Tuesday 17 May 2011

SEKTA BINAFSI ITEKELEZE MKAKATI WA UKIMWI

Sekta binafsi itekeleze mkakati wa UKIMWI

Na Nafisa Madai, Maelezo
SEKTA binafsi zimetakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kupambana na UKIMWI kwa kuanzisha mipango maalum ya kukabiliana na gonjwa hilo katika sehemu za kazi.
Akifungua semina ya siku moja Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Islam Seif aliwataka viongozi wa sekta binafsi kutimiza wajibu wao kwa kuwasaidia wenye kuishi na VVU na watoto wenye kuishi kwenye mazingira magumu.
Islam aliyefungua semina hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais alizitaka asasi hizo kuacha kunyanyapaa na ubaguzi kwa watu wenye UKIMWI kwani kufanya hivyo ni kinyume na katiba ya Zanzibar ambayo inakataza ubaguzi.
Alisema mkakati wa taifa uliopo ukifuatwa utasaidia kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya UKIMWI katika sehemu za kazi jambo ambalo litaiweka salama nguvu kazi ya taifa hili.
Alisema vijana ndio waathirika wakubwa wa gonjwa hili hali inayohatarisha kuzorota uchumi nchi kutokana na kupoteza nguvu kazi tegemezi ya taifa na kupoteza vipato vya watu kwa kugharamia huduma za tiba.
Islam alisema licha kuwa Zanzibar takwimu za UKIMWI ni 0.6 ikilinganishwa na nchi nyengine lakini ipo haja kupunguza idadi hiyo kutokana na idadi hiyo iliyopo kutokana udogo wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Naibu huyo alifahamisha kuwa ipo haja ya kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa maeneo ya sekta binafsi kwa kushirikiana na jumuia ya wafanyabiashara ya ABCZ.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC), alisema jamii iyashughulikie makundi maalum ambayo yako kwenye uwezekano wa kuambikizwa ikiwemo watumiaji wa dawa za kulevya, madada poa pamoja na wanaume wanaojishughulisha na vitendo vya ushoga.
Wakichangia katika semina hiyo washirikia hao walipendekeza yapo mabadiliko ya mila na desturi ndiko kunakochangia kasi ya maambikizi na kutaka sheria za uwekezaji zifuatwe.
Mkutano huo ambao una azma ya kuweka muelekeo mpya wa kimtizamo na kifikra na na misingi ya kuimarisha muitikio wa sekta binafsi katika mapambano ya UKIMWI Zanzibar imewahusisha wadau mbali mbali wa sekta binafsi wa Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment