na kuondokana na umasikini.

MAONI AJALI

Tuzikomeshe ajali za barabarani

AJALI za barabarani zimekuwa zikiongezeka ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo kiasi cha watu 100 hufariki kila mwaka kutokana na ajali hizo ambazo hutokea sehemu mbali mbali nchini.
Hizo ni takwimu za vifo, lakini katika ajali hizo pia itegemewe kuwepo kwa majeruhi ambao wengine masikini hupata ulemavu wa kudumu bila ya kutegemea katika maisha yao, kweli kama hujafa hujaumbika.
Ajali zinazotokea huchangiwa kutokea kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo uzembe watumiaji barabara na uzembe wa madereva na hili linatokena na kutoeleweka kwa sheria za barabarani.
Tunakubali wapo watembea kwa miguu au waendesha vyombo vya magurudumu mawili baadhi yao hufanya uzembe na kusababisha ajali, lakini kwa kiasi kikubwa uzembe wa madereva wa gari ndio unaomaliza maisha ya wananachi.
Uzembe wa madereva hutokana na sababu mbali mbali ikiwemo wakati mwengine ulevi pamoja na shetani aliowajaa vijana ambaye huwasimamia na kuwaambia waendesha mbio vyombo hivyo.
Utashangaa vyombo vya moto kama vile pikipiki na vespa vinaendeshwa kwa mwendo wa kasi chochoroni na ikitokezea ajali ya kumgonga mtoto utasikua si makusudi.
Haikatazwi kuendesha vyombo katika mitaa yetu, lakini kwa spidi kama ya barabarani, hali unajua kuwa kutwa nzima watoto wanakwatisha njia wakiwa kwenye michezo yao.
Ajali zinazosababishwa na daladala hizo ndio hazisemeki ni za kizembe, uzembe ambao huwezi kukadiria kama unaweza kufanywa na dereva aliyefanyiwa majaribio kabla ya kupewa leseni.
Wapo madereva ambao kila siku wao wamekuwa wakikiuka sheria za barabarani hata haieleweki vigezo gani vilitumika kupewa lesini watu hawa.
Lakini wapo baadhi ya madereva walioua kwa kusababisha ajali wanaonekana mitaani wakidunda kama vile roho iliyotoka si ya binaadamu.
Suala hili ndilo linapa shida wananchi na kujiuliza, hivi hizi sheria zetu zikoje, mbona badala kulinda waliofanyiwa makosa zinawalinda waliofanya makosa.
Sisi tungependa kuona hatua zinachukuliwa katika kukabiliana na suala la ajali za barabarani ili kupunguza vifo vya watu pamoja na kupata ulemavu usiotarajiwa.
Bila shaka hilo litawezekana kama wale madereva watukutu watalazimishwa kutumia sheria za usalama barabarani.
Tunadhani hatua ya Idara ya Leseni na Usafiri ya kuwafutia leseni madereva watukutu ni miongoni mwa njia zitakazo weza kuwafanya madereva wa aina hii kufuata sheria za usalama barabarani.
Jambo jengine ambalo litaweza kupunguza ajali za barabarani ni sheria kwa dereva anayeua zirekebishwe na apewe adhabu kali.
Kwa njia hii kila dereva akishika usukani atakumbuka kuwa akiua sheria kali inamsubiri, hivyo tahadhari itakuwa kichwani mwake kila wakati kabla ya kusababisha ajali.

MASHABIKI WA SOKO WA ASERNAL

MWENYEKITI  wa ZFA Wilaya ya  Mjini  Hassan  Chura akimkabidhi Nahodha wa Timu ya Mashabiki  wa Asernal  baada ya kuifunga timu ya  Barcelona katika mchezo wa bonaza la timu za mashabiki wa timu hizi uliofanyika Uwanja wa Mao timu ya Asenal imeshinda 1-0 (Picha na Othman Maulid)

MAN UNITED MABINGWA WAPYA ENGLAND

Man. United mabingwa wapya England

LONDON, England
MANCHESTER United imetangazwa mabingwa wapya wa England, baada ya kulazimisha sare ya goli 1-1 na Blackburn Rovers kwenye dimbani la Ewood Park jana.
Sare hiyo iliiwezesha Manchester United kufikisha pointi 77 ambazo hazitaweza kufikiwa na waliokuwa wakishikilia taji hilo, Chelsea ambayo hata kama itashinda michezo yake miwili iliyobakia itafikisha pointi 76.
Chelsea leo itashuka kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Stamford Bridge kuikaribisha Newcastle United katika mchezo ambao utakuwa wa kusaka heshima na kuendelea kukaa katika nafasi ya pili.
Kipigo cha magoli 2-1 ilichokipata Chelsea dhidi ya Manchester United wiki iliyopita, kilifuta ndoto za miamba hiyo kuendelea kutetea taji hilo.
Manchester United sasa imebakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Blackpool kwenye uwanja wa Old Trafford ambao utakamalisha ligi hiyo Mei 22, kabla ya kuelekea katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona ya Hispania Mei 28, mwaka huu.
Blackburn iliwaweka roho juu mashabiki wa Manchester United kwa kufunga goli la kuongoza lililofungwa na Brett Emerton kunako dakika ya 20 huku mlinda mlango, Thomas Kuszczak, akienda sokoni.
Hata hivyo, Wayne Rooney, aliisawazishia Manchester United kwenye dakika ya 73 kutokana na mkwaju wa penalti na hivyo kushusha presha ya Sir Alex Ferguson.
Penalti hiyo ilitokana na mlinda mlango wa Blackburn, Paul Robinson, kumuangusha, Javier Herndandez, kwenye eneo la hatari na wageni kuzawadiwa penalti hiyo.
Kocha wa Manchester United, Sir Ferguson, aliwapongeza wachezaji wake kutokana na kujituma na kuweza kuibuka na ubingwa huo.
"Mchezo ulikuwa mgumu, lakini wachezaji walijituma na kupata pointi muhimu tuliyokuwa tukiihitaji", alieleza, Ferguson.
Huo ulikuwa ubingwa wa 19 kwa Manchester United na kuipiku Liverpool ambayo ilishatwaa ubingwa wa England mara 18.
Kwa matokeo hayo, Blackburn inaendelea kubakia kwenye nafasi ya 15 ikifikisha pointi 40 ambazo bado si salama kwa miamba hiyo katika janga la kushuka daraja.
Katika michezo mingine,Blackpool iliilaza Bolton magoli 4-3 huku Sunderland ikitandikwa magoli 3-1 na Wolves wakati West Brom iliilaza Everton goli 1-0.
Blackpool, Wigan na West Ham United zinaendelea kushika mkia wa ligi hiyo iliyobakisha mechi kukamilisha ratiba. (BBC Sports).

ARSENAL ZENJ WAMFUTA MACHOZI WENGER

Arsenal Zenj wamfuta machozi Wenger

Na Salum Vuai, Maelezo
TIMU ya mashabiki wa Arsenal waliopo Zanzibar, wamefanikiwa kumfuta machozi Mzee Arsen Wenger aliyeshindwa kupata angalau kikombe cha ‘babu’ msimu huu, baada ya kuibuka bingwa wa ‘Serengeti Soccer Bonanza’.
Katika bonanza hilo lililofanyika jana kwenye uwanja wa Mao Dzedong likishirikisha vikosi vya wapenzi wa klabu nane mashuhuri za Ulaya, washika bunduki hao waliifumua Barcelona kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali.
Bao hilo la ushindi lilipachikwa kimiani na Mwita Iddi Shaaban kwa shuti la adhabu lililokwenda moja kwa moja nyavuni mnamo dakika za mwisho za mchezo huo.
Kabla kutinga hatua hiyo, Barcelona iliitoa nje Chelsea kwa magoli 2-0 huku Arsenal ikiifurusha Manchester United kwa changamoto ya mikwaju ya penelti baada ya wamaume hao kumaliza dakika 14 za mchezo bila kufungana.
Kufuatia ushindi huo, Arsenal ilizawadiwa kikombe pamoja na kitita cha shilingi laki tano, ambapo Barcelona walitia mfukoni shilingi laki tatu na kikombe kidogo.
Jumla ya timu nane za Ulaya ziliwakilishwa na mashabiki wao katika patashika hiyo iliyoandaliwa na vituo vya redio vya Coconut FM cha Zanzibar na kile cha Clouds FM chenye maskani yake jijini Dar es Salaam, na kudhaminiwa na kampuni ya Serengeti pia ya Dar.
Mbali na Arsenal na Barcelona, timu nyengine kwenye kinyang’anyiro hicho zilikuwa Manchester United, Liverpool, Chelsea, Inter Milan, AC Milan pamoja na Real Madrid.
Bonanza hilo lililotanguliwa na maandamano ya timu zote yaliyoanzia viwanja vya Muembe Kisonge na kuongozwa na beni la mbwakachoka, yalivutia wapenzi wengi waliofurahia vipaji vya wachezaji wa hapa ambapo kila timu ilikuwa ikicheza na wachezaji saba kwa kutumia magoli yanayotumika kwa mpira wa mikono.

SERIKALI YASHAURIWA KUSHUSHA USHURU WA VIFAA VYA MICHEZO.

Serikali yashauriwa kushusha ushuru wa vifaa vya michezo
Na Mwantanga Ame
SERIKALI imshauriwa kushusha ushuru wa vifaa vya michezo ili kuziwezesha klabu ziliopo wilayani kumudu gharama na kuweza kufanya vizuri katika michuano mbalimbali.
Hayo yalielezwa na Meneja wa uwanja wa Amaan, Khamis Ali Mzee, hivi karibuni.
Alisema, michezo mingi imekuwa ikichezwa zaidi mjini kunakosababishwa na ukosefu wa vifaa jambo ambalo serikali inapaswa kuliangalia suala la kupunguza ushuru ili timu za vijijini ziweze kumudu gharama hizo.
Alisema mchezo wa skwash hivi sasa unawanufaisha zaidi wanamichezo wa mjini kutokana na kuwepo kwa viwanja viwili vinavyotumika kwa mchezo huo wakati vijiji kukiwa hakuna hata kiwanja kimoja.
Meneja huyo alisema kukosekana kwa miundo mbinu hiyo katika vijiji kwa kiasi kikubwa kumewafanya wakaazi wa maeneo hayo kushiriki zaidi katika mchezo mmoja na kupelekea vipaji vyengine kupotea.
Aliutaja mchezo wa mpira wa mikono hivi sasa unachezwa katika vijiji vingi kutokana na kuhamasishwa, lakini mpira wa kuchezea ikiuuzwa kwa shilingi 35,000 hadi 45,000.
Alisema hizo ni gaharama kubwa kwa wananchi wa kijijini kuweza kumudu vifaa vya michezo hivyo ni
vyema serikali ikafikiria kupunguza gharama hizo.

Tuesday, 10 May 2011

SEMINA ELEKEZI YA VIONGOZI, WATENDAJI SERIKALI YA TANZANIA.

SEMINA ELEKEZI YA VIONGOZI, WATENDAJI SERIKALI YA TANZANIA

JK: Uongozi ni kutumikia wananchi

·        Ataka viongozi wa kisiasa, watendaji kushirikiana
·        Asema ulevi, uzinzi, rushwa si sifa ya kiongozi
·        Akemea Mawaziri, Makatibu Wakuu kuficha habari
·        Aeleza kuficha habari ni kukaribisha upotoshaji taarifa
·        Aagiza maofisa habari waruhusiwe kuzungumza
·        Ataka uwajibikaji kuongezwa kufikia Vision 2025
·        Asema mafanikio MKUKUTA 1 hayaridhishi
·        Nguvu zielekezwe kurekebisha kufanikisha MKUKUTA 2
·        Abainisha umasikini bado tatizo Tanzania
·        Ataka viongozi wasibweteke maofisini
·        Watembee kuona changamoto za maisha ya wananchi
·        Asema vita dhidi ya rushwa, dawa za kulevya kuendelea
·        Viongozi kuendelea kubanwa kimaadili
·        Ataka jitihada kukusanya mapato zaidi
·        Aagiza umakini kuongezwa kuziba mianya kuvuja mapato
·        Ataka huduma za jamii kuenezwa zaidi na kuboreshwa


Na Mwandishi wetu

VIONGOZI wa kisiasa na Watendaji wa Serikali ya Tanzania, wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo wakielewa kuwa kupewa kwao vyeo ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Hayo yalielezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete, alipofungua semina elekezi kwa viongozi hao Mjini Dodoma jana.

Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na vituo mbali mbali vya televisheni na redio na kushuhudiwa na waandishi wa vyombo vya habari mbali mbali nchini, ambapo gazeti hili limefuatilia kupitia vituo hivyo, Dk.Kikwete ameeleza kwamba uwajibikaji na ushirikiano wa viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu ndiyo dira ya mafanikio na maendeleo ya nchi.

Dk.Kikwete aliwaeleza bayana viongozi hao kuwa ni lazima washirikiane ili wawe mfano wa kuigwa na wanaowaongoza huku wakielewa kuwa matumaini ya wananchi kwa Serikali yao yako katika majukumu waliyopewa wao.

Rais Kikwete aliwataka viongozi kuelewa kwamba mbali ya majukumu yao ya kikazi, pia wanalazimika kubadilika kitabia, kwani kuna baadhi ya mambo ni aibu kufanywa na viongozi wa juu Serikalini.

“Ulevi kupindukia mpaka unabebwa, uzinzi, ulaji rushwa na matusi mbele ya walio chini yako si sifa ya uongozi…….ni lazima tujiepushe na mambo hayo” alisisitiza Dk.Kikwete.

Dk. Kikwete alikemea tabia ya Mawaziri na Makatibu wakuu kukataa kutoa habari kwa vyombo vya habari nchini kuhusiana na mambo yanayohusu sekta zao, jambo ambalo husababisha upotoshwaji wa taarifa za Serikali na kukosesha wananchi fursa ya kuelewa utendaji halisi wa Serikali yao.

Kikwete aliwataka viongozi hao kuacha tabia ya kuwabana Maafisa habari wa Wizara, ambao wameajiriwa kwa lengo la kutoa habari, jambo linaweza kuwachochea kutoa habari kwa vyombo ambavyo mara zote vipo kutafuta habari hizo na baadae kuwalaumu kuwa wamepotosha.

“Mawaziri na Makatibu Wakuu mnawazuia Maafisa habari kutoa habari…….kila wakati mnataka mseme nyinyi na hapo hapo mnageuka ‘punching bag’” alieleza Rais Kikwete.

Akizungumzia umasikini nchini, Rais Kikwete amesema bado Watanzania walio wengi wanaishi maisha ya kimasikini ambapo Tanzania ni moja kati ya nchi 49 zilizo na umasikini mkubwa duniani, ambapo kupitia MKUKUTA 1 umasikini umepungua kwa asilimia 2 miaka mitano iliyopita.

Amesema katika kuongeza kasi ya kupunguza umasikini kuna haja ya hatua madhubuti kuchukuliwa kuhakikisha umasikini unaondoka zaidi kwa kurekebisha matatizo kupitia MKUKUTA 2.

Alisema juhudi zichukuliwe kufikia lengo la kuiwezesha Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya 2025.

Akitaja baadhi ya njia za kuondosha umasikini nchini, Dk.Kikwete alisema ni kuinua hali za maisha ya wananchi kwa kuwaongezea kipato na kuwawezesha kulala pazuri, kula vizuri na kusomesha watoto wao.

Nyengine alisema ni kuimarisha miundombinu na kuweka mikakati ya kuongeza ajira ili kila mmoja aweze kufanya kazi na kupata kipato, kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na umeme kwa kuisogeza karibu na wananchi na kuifanya kuwa bora zaidi.

Aliwaambia viongozi hao ni wajibu wa Serikali kuwapatia huduma bora za kijamii wananchi hivyo wanalazimika kupanga mikakati ya kuweza kufanikisha hilo kwa kila sekta kupanga mipango ya utekelezaji.

Hata hivyo alibainisha changamoto zinazoikabili Serikali katika kufanikisha hilo, ambapo alisema linategemea zaidi upatikanaji wa rasilimali fedha kwa Serikali na matumizi yake.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali alisema hali si mbaya kwa kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 500 kwa mwezi kwa wastani, lakini bado kiwango hicho hakitoshi na uwezekano wa kukusanya zaidi upo hivyo hatua zichukuliwe.

Alieleza kuwa kuna kundi kubwa lenye wajibu wa kulipa kodi ambalo halijafikiwa, pamoja na kuchukuliwa hatua zaidi za kuziba mianya inayovujisha mapato ya Serikali.

Alieleza chanzo chengine cha mapato kuwa ni misaada na mikopo kutoka Jumuiya mbali mbali za kimataifa, pamoja na nchi marafiki, ambapo huko nyuma Tanzania imepata fedha nyingi kupitia vianzio hivyo na inatarajia kupata zaidi.

Akitoa mfano alisema tayari Benki ya Dunia imepanga kuipatia Tanzania dola bilioni 2.8 kama mkopo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Semina hiyo elekezi ambayo imeshirikisha Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wa taasisi za umma na wakuu wa Mikoa na wilaya, imetoa maelekezo mbali mbali ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

Miongoni mwa mada zilizotolewa kwenye semina hiyo ni masuala ya kuendeleza uchumi, mawasiliano ya habari kwa viongozi na wananchi, hali ya usalama wa Taifa, mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya.

Wataalamu wa ndani na nje ya nchi waliwasilisha mada hizo wakiwemo kutoka Benki ya Dunia, pamoja na viongozi wengine kuelezea uzoefu wao wa utendaji Serikalini akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa.